Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Primary Question
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza: - Je, lini Serikali itaanza kusambaza maji katika Vijiji vya Hatete, Ihowa, Welu II, Ruanda na Myovizi – Vwawa?
Supplementary Question 1
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza niishukuru sana Serikali kwa kuanza kutekeleza mradi huu. Kwa kweli Serikali imefanya vizuri sana, hongereni sana. Ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza. Kwa kuwa katika eneo la intake pale pana malalamiko ya baadhi ya wananchi, lakini pia wamevamia katika maeneo yale ambapo pana intake. Je, upi mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba wanajenga wigo kwa ajili ya kulinda ile intake pamoja na kupanda miti katika maeneo yale kusudi maji yasije yakapungua siku za usoni?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa tanki moja la lita 2,000 ni dogo sana ukilinganisha na ukubwa wa vijiji na umbali wa vijiji vilivyopo, je, upi mpango wa Serikali wa kuhakikisha kwamba mnajenga matanki mengine katika kila kijiji kusudi wawe na uhakika wa upatikanaji wa maji?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na ninamshukuru sana kaka yangu Hasunga. Kwanza kwa niaba ya Serikali ninapokea pongezi zako na hizi maana yake ni pongezi za wananchi wake. Tunampongeza pia Mheshimiwa Hasunga kwa kazi nzuri anayoifanya kwa wananchi wake na tunampongeza kwa kuendelea kushirikiana na Wizara ya Maji ili kuendelea kutatua changamoto za maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria namba Tano ya Mwaka 2019 inawapatia mabonde. Kuna Bodi za Mabonde ambazo majukumu yake ni kulinda vyanzo vya maji, na pia kuendeleza kuhakikisha kwamba hatuwi na changamoto katika vyanzo vyetu vya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hii intake kama kuna malalamiko ya wananchi na kuvamia, sisi kupitia mabonde tutahakikisha kwamba kwa kushirikiana na Serikali ya Wilaya tunajenga ili kuhakikisha kwamba kusiwe na changamoto wakati wa kutatua changamoto nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, lengo ni kwamba, vyanzo vilindwe, lakini na wananchi wasikilizwe kuangalia malalamiko yao yapo na base ipi ili kuleta maridhiano ambayo hayatakuwa na changamoto katika Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa tanki hili la lita 200,000, ni kwamba, tunapofanya usanifu wa miradi tunaangalia mahitaji ya wananchi katika eneo husika; na tunapoona kwamba mahitaji, hatuwezi kujenga tanki kubwa wakati tunajua kabisa mahitaji yanahitajika kwa kiasi fulani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaendelea kupokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge. Kulingana na sensa ya watu na makazi na ongezeko la watu, tutajaribu kuwa proactive kuangalia ongezeko hilo kama litaathiri upatikanaji wa maji kulingana na tanki ambalo tulikuwa tunalijenga. Kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge, hilo tutalizingatia sana na tunaupokea ushauri wako kama Serikali. Ahsante sana.
Name
Francis Kumba Ndulane
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilwa Kaskazini
Primary Question
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza: - Je, lini Serikali itaanza kusambaza maji katika Vijiji vya Hatete, Ihowa, Welu II, Ruanda na Myovizi – Vwawa?
Supplementary Question 2
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kijiji cha Kinjumbi Kata ya Kinjumbi, Jimboni Kilwa Kaskazini Serikali ilianza kutekeleza mradi wa maji wa kisima kirefu tangu mwaka 2021. Je, ni lini Serikali itakamilisha mradi huu wa kimkakati katika Kata ya Kinjumbi ili kuwatua wakina mama ndoo kichwani na kuhakikisha kwamba maji safi na salama yanaweza kupatikana?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na ninamshukuru sana kaka yangu, kwa kweli amekuwa akiusemea sana mradi huu. Nimtoe hofu, na ninaomba nilipokee kwa ajili ya kulifuatilia na ili tutoe majibu ya uhakika kwa wananchi wake.
Name
Jonas William Mbunda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbinga Mjini
Primary Question
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza: - Je, lini Serikali itaanza kusambaza maji katika Vijiji vya Hatete, Ihowa, Welu II, Ruanda na Myovizi – Vwawa?
Supplementary Question 3
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilitoa shilingi 1,800,000,000.00 kujenga mradi wa maji katika Kata ya Mbangamao iliyopo katika Mji wa Mbinga. Mradi ule ulikamilika na ukaanza kutoa maji, lakini una changamoto kubwa sana. Wananchi bado hawapati maji safi na salama kama inavyotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba wananchi wale wanapata maji na mradi ule unarekebishwa ili wananchi waendelee kupata maji? (Makofi)
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na ninamshukuru sana Mheshimiwa Jonas Mbunda na ninamshukuru pia kwa kutambua uwekezaji mkubwa sana wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika eneo la Mbangamao ndani la Jimbo lake la Mbinga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutatuma timu ya wataalamu. Sisi Wizara ya Maji tunayo taasisi ambayo inashughulika na kupima ubora wa maji na usalama wa maji. Lengo ni kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, tutatuma timu yetu ya wataalamu wakachunguze na kujiridhisha kama hayo maji yana changamoto ya kiusalama, basi tutachukua hatua stahiki. Lengo ni kwamba wananchi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na wananchi wa Mheshimiwa Jonas Mbunda wapate huduma ya maji safi na salama.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved