Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Innocent Lugha Bashungwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Karagwe

Primary Question

MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA aliuliza: - Je, lini Serikali itapeleka fedha za kukamilisha ujenzi wa Mradi wa Maji wa Kayanga?

Supplementary Question 1

MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kujibu vizuri; na tunaishukuru Serikali kwa kutuwezesha kutekeleza Mradi wa Rwakajunju. Pamoja na kazi nzuri ambayo inafanywa katika mradi wa Rwakajunju, mradi wa maji Kata ya Nyakasimbi na Kata ya Chanika utekelezaji wake umesimama kwa sababu ya kutokupelekewa fedha. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha katika kata hizi ili miradi hiii iweze kukamilika?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuna miradi ilikamilika katika Kata za Nyakakika, Nyakabanga, Bweranyange, na Bisheshe, lakini miradi hii haitoi huduma kwa wananchi. Je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kufanya ziara katika Wilaya ya Karagwe ili twende kwenye kata hizi ajionee hali ilivyo, kwamba miradi imekamilika lakini haitoi huduma?

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Innocent Bashungwa kwa kazi kubwa, kwanza ya ufuatiliaji wa karibu sana wa miradi inayoendelea kutekelezwa ndani ya jimbo lake; pili, kwa ushauri ambao ameendelea kuutoa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba miradi hii inakamilika ikiwa na thamani ya fedha kulingana na ambavyo Serikali imepanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kuhusu mradi wa Chanika na Nyakasindi; bahati nzuri nilishafika katika mradi huu. Mradi huu ulikuwa na changamoto kweli, lakini baadaye tukaitatua changamoto hiyo ya kubadilisha mkandarasi; na sasa tayari tumeshafunga pump, tumeshaweka umeme, na wiki hii tunaanza testing ya kuona namna gani mradi huu unaenda kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kipengele cha pili kwa Kata ya Nyakachika pamoja na Nyakabange, kulikuwa na visima viwili. Kimoja kilikuwa kinafanya kazi vizuri, lakini kime-shake kidogo, lakini kisima kilichobaki ambacho wananchi wamelalamika maji yake yana chumvi, kwa hiyo, kusababisha wananchi kuona kwamba huduma haitolewi katika mradi huu. Sasa Serikali tumechukua hatua na wataalamu wetu kufika pale kufanya tathmini ili tujiridhishe kama tunaweza kuchimba kisima kingine ili kuhakikisha kwamba wananchi wa eneo hili wanapata huduma ya majisafi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Bweranyange ni kwamba tulikuwa na changamoto ya uendeshaji. Pale tulikuwa na CBUSO ambazo ndizo zilizokuwa zinaendesha, lakini baadaye ikabainika kwamba wananchi hawakuyatumia yale maji; na katibu ambaye ndiye Katibu wa ile CBUSO, akajikuta haoni sababu ya kufungua yale maji kwa sababu wananchi hawaendi kuchota, lakini kumbe kulikuwa na wananchi wengine walikuwa wanayahitaji yale maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tukafanya mabadiliko ya kiuongozi, tukamtoa yule katibu na sasa mradi huo unaendelea kufanya kazi, japo kuna changamoto za hapa na pale ambapo Mheshimiwa Mbunge ameomba tufike pale kuona nini kinachoendelea?

Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa zaidi, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji ninaomba nimwelekeze RM Mkoa wa Kagera aende katika miradi hii minne kabla ya mimi kwenda na Mheshimiwa Mbunge, atupatie ripoti ndani ya wiki moja ili tujiridhishe changamoto kubwa iko wapi, ili miradi hii inapotekelezwa kwa fedha za walipakodi wa Tanzania tuone inafanya kazi na inatoa maji kwa Watanzania kama ambavyo imekusudiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi la Mheshimiwa Mbunge nimelikubali, nipo tayari kuongozana naye, lakini kabla ya hapo hatutahitaji kusubiri wananchi mpaka Bunge liishe ili twende wakati kuna wataalamu wetu wapo kule. Wachukue hatua haraka. Kama kuna tatizo la kiufundi, tuweze kulitatua, na kama kuna tatizo la kinidhamu la uzembe tuchukue hatua ili wananchi waweze kupata huduma ya majisafi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana.

Name

Esther Nicholas Matiko

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tarime Mjini

Primary Question

MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA aliuliza: - Je, lini Serikali itapeleka fedha za kukamilisha ujenzi wa Mradi wa Maji wa Kayanga?

Supplementary Question 2

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria ambao unakaribia kukamilika mwaka huu Septemba kuna wananchi ambao walipisha huo mradi. Sasa ningetaka kujua hawa wananchi waliopisha mradi huu mkubwa ni lini wanaenda kulipwa fidia?

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana na ninamshukuru sana Mheshimiwa Esther Matiko, Mbunge kwa kuendelea kuwapigania. Kwanza kuhitaji wa wananchi wapate huduma ya majisafi na salama, lakini pia wale ambao wanapisha mradi wahakikishiwe kwamba wanapewa haki yao ya msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Serikali, kabla hatujalipa tunafanya tathmini na kujiridhisha wanastahili kulipwa kiasi gani? Yupi anayestahili kulipwa, na yupi ambaye hastahili kulipwa? Baada ya kujiridhisha, Serikali inakwenda kufanya malipo kulingana na haki ya kila mwananchi ambaye atakuwa sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutekeleza miradi ya maji.

Name

Eric James Shigongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buchosa

Primary Question

MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA aliuliza: - Je, lini Serikali itapeleka fedha za kukamilisha ujenzi wa Mradi wa Maji wa Kayanga?

Supplementary Question 3

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kuniona. Wananchi wa Jimbo la Buchosa walitoa 98% za kura zao kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu ya miradi ya maji ya shilingi bilioni 21. Hata hivyo, hivi sasa miradi ya maji ya Kafunzo, Iligamba, Bugoro, Lugata, imesimama kwa sababu hakuna fedha ya kukamilisha miradi hiyo. Je, Serikali italeta lini fedha ili miradi hiyo iweze kukamilika?

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana, na ninamshukuru sana Mheshimiwa Eric Shigongo, Mbunge wa Buchosa kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya katika Jimbo lake la Buchosa, na hasa katika kuwasemea wananchi wapate huduma ya majisafi na salama, na ufuatiliaji wa karibu wa miradi ambayo inaendelea kutekelezwa ndani ya jimbo lake.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa, tuna miradi inayoendelea nchi nzima, zaidi ya miradi 787 ambayo inahitaji zaidi ya shilingi trilioni 1.3. Ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba miradi hii inakamilishwa na wananchi wanapata huduma ya majisafi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, Mheshimiwa Waziri wa Maji ameelekeza wataalamu wote kutoka mikoa yote kuleta hati za madai za wakandarasi ambao inasubiri kulipwa, ili tuhakikishe kwamba wakandarasi hao wanaendelea kulipwa na wahakikishe kwamba miradi hiyo inaendelea kukamilishwa, ikiwemo miradi ya Mheshimiwa Eric Shigongo ndani ya Jimbo lake la Buchosa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimtoe hofu kwamba Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeelekeza kuhakikisha kwamba miradi hii tunaendelea kuikamilisha kwa haraka sana, lakini bila kupoteza ubora wa miradi inavyotakiwa kukamilika kwa wakati, na ikiwa na thamani ya fedha inayostahili katika miradi hiyo.

Name

Philipo Augustino Mulugo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Songwe

Primary Question

MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA aliuliza: - Je, lini Serikali itapeleka fedha za kukamilisha ujenzi wa Mradi wa Maji wa Kayanga?

Supplementary Question 4

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Wilaya ya Songwe ina Jimbo moja la Songwe na miradi yote ya Jimbo la Songwe imesimama takribani mwaka mmoja. Nini tatizo kwenye Serikali na Mheshimiwa Naibu Waziri nilishamwambia, na tumeshampelekea maandiko mengi?

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Mheshimiwa Mulugo tumekuwa tukiwasiliana naye mara kwa mara, hata Bunge lililopita, na hata katika ofisi zetu amekuwa akifika kuongelea kuhusu miradi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie kwamba, ni dhamira ya Serikali, na tuko tayari kuendelea kutoa ushirikiano kuhakikisha kwamba miradi hii ambayo imekwama na hata ile mingine ambayo Mheshimiwa Mbunge amependekeza ifanyike ndani ya jimbo lake, tunaendelea kuichakata.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika bajeti hii ya mwaka 2026/2027 tunaenda kuweka vipaumbele vya maeneo ambayo ni ya kimkakati likiwemo eneo la Mheshimiwa Mulugo ili wananchi wake wapate huduma ya majisafi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo dhamira ya Serikali, na siyo lengo la Serikali miradi kusimama. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba miradi inakamilika ili itoe huduma ya majisafi na salama. Kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge, dhamira hiyo ya Serikali iko pale pale na sisi wasaidizi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan tunaendelea kufuatilia kwa ukaribu sana ili kuhakikisha kwamba miradi hii inaenda kukamilika.

Name

Christina Solomon Mndeme

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA aliuliza: - Je, lini Serikali itapeleka fedha za kukamilisha ujenzi wa Mradi wa Maji wa Kayanga?

Supplementary Question 5

MHE. CHRISTINA S. MNDEME: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itakamilisha mradi wa maji wa Ziwa Victoria kutoka Kata ya Nkinga kwenda Kata ya Simbo Wilaya ya Igunga, kwa sababu mradi huu ulitakiwa ukamilike tangu mwezi Aprili, 2025 lakini mpaka sasa hivi haujakamilika?

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Kata za Chabutwa, Simbo, na Mwisi Wilaya ya Igunga wanapata shida sana, wakiwemo wanawake na wasichana. Ni lini mradi huu utakamilika ili mama huyu aweze kutuliwa ndoo kichwani na dhamira ya Mheshimiwa Rais iweze kutekelezwa kwa vitendo?

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na maelezo na swali ambalo ameuliza Mheshimiwa Mndeme, ameendelea kuwapambania sana wananchi, na hasa akina mama wa Tabora. Hata kabla ya leo, juzi Mheshimiwa aliweza kuwasilisha changamoto hiyo ya wananchi wa Mkoa wa Tabora hususan katika eneo la Igunga, na sisi tuliipokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge, tunaendelea kuifanyia kazi. Tunafahamu kabisa kwamba mradi huu ulitakiwa kukamilika mwaka 2025 na kwa bahati mbaya kulitokea changamoto kidogo, tunaendelea kuzifanyia kazi. Tukishakamilisha, tunaamini kwamba wakandarasi wataenda kuutekeleza mradi na kuukamilisha kama ambavyo imekusudiwa.

Name

Florent Laurent Kyombo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkenge

Primary Question

MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA aliuliza: - Je, lini Serikali itapeleka fedha za kukamilisha ujenzi wa Mradi wa Maji wa Kayanga?

Supplementary Question 6

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa nafasi. Ninaishukuru Serikali, ilianza ujenzi wa mradi wa Ziwa Victoria kwa Kata za Kashenye, Kanyigo, na phase ya pili Kata ya Bwanjai. Mradi huo umefikia 95%. Ni mwaka sasa, na ninashukuru transformer imefungwa. Je, ni lini sasa mradi huo utakamilika na wananchi wa Kata hizo za Kashenye, Kanyigo, na Bwanjai waanze kupata maji?

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru na ninamshukuru sana kaka yangu kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya na kwa kufuatilia kwa ukaribu sana, na mpaka sasa anajua tumefikia asilimia ngapi. Ni dhahiri kabisa kwamba anatambua kazi kubwa ya Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwekeza katika Sekta ya Maji na ndani ya jimbo lake ni wanufaika wa miradi mikubwa ya kimkakati na ya Kitaifa ambayo inaendelea kufanyika ndani ya jimbo lake.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimtoe hofu kama ambavyo sasa amefikia asilimia tisini na kitu, maana yake ni kwamba tumebaki kwenye vitu vidogo vidogo. Tukishakamilisha, maji yataanza kutoka kwa ajili ya wananchi wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge avute subira, ninaamini kwamba sherehe inakaribia ili wananchi wake wapate huduma ya majisafi na salama.