Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Juma Ramadhani Mustafa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Igalula
Primary Question
MHE. JUMA R. MUSTAFA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza ujenzi wa Daraja la Loya ili liweze kupitika muda wote na kuruhusu shughuli za kijamii?
Supplementary Question 1
MHE. JUMA R. MUSTAFA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa ninapenda niipongeze Serikali kwa kazi nzuri ambayo inaendelea kuzifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Kata ya Loya ni kata ya kimkakati kiuchumi katika Jimbo la Igalula imepakana na kata sita, lakini pia imepakana na Halmashauri ya Igunga na Halmashauri ya Ikungi Mkoa wa Singida.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali haioni haja sasa ya kupitia hizi barabara zilizopo ndani ya Kata ya Loya na kuweza kubaini maeneo korofi na ili kuweza kuyaunganisha kwenye bajeti ya ujenzi wa daraja hili, kwani tukienda kuwekeza hizi shilingi bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa daraja hili, kama kuna maeneo mengine yatakuwa hayapitiki kirahisi, hatutakuwa tumeweka tija zaidi katika uwekezaji huu ambao Serikali inakwenda kuwekeza shilingi bilioni 10.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Ni lini mkandarasi msimamizi atapatikana? Ni lini ujenzi utakwenda kuanza kwa daraja hili la Loya? Ahsante.
Name
Kwagilwa Reuben Nhamanilo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Handeni Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimejibu kwenye swali langu la msingi, tayari Serikali imeshaanza kutenga fedha, na wote tunafahamu kwamba ujenzi unakua hatua kwa hatua. Kwa hiyo, tukitenga shilingi milioni 318 kwa ajili ya kufanya usanifu, ndiyo maana tumeweza kujua gharama halisi za madaraja yote Matano; kubwa moja na yale madogo manne kwa gharama ya shilingi bilioni 26.68.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye mwaka wa fedha huu unaokuja tutakwenda kuzijenga Barabara ya Loya, lakini siyo tu barabara hiyo, kwenye jimbo la Mheshimiwa Mbunge tunakwenda kujenga Barabara ya Esuli Minyenze, vilevile Barabara ya Mwisole - Minyeze - Nyahua, Barabara ya Malongo – Mabeshi; na kwenye hilo daraja, linaunganishwa na Barabara ya kutoka Mabeshi pamoja na kutoka Miswaki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imejipanga kikamilifu kujenga barabara hizo ili wananchi wa Igalula waweze kunufaika nazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali la pili kama nilivyosema kwenye swali la msingi, tupo hatua za mwisho za manunuzi za kumpata Mhandisi Msimamizi. Muda wowote kuanzia mwezi Mei, kama nilivyosema, tutakuwa tumeshapata mkandarasi na ujenzi utakuwa unaanza.
Name
Emanuel Qambaji Nuwas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbulu Vijijini
Primary Question
MHE. JUMA R. MUSTAFA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza ujenzi wa Daraja la Loya ili liweze kupitika muda wote na kuruhusu shughuli za kijamii?
Supplementary Question 2
MHE. DKT. EMANUEL Q. NUWAS: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Mbulu Vijijini, kuna Barabara ya Geterer kupitia Hydarer kwenda Orbesh ambayo inaunganisha halmashauri tatu: Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Vijijini; Halmashauri ya Hanang; na Halmashauri ya Babati Vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna Kivuko cha Dagay au Hydarer ambacho kimekuwa kikishidwa kuhimili maji. Katika msimu huu wa mvua imesababisha kukwamisha wananchi kusafiri ikiwemo wagonjwa kwa zaidi ya mara 10, na pia maji yalipovuka yaliathiri nyumba zaidi ya 10 na kuathiri mali za wananchi. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga daraja katika eneo hilo ili kuweza kuwasaidia wananchi hawa?
Name
Kwagilwa Reuben Nhamanilo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Handeni Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ambayo ameitaja Mheshimiwa Mbunge wa Mbulu Vijijini, ni barabara muhimu kwenye eneo lile. Mheshimiwa Waziri Mkuu alifanya ziara kwenye Mkoa wa Manyara na eneo hilo la Mbulu na sisi TAMISEMI tuliambatana naye.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaielewa changamoto hiyo anayoizungumza Mheshimiwa Mbunge, na barabara hii inakwenda kwenye Hospitali ya Haydom ambayo ni Hospitali ya Rufaa, hospitali muhimu sana kwenye Mkoa huo wa Manyara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo Mheshimiwa Waziri Mkuu alishaitolea maelekezo barabara hii, tumeichukua kwenye bajeti zetu na kwa kweli inakwenda kujengwa kama ambavyo kiongozi wetu ameahidi.
Name
Arif Suleiman Premji
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtwara Vijijini
Primary Question
MHE. JUMA R. MUSTAFA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza ujenzi wa Daraja la Loya ili liweze kupitika muda wote na kuruhusu shughuli za kijamii?
Supplementary Question 3
MHE. ARIF S. PREMJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Waziri, Kijiji cha Namuhi na Kijiji cha Mnyija, katikati hapo kuna daraja ambalo limeathirika na kuharibika sana kutokana na athari za mvua na hapa tunapoongea sasa hivi wananchi wengi pamoja na wanafunzi wanapitia tabia hiyo ya hilo daraja kuvunjika. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kuwasaidia wananchi na wanafunzi hao waweze kupata hiyo access kwa ajili ya kupita?
Name
Kwagilwa Reuben Nhamanilo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Handeni Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mvua nyingi kunyesha maeneo mengi ya nchi yetu, Serikali kupitia TARURA tumeendelea kufanya tathmini ya maeneo yote ambayo yameathirika na mvua na ndani ya Serikali tunaendelea kujipanga kwa ajili ya kupata fedha ili tuweze kukabiliana na changamoto hii ya kukatika kwa barabara ambayo imeletwa na neema ya mvua.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwahakikishie Wabunge wote, maeneo yote ambayo yameathirika, Serikali inayafuatilia kwa ukaribu kwa kufanya tathmini na tunajipanga kwa ajili ya kuyafanyia matengenezo.
Name
Saashisha Elinikyo Mafuwe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hai
Primary Question
MHE. JUMA R. MUSTAFA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza ujenzi wa Daraja la Loya ili liweze kupitika muda wote na kuruhusu shughuli za kijamii?
Supplementary Question 4
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Hivi karibuni mvua imenyesha na kusababisha mafuriko Wilaya ya Hai na kufanya Mto Mbuguni ufurike maji. Wananchi wanavuka kutoka Wilaya ya Hai kwenda Simanjiro kwa kutumia boti ilhali mto ule una mamba wakali. Je, Serikali ina mpango gani angalau kwa dharura kujenga daraja la kuunganisha Kijiji cha Tindigani, Kitongoji cha Bonza na Wilaya ya Hai kwenda Simanjiro ili wananchi waweze kupata huduma?
Mheshimiwa Naibu Spika, wanafunzi sasa hivi wanavushwa kwa boti ambayo ni hatari sana. Ninaomba Serikali itupatie mpango sasa wa kujenga daraja hili.
Name
Kwagilwa Reuben Nhamanilo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Handeni Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimetangulia kujibu kwenye maswali ya nyongeza yaliyotangulia, maeneo yote ambayo yameathirika na mvua likiwemo eneo ambalo ameuliza Mheshimiwa Mbunge Saashisha linalounganisha Hai pamoja na Simanjiro, Serikali itakwenda kufanya matengenezo ili kurejesha huduma wananchi waendelee kupita kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Jimbo la Hai, mbali na dharura hii ambayo Mheshimiwa Mbunge ameizungumza hapa, Serikali inafanya kazi kubwa ya kurekebisha miundombinu ya barabara iliwemo na kutengeneza barabara ya kutoka Spencon – Mabogini – Kahe mpaka Chekereni.
Name
Mwita Mwikwabe Waitara
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Primary Question
MHE. JUMA R. MUSTAFA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza ujenzi wa Daraja la Loya ili liweze kupitika muda wote na kuruhusu shughuli za kijamii?
Supplementary Question 5
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa nafasi. Katika Jimbo la Tarime Vijijini, barabara nyingi ambazo zilipangwa mwaka wa fedha ambao tunamaliza, fedha zilikwenda TARURA. Hivi ninavyozungumza, kata zangu zaidi ya 10 hakuna mawasiliano kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumefanya tathmini, inatakiwa shilingi bilioni 2.3 ili kurejesha mawasiliano kwa wananchi. Nini mpango wa dharura wa Serikali kurejesha mawasiliano katika Jimbo la Tarime Vijijini ili kupunguza malalamiko ya wananchi wangu?
Name
Kwagilwa Reuben Nhamanilo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Handeni Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpe pole Mheshimiwa Mbunge wa Tarime Vijijini pamoja na wananchi wa Tarime Vijijini kwa adha hiyo kubwa ambayo wameipata ya kuathirika kwa barabara ndani ya kata 10. Jambo hili ni jambo kubwa. Kwa niaba ya Waziri wa TAMISEMI nimwelekeze Meneja wa TARURA mkoa huo afike maeneo yale na tupate tathmini hiyo haraka iwezekanavyo. (Makofi)