Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Felista Deogratius Njau

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. FELISTA D. NJAU K.n.y. MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza:- Je, nini mkakati wa Serikali kuhakikisha Wazee wanapata huduma za afya bila kikwazo?

Supplementary Question 1

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wazee bado wanatozwa fedha wanapokwenda kupata huduma za afya licha ya Sera ya Afya kutamka kwamba wazee wapate huduma hii bure, hasa Jimbo la Moshi Vijijini na nchi nzima. Serikali haioni haja sasa ni wakati wa kutengeneza bima za dharura kwa ajili ya wazee hawa wakati wanasubiri Bima ya Afya kwa Wote kwa nchi nzima? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kumekuwa na gharama kubwa na mzunguko mkubwa kwa wazee kuelekea kwenye vituo vya afya kwa ajili ya kupata huduma, ikizingatiwa wazee wengi wamepata magonjwa mengi yasiyoambukizwa, hivyo kuwa na mzunguko mkubwa katika vituo vya afya na hivyo kusababisha usumbufu mkubwa sana. Je, Serikali haioni sasa ni wakati wa kuweka dirisha maalum kwa ajili ya wazee na wahudumu wake ili waweze kupata huduma hii kirahisi? Ahsante. (Makofi)

Name

Dr. Godwin Oloyce Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Siha

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nianze kwa kumpongeza dada yangu kwa maswali yake mazuri sana, lakini michango yake mizuri sana kwa sekta yetu ya afya kwa kipindi chote ambacho amekuwa hapa Bungeni na anayo maswali yake mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ni kuhusu suala hili la wazee. Ni kweli tunazungumzia wazee wasiojiweza, lakini kuna mtu kwa mfano, baba yake Mheshimiwa Dkt. Mollel au mwenye uwezo hata kuliko Mheshimiwa Dkt. Mollel, ambaye ni mzee wa miaka 60, huyo kwa sababu ya suala zima la bajeti, pia ukiangalia shilingi bilioni 200 tunayopitisha, tukisema tuwahudumie watu wote wasiojiweza, fedha hiyo inaweza isitoshe. Kwa hiyo, tunatumia hekima kuhakikisha wale wanaoweza kuchangia, wanachangia lakini wale wasioweza, basi wanahudumiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii siyo tu kwa group la wazee, ni pamoja na akina mama wajawazito, watoto chini ya miaka mitano na wengine ambao hawako kwenye makundi hayo lakini hawana uwezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika checks and balance, basi yule anayeweza, tunamwomba achangie, kwa sababu hata ukiangalia gharama za bei za afya kwenye nchi yetu iko chini ukilinganisha na nchi zilizotuzunguka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni nini? Serikali inachangia kwa ulipiaji, huwa ni watu wanachangia percent wakati tayari Serikali imeshachangia kiasi kikubwa, ndiyo maana gharama zetu ni ndogo ukilinganisha na wenzetu waliotuzunguka. Kwa hiyo, ninakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwa kweli tunahitaji kuongeza nguvu kwenye eneo hilo, pia baadaye kuongeza bajeti kwenye eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusu suala la kwamba wazee wasizunguke sana kwenye hospitali zetu kwenda maeneo mbalimbali; nitumie fursa hii kumtaarifu kuwa, kwa kweli tumeanza. Kwenye hospitali zetu zote tayari limeshatolewa maelekezo, na baadhi ya hospitali zetu za Mikoa, hospitali za Taifa na baadhi ya hospitali za Wilaya wanalo dirisha la wazee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kupitia swali hili kuagiza vituo vyote vya afya nchini, kuanzia zahanati mpaka Hospitali ya Taifa, pawepo na dirisha la wazee na kutengenezwa mechanism ambayo wazee hawatakiwi kuzunguka sana wakati wanapata huduma. Siyo wazee tu, na wengine wenye ulemavu mbalimbali na wengine wenye matatizo mbalimbali ambayo hayawahitaji kuzunguka. (Makofi)

Name

Hawa Subira Mwaifunga

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. FELISTA D. NJAU K.n.y. MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza:- Je, nini mkakati wa Serikali kuhakikisha Wazee wanapata huduma za afya bila kikwazo?

Supplementary Question 2

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Vifurushi vya Bima ya Afya bado vinaonesha vina gharama kubwa sana kwa wazee kuanzia miaka 60 na kuendelea. Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba wazee hawa angalau wanapunguziwa gharama za matibabu ili waweze kupata matibabu inavyostahili? (Makofi)

Name

Dr. Godwin Oloyce Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Siha

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimjibu shemeji yangu Mheshimiwa Hawa Mwifunga, na nimshukuru kwa mchango wake mkubwa kwenye eneo hili kwa kipindi chake chote alichokuwa Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba, kwanza moja kuna vifurushi ambavyo ni optional, kwa maana mtu unachagua, tusichanganye. Tunapozungumzia Bima ya Afya kwa Wote, vifurushi vilivyowekwa siyo kwa ajili ya Bima ya Afya kwa Wote, kwa hiyo, ni optional.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusisahau kwamba bima ya afya siyo mfuko wa kusaidia wasiojiweza, ni watu wanachangia fedha zao halafu ziwatibu wakati watakapokutana na matatizo ya kiafya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukigeuza bima ya afya kwamba ni mfuko wa kusaidia wasiojiweza, mwisho wa siku wewe Mbunge na wafanyakazi wa umma ambao wanachangia kwenye ule mfuko siku wanakuja kuugua wao watakuta fedha hazipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana kuna options hizi ambazo nimezungumzia hapa ambazo zimetajwa na Sera yetu ya Mwaka 2027 ya kusaidia wasiojiweza waweze kupata huduma, lakini kumbuka magonjwa haya ya kuambukiza ni gharama sana. Kwa hiyo, tunachosema alipie yule kwenye bima ambaye anaweza kulipia, asiyeweza, atapitia kwenye hili dirisha lingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, huyo wa bima atakayelipia kifurushi kidogo ambacho ana uwezo nacho, lakini ikifika mahali anatumia bima yake, anatakiwa aongeze fedha na hana fedha, bado kuna dirisha Serikali imeweka asaidiwe asiongeze fedha, bima yake ichangie kile kilichochangiwa, lakini zifuatwe procedures nyingine ili aweze kusaidiwa hizo fedha ambazo zimeongezeka pale juu. Kwa hiyo, kuna namna mbalimbali za kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukisema bima, wasipige hesabu sahihi ambayo itafanya mfuko uweze kuwa sustainable, tutarudi hapa Bungeni kwamba Mfuko wa Bima ya Afya umeingia kwenye matatizo. Bado wewe Mbunge utalaumu kwa nini mmeua bima ya afya? (Makofi)