Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Hawa Subira Mwaifunga
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Barabara ya kutoka Kata ya Uyui - Kakola hadi Ikomwa?
Supplementary Question 1
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Pamoja na majibu ya Serikali, barabara hii inaunganisha kata tatu ambazo ni kata za pembezoni na wananchi wale wanategemea kilimo na mifugo. Barabara hii ni barabara ambayo wanaitumia zaidi kwa ajili ya kujipatia kipato kwenye maeneo yao kuja mjini kwa ajili ya kuuza mazao yao, lakini pia na mifugo yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali sasa haioni umefika wakati wa kuhakikisha wanaiboresha barabara hii ili kuwasadia wananchi wetu wa kata hizo katika majukumu yao ya kila siku?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili. Mheshimiwa Naibu Waziri, anaonaje basi baada ya kumaliza shughuli zetu za Bunge tuweze kuongozana ili akaone barabara zote za Jimbo la Tabora Mjini ambazo zinahitaji ukarabati, lakini pia, zinahitaji ujenzi, ili wananchi wetu waweze kujiinua kiuchumi kutokana na barabara hizo?
Name
Kwagilwa Reuben Nhamanilo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Handeni Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Naibu Spika, ninakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba, barabara hii inaunganisha kata tatu; Kata ya Uyui, Kakola pamoja na Ikomwa na kwamba, wananchi wa maeneo haya wanajishughulisha na shughuli za kilimo pamoja na ufugaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ni muhimu sana kwao, kwa ajili ya kupeleka mazao kwenye maeneo ya masoko na kwenda kwenye shughuli zao mbalimbali za kiuchumi, ndiyo maana Serikali kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, tumeweka mkandarasi, tayari yupo site, lakini mkandarasi huyo alikuwa na package karibia tatu, na hii ilikuwa ni ya nne. Kwa hiyo, ameshaanza kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye zile package nyingine anatengeneza makalavati eneo la Kipela, Itema na Tumbi. Anataengeneza makalavati eneo la Kiloleni kwenda Magoweko, lakini vivyo hivyo anatengeneza mifereji ya karibia mita 800 kwenye Barabara ya Magereza kwenda Timukeni. Atakapomaliza tu maeneo haya ambayo ameanzanayo atahamia kwenye barabara hii muhimu inayounganisha kata hizi tatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kuambatana na Mheshimiwa Mbunge, naomba kukujulisha, niko tayari hata sasa. (Makofi)
Name
Salma Rashid Kikwete
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Mchinga
Primary Question
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Barabara ya kutoka Kata ya Uyui - Kakola hadi Ikomwa?
Supplementary Question 2
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Awali ya yote naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu. Baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, nachukua nafasi hii kusema ya kwamba, mvua ni baraka na mvua ni neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na neema hiyo, mvua inaponyesha kwa wingi inaleta madhara katika maeneo mbalimbali nchini. Kwa hiyo, nawapa pole sana Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamekumbwa na kadhia hii, na Watanzania kwa ujumla. Sambamba na hili, nawapa pole Wanamchinga wa Jimbo zima la Mchinga ambao wamepatwa na maafa hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni kwamba, nina barabara inayotoka Kitomanga, pale Mkwajuni, kuelekea Mipingo – Nyangara. Kutokana na mvua hizi, barabara ile imeharibika yote, madaraja yote yamevunjika, na ni barabara muhimu sana kwa uchumi wa nchi kwa sababu, tunazalisha korosho na ufuta kule. Baada ya muda mfupi ufuta utavunwa. Kwa hiyo, ina maana kwamba, hatutakuwa na barabara ya kusafirisha ufuta kutoka kule unakolimwa mpaka kwenye maeneo yale.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nini mpango au mkakati wa Serikali wa haraka kuhakikisha kuwa barabara hii inatengewa fedha ya haraka, ili kuweza kuinusuru na wananchi kuleta mazao yao sokoni? Ahsante sana. (Makofi)
Name
Kwagilwa Reuben Nhamanilo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Handeni Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Barabara ya Mkwajuni – Kitomanga kwenda Mipingo imekatika katikati na maeneo haya mawili wanajishughulisha na kilimo cha ufuta kwa kiasi kikubwa, na kwamba, barabara hii wanaitegemea sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaelekeza TARURA, Mkoa wa Lindi, katika tathmini ambayo tunaendelea kuifanya nchi nzima wahakikishe wanafika kwenye barabara hii ya kutoka Mkwajuni – Kitomanga kwenda Mipingo, ili miongoni mwa maeneo watakayoyafanyia tathmini iwe ni pamoja na eneo hilo. (Makofi)
Name
Lucy Thomas Mayenga
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Barabara ya kutoka Kata ya Uyui - Kakola hadi Ikomwa?
Supplementary Question 3
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Ninafahamu kwamba, Serikali imekuwa ikifanya kazi kubwa sana, hasa TARURA, kwenye ujenzi wa barabara, lakini ninaomba kuuliza swali hili la msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo langu la Kishapu kuna Barabara ya Gimagi – Magarata yenye jumla ya kilomita 35, hali yake ni mbaya sana. Je, ni kwa vipi Serikali itakuwa na utaratibu wa kuhakikisha kwamba, barabara ambazo zina faida kiuchumi zinaanza kujengwa, lakini kwa kuzingatia wakandarasi ambao wanapewa kazi nyingi wanapunguziwa ili wafanye kazi kwa uwezo unaostahili?
Name
Kwagilwa Reuben Nhamanilo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Handeni Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itazingatia ushauri wa Mheshimiwa Mbunge ambao ameutoa, kama ambavyo ameshauri. Ni kwamba, sisi tuko tayari, kwa ajili ya kuchukua ushauri, siyo tu wa Mheshimiwa Mbunge hapa, lakini ushauri wa Wabunge wote unaotolewa ndani ya Bunge hili.
Name
Zuena Athumani Bushiri
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Barabara ya kutoka Kata ya Uyui - Kakola hadi Ikomwa?
Supplementary Question 4
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, asante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika Wilaya ya Rombo, Barabara ya Huriri – Tarakea itakamilika lini ujenzi wake kwa kuwa, juzi Waziri Mkuu alivyopita alitoa ahadi kwamba, barabara hiyo itajengwa kwa kilomita kumi na mpaka sasa mkandarasi tayari ameshasaini? Je, ni lini sasa Serikali italipa fedha, kwa ajili ya kumaliza barabara hiyo? Ahsante sana. (Makofi)
Name
Kwagilwa Reuben Nhamanilo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Handeni Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ya Huriri kwenda Tarakea tayari ina maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu, alifanya ziara kule na kutupatia maelekezo ya kuhakikisha panakuwa na mwendelezo wa ujenzi wa barabara hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwendelezo huo ulikuwa ni kwenye mwaka wa fedha huu tunaomalizia 2025/2026, na bajeti hii tunayokwenda kuipitisha. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, ujenzi wa barabara hiyo utaendelea na utafanyika kama ambavyo Mheshimiwa Waziri Mkuu ametoa ahadi.
Name
Agnesta Lambert Kaiza
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Barabara ya kutoka Kata ya Uyui - Kakola hadi Ikomwa?
Supplementary Question 5
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Ni zaidi ya miaka sita wananchi na wakazi wa Kata ya Tabata, Kata ya Kisukuru na Kata ya Kimanga wameahidiwa kutengenezewa Barabara ya kutoka Tabata Bima kuelekea Masda, barabara ambayo imekuwa ni mbovu kwa miaka mingi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa ninavyoongea barabara ile, hakuna mawasiliano kati ya hizi kata tatu, na lile daraja ambalo limekuwepo, limetitia kabisa, hakuna usafiri wala mawasiliano hata kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu kwa Serikali, nini mpango mkakati wa kutengeneza ile barabara, sawasawa na jinsi ambavyo Serikali imekuwa ikiahidi zaidi ya miaka sita?
Name
Kwagilwa Reuben Nhamanilo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Handeni Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Mkoa wa Dar es Salaam, Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inatekeleza mradi mkubwa wa kuboresha miundombinu kwa kujenga barabara zenye urefu wa karibia kilometa 250, kujenga mifereji ya maji yenye urefu wa karibia kilometa 90. Kupitia mradi huo pia, kwenye mkoa huu tutajenga masoko 18 pamoja na stendi za mabasi tisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye upande huo wa barabara ambao ameuliza Mheshimiwa Mbunge, Barabara ya Tabata – Kisukuru – Kimanga, Serikali itakwenda kuijenga barabara hii kupitia mradi wa DMDP II, kama ambavyo tumefanya kwenye wilaya na Halmashauri zote za Mkoa wa Dar es Salaam.
Name
Boniphace Mwita Getere
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda
Primary Question
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Barabara ya kutoka Kata ya Uyui - Kakola hadi Ikomwa?
Supplementary Question 6
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika Jimbo la Bunda, Barabara ya Kiroleli ya Buzume imeharibika, Barabara ya Mariwanda – Sarakwa imelimwa, lakini sasa wananchi hawapiti.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya kutoka Kambugu inayopita Malambeka imeharibika, Barabara ya kutoka Malambeka kwenda Bigevu imeharibika, na Barabara ya kutoka Nyaburundu…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, swali. Unachangia? Uliza swali moja la nyongeza.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya kutoka Nyaburundu imeharibika. Sasa lini Serikali itaenda kutengeneza barabara hizo wananchi wapite?
Name
Kwagilwa Reuben Nhamanilo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Handeni Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Naibu Spika, barabara alizozitaja Mheshimiwa Getere, Mbunge wa Bunda, ni miongoni mwa barabara ambazo zimeathirika na neema hizi za mvua ambazo tumezipata ndani ya nchi yetu. Nawaelekeza viongozi wetu wa TARURA kwa maana ya Meneja wa Mkoa wa TARURA, Mkoa wa Mara, katika tathmini anayoifanya na ambayo tunasubiri kuipata kwa nchi nzima wahakikishe wanafika kwenye Jimbo hili la Bunda na kuzifikia hizi. Siyo tu hizi ambazo amezitaja Mheshimiwa Mbunge, najua ni kwa sababu ya muda, angeweza kutaja barabara nyingi, wazifikie barabara zote ambazo zimeathirika tuweze kupata tathmini yake.