Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Chacha Mwita Wambura
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita Mjini
Primary Question
MHE. CHACHA M. WAMBURA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga na kukarabati mitaro katika Mitaa ya Mbugani na Kivukoni Geita ili kupunguza athari za mafuriko?
Supplementary Question 1
MHE. CHACHA M. WAMBURA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, ninamshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali ambayo ameyatoa, lakini pamoja na hayo ninaomba niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo haya ya Mbugani na Kivukoni ni maeneo ambayo kwa kweli yamekaliwa na wakazi wa Geita, lakini ni maeneo ambayo ni ya kibiashara, na kwa sababu hiyo, sasa ningependa kufahamu, je, Serikali haioni haja ya kuja na mpango wa dharura ili kuhakikisha kwamba tunakabiliana na changamoto hii ikizingatiwa kwamba imeshadumu kwa muda mrefu, wananchi wa maeneo haya wamekuwa wakipata hii changamoto kila mvua za masika zinapokuwa zinanyesha?
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuuliza swali dogo la pili la nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri. Ninawashukuru kwamba tulipata Mradi wa TACTIC wa barabara wenye urefu wa kilometa 17 pale Mjini Geita na barabara za nguzo mbili Mwatulole, nguzo mbili Mkolani na Nyankumbu mpaka Uwanja.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kupata mradi huu, umekuwa ukisuasua kwa muda mrefu. Mwanzoni ulikuwa uishe mwaka 2025 mwezi wa Pili, lakini mkandarasi hakuutimiza, akaongezewa muda amalize mwezi wa Kumi, lakini bado mwezi wa Kumi mkandarasi hakumaliza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningetamani kufahamu sasa, Serikali ina mpango gani na inatoa kauli gani ili kuhakikisha kwamba inamsimamia yule mkandarasi ili mwisho wa siku hii kazi iweze kwisha na wananchi wa Geita Mjini waweze kufaidika na mradi huu ambao umeletwa na umechukua muda mrefu? (Makofi)
Name
Kwagilwa Reuben Nhamanilo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Handeni Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mpango wa dharura wa ujenzi wa mitaro eneo la Mbugani na Kivukoni, eneo hili tayari upo mtaro ambao ndiyo tumebainisha kwenye tathmini kwamba unahitaji kupanuliwa, lakini maeneo ambako mtaro huu unapita wapo wananchi ambao wamejenga karibia na mtaro huu. Upanuzi wa mtaro huu utatutaka na unatulazimu kwa kweli kuwahamisha baadhi ya wananchi ambao wapo karibu na mtaro huu ili tupate nafasi ya kuupanua.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia halmashauri yetu pale Geita Mjini, mwaka wa fedha huu ambao tunapitisha bajeti yake, tumetenga shilingi milioni 200 kwa ajili ya kuhamisha wananchi hawa ambao ni kama nyumba mbili, tatu au nne hivi ili waweze kupisha na tuweze kufanya upanuzi wa mtaro huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba tunao Mradi wa TACTIC ambao ulikuwa awamu ya kwanza miongoni mwa ile miji 12 ambayo tulisaini mikataba 24 ilikuwa ni Geita Mjini. Ni kweli mkandarasi amekuwa akisuasua na Serikali iliamua kuchukua hatua kali za kuvunja mkataba ule baadaye tulipofanya mazungumzo naye ya kina, tulikubaliana mambo yafuatayo na mkandarasi huyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, tulikubaliana aongeze vifaa eneo la kazi, aongeze wataalamu eneo la kazi lakini na ahakikishe kuna flow ya fedha kwenye eneo la kazi. Siyo hivyo tu, tumekubaliana kwamba ili aendelee kukamilisha kazi hiyo, tutamkata fedha (liquidation damage) shilingi bilioni 2.2.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuwa amekubali masharti yetu, mkandarasi huyo hivi sasa ameshaanza kazi kwa kasi na anaendelea, na hata mpaka jana, alikuwa na material ya lami yanayotosha kuweka kilometa 11 zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Geita Mjini kwamba mradi huu sasa utakwenda kukamilika, na lengo la Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuweka shilingi bilioni 22 kwenye mradi huu, litakwenda kutimia.
Name
Benjamin Lukubha Ngayiwa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kahama Mjini
Primary Question
MHE. CHACHA M. WAMBURA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga na kukarabati mitaro katika Mitaa ya Mbugani na Kivukoni Geita ili kupunguza athari za mafuriko?
Supplementary Question 2
MHE. BENJAMIN L. NGAYIWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkandarasi wa ujenzi wa barabara za TACTIC pale Kahama Mjini (Sichuan) alisitishiwa mkataba wake baada ya kusuasua na kuchelewa kukamilisha mradi huo ndani ya muda. Mchakato wa kuanza kutafuta mkandarasi mpya umeanza. Sasa swali langu kwa Mheshimiwa Naibu Waziri, ni lini mchakato huo wa kumpata mkandarasi mpya utakamilika ili barabara za pale Kahama ambazo zimekuwa kero sana kipindi hiki cha mvua ziweze kuanza kujengwa?
Name
Kwagilwa Reuben Nhamanilo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Handeni Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba pale Kahama palikuwa na mkandarasi huyu huyu ajulikanaye kama Sichuan. Baada ya kuwa amesuasua kwa muda mrefu, Serikali iliamua kusitisha, na kwa kweli iliamua kuvunja mkataba. Tulivunja mkataba huo na tumeelekeza kwamba mkandarasi apatikane ndani ya mwezi mmoja na nusu toka tarehe ya kuvunjwa kwa mkataba huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Benjamin, Mbunge wa Kahama, chini ya usimamizi wa Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan barabara hiyo itakwenda kujengwa na kukamilika ili wananchi wa Kahama waweze kutumia barabara hizo.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved