Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Kassimu Amari Mbaraka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tanga Mjini

Primary Question

MHE. KASSIMU A. MBARAKA aliuliza: - Je, lini Serikali itafunga viti katika Uwanja wa Mpira wa Mkwakwani – Tanga kwa kuwa viti vimepelekwa na vipo uwanjani?

Supplementary Question 1

MHE. KASSIM A. MBARAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, shukrani sana. Nina maswali mawili ya nyongeza: -

(a) Je, ni lini sasa Serikali itaamua kuingia ubia na wadau mbalimbali wa michezo wenye viwanja mbalimbali ndani ya Taifa hili ili kuweza kuviendeleza, kuviimarisha na kuviboresha viwanja hivyo ili kuondoa kero na adha ya viwanja mbalimbali nchini kufungiwa mara kwa mara?

(b) Je, ni lini sasa Serikali itakuja na mpango mkakati wa kutosha ndani ya Mkoa wa Tanga tuwe na uwanja mkubwa wa kisasa wa mpira, kwa sababu mpaka sasa hivi Serikali haina uwanja wowote wa mpira mkubwa wa kisasa wenye kukidhi viwango na haja ndani ya Mkoa wa Tanga, ukiacha kituo kilichokuwepo cha TFF katika Kata ya Mnyanjani? Ni lini? Tuweze kupata majibu hayo?

Name

Hamis Mohamed Mwinjuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Kwanza ninampongeza Mheshimiwa Amari Mbunge wa Tanga Mjini kwa maswali mazuri yenye kujenga, lakini halikadhalika kwa kuendelea kuwasemea kwa sauti kubwa wananchi wa Jiji la Tanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilishaanzisha mazungumzo na Chama cha Mapinduzi ambacho chenyewe ndicho kimekuwa na viwanja vingi katika Mikoa mbalimbali nchini, ili kuona namna ambavyo tunaweza kuingia ubia kwa utaratibu unaokubalika kwa mujibu wa sheria ili Serikali iweze kuvikarabati na kuviendesha viwanja hivi na wananchi wapenda michezo nchini wapate maeneo kwa ajili ya kufanya shughuli za michezo; iwe ni aidha kwa burudani, kwa kuweka afya zao sawa, ama kama ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mazungumzo haya hayajafa, yanaendelea na tutakapokuwa na taarifa ya nini kimefikiwa, na utaratibu gani utatumika, tutakuja kwenye Bunge lako Tukufu kuwafahamisha wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali la pili kuhusu uwanja wa kisasa mkoani Tanga, ni kweli Serikali Awamu ya Sita chini ya mwanamichezo namba moja Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inafahamu haja na hamu ya wananchi wapenda michezo kote nchini kuona kunakuwa na ongezeko pamoja na uboreshaji wa maeneo mbalimbali ya michezo nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili jambo siyo kwamba tumelifumbia macho. Kwa sasa Serikali imejielekeza kwenye ujenzi wa miundombinu itakayotumika kwa ajili ya mashindano ya AFCON, ambapo tunajenga uwanja mpya wa kisasa Jijini Arusha, tunafanya ukarabati mkubwa wa Uwanja wa Benjamin Mkapa, lakini tunajenga Uwanja wa Dodoma, halikadhalika na viwanja 15 vya mazoezi, pamoja na Uwanja wa Fumba kule Zanzibar.

Mheshimiwa Naibu Spika, tutakapomaliza azimio hili la kuhakikisha tuna miundombinu sawasawa kwa ajili ya ku-host AFCON, tutajielekeza kwenye ujenzi wa miundombinu ya michezo katika mikoa mbalimbali. Serikali hivi tunavyoongea imeshaanzisha mchakato wa uanzishaji wa taasisi mahususi kwa ajili ya ujenzi na usimamizi wa miundombinu ya michezo ambayo itaitwa SIMA, na ambayo hivi karibuni pengine itakuwa tayari kuanza kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo lake ni kuhakikisha kila mkoa na kila halmashauri nchini inakuwa na miundombinu sahihi ya michezo kwa ajili ya wananchi wapenda michezo.

Name

Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Primary Question

MHE. KASSIMU A. MBARAKA aliuliza: - Je, lini Serikali itafunga viti katika Uwanja wa Mpira wa Mkwakwani – Tanga kwa kuwa viti vimepelekwa na vipo uwanjani?

Supplementary Question 2

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muda mrefu tumekuwa tukizungumzia suala la ujenzi wa arena kwenye nchi yetu na wamekuwa wanasema mchakato unaendelea. Ujenzi wa arena umefikia hatua gani ili kusaidia kazi za wasanii?

Name

Hamis Mohamed Mwinjuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza Mheshimiwa Sanga kwa swali zuri. Ni kweli tumekuwa tukijibu kuhusiana na michakato inayoendelea kuhusiana na ujenzi wa arena. Ujenzi wa arena umetengewa fedha kwenye bajeti hii, tunapata takribani shilingi bilioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa arena na ujenzi wa studio ya kisasa ya filamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizi zinatokana na mkopo wa masharti nafuu ambao umepatikana kwa benki ya Exim ya Korea na mchakato wa mwanzo wa ujenzi utaanza hivi karibuni. Kwa hiyo, hili la arena tunalifanyia kazi, na liko katika hatua za mwisho za kuanza utekelezaji wake.

Name

Rebeca Sanga Nsemwa

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. KASSIMU A. MBARAKA aliuliza: - Je, lini Serikali itafunga viti katika Uwanja wa Mpira wa Mkwakwani – Tanga kwa kuwa viti vimepelekwa na vipo uwanjani?

Supplementary Question 3

MHE. REBECA S. NSEMWA: Mheshimiwa Naibu Spika, je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kuiwezesha timu ya Taifa ya Mpira wa Pete, kwani timu hii imekuwa ikifanya vibaya sana katika mashindano ya Kimataifa, lakini pia imekuwa ikienda kushiriki katika mashindano haya ikiwa haijakaa kambi, wala haina jezi zenye nembo ya bendera yetu ya Taifa?

Name

Hamis Mohamed Mwinjuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Rebeca kwa swali zuri. Serikali imekuwa ikiigharamia mara kwa mara Timu ya Mpira wa Pete, na kama anavyosema, hatujawahi kuwa na matokeo mazuri sana katika miaka ya karibuni.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado tunaendelea na juhudi mbalimbali za kuiwezesha timu hii, na kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha tunahakikisha ya kwamba timu hii inakaa kambi na kuwa na vifaa vya kutosha na inaweza kusafiri na kuweza kuhudhuria mashindano mbalimbali kwa ajili ya kuiwakilisha nchi yetu. Bado tunafanya juhudi nyingi kuhakikisha uwezo na ubora wa timu hiyo unaimarika. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ya kwamba tutaendelea kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Pete ili kuhakikisha tunaimarisha timu hii.

Name

Ahmed Mabkhut Shabiby

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Gairo

Primary Question

MHE. KASSIMU A. MBARAKA aliuliza: - Je, lini Serikali itafunga viti katika Uwanja wa Mpira wa Mkwakwani – Tanga kwa kuwa viti vimepelekwa na vipo uwanjani?

Supplementary Question 4

MHE. YOHANA S. MSITA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Tanzania itakuwa mwenyeji wa mashindano ya AFCON na kwa kuwa Tanzania utaratibu wetu ni kuwa na wachezaji wa kigeni 12 kwenye kila timu, sasa ninataka kujua, nini mkakati wa Serikali katika kuhakikisha wachezaji wazawa wanapewa nafasi ya kucheza muda mwingi ili kuimarisha timu yetu ya Taifa?

Name

Hamis Mohamed Mwinjuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Msita kwa swali zuri. Ni kweli kumekuwa na ongezeko la wachezaji wa kigeni kwenye vilabu vyetu ambavyo vinacheza ligi kuu, lakini nimhakikishie uwepo wa wachezaji hao wa Kimataifa, moja ya mambo ambayo wamekuja kufanya ni kuongeza viwango vya ushindani na kuongeza ubora wa wachezaji wetu wa ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama unaweza kuona kwenye timu zetu kubwa, wachezaji wa ndani ambao wameweza kuwa wana uwezo wa kupata namba na kuziwakilisha timu hizi, wamekuwa wanatumika sana kwenye timu ya Taifa kwa vile viwango vyao vinakuwa vya kiushindani zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, uwepo wa wachezaji wa Kimataifa vilevile umefanya timu zetu kufanya vizuri kwenye mashindano makubwa ya vilabu Barani Afrika na hivyo vimesaidia kukua kwa kiwango cha soka letu. Kwa hiyo, kunazo juhudi mbalimbali ambazo tunaendelea kuzifanya ikiwamo mpango wa kuanzisha ligi ya wachezaji wa ndani pamoja na kuanzishwa kwa ligi ya Muungano.

Mheshimiwa Naibu Spika, halikadhalika, tunaendelea kuimarisha mashindano ya UMISSETA, UMITASHUMTA pamoja na timu zetu za vijana ili kuhakikisha tuna wachezaji wa ndani ambao wana uwezo wa kushindana kuiwakilisha nchi yetu kwenye michezo ya Kimataifa.

Name

William Kafiti Kafiti

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Primary Question

MHE. KASSIMU A. MBARAKA aliuliza: - Je, lini Serikali itafunga viti katika Uwanja wa Mpira wa Mkwakwani – Tanga kwa kuwa viti vimepelekwa na vipo uwanjani?

Supplementary Question 5

MHE. KAFITI W. KAFITI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniruhusu kuuliza swali la nyongeza. Itakumbukwa tarehe 2 Juni, 2023 Wizara ya Utamaduni na Michezo mliomba eneo katika Wilaya ya Ilemela eneo la North Buswelu kwa ajili ya kuanzisha kituo cha ufundishaji wa michezo, lakini mpaka sasa hakuna kitu kinachoendelea. Je, ni lini Serikali itatimiza maombi yake juu ya eneo hilo?

Name

Hamis Mohamed Mwinjuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu swali la Mheshimiwa Kafiti, Mbunge wa Ilemela ni kwamba kweli Serikali tarehe 2 Juni, 2023 iliandika barua kwa ajili ya kuomba eneo kutengeneza Center for Sports Excellence pale Ilemela na mpango ule haujafa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nilijibu wakati najibu kwenye swali la msingi la Mheshimiwa Amari, kwa sasa tumejielekeza kwenye ujenzi wa miundombinu itakayotumika kwa ajili ya mashindano ya AFCON. Pia Serikali inaanzisha Taasisi ya Sports Infrastructure Management Agency ambayo kazi yake itakuwa pamoja na mambo mengine kutambua, kujenga, kukarabati na kusimamia, kwa maana ya kuendesha maeneo mbalimbali ya michezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Ilemela halijatoka kwenye mipango ya Serikali, na nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Kafiti aendelee kuwa na Subira, litafikia muda wake na litafanyika tutakapomaliza programu hii ya ya AFCON.