Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Primary Question

MHE. FESTO R. SANGA aliuliza: - Je, lini ujenzi wa Barabara ya Usalimwani - Ikuwo hadi Nkenja kwa kiwango cha changarawe utaanza?

Supplementary Question 1

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nichukue nafasi hii kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Makete, hususan wananchi wa Kata hii ya Ikuwo pamoja na Kata ya Mfumbi kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa ambayo wameifanya ya kujenga barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ilikuwa ni barabara yenye changamoto kubwa sana, lakini tulipoomba kuipandisha isimamiwe na TANROADS, wakapokea na wakaitengea fedha kwa ajili ya kuijenga na imejengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii barabara hii imetumika kama mbadala. Unajua changamoto ya barabara kutoka Makete kwenda Mbeya, barabara hii ndiyo imetumika mbadala sasa hivi kuisaidia Wanamakete. Kwa niaba ya wananchi wa Makete na kwa niaba ya Serikali ya Makete nichukue nafasi hii kupongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina swali moja tu kwa Mheshimiwa Waziri. Barabara kutoka Lupila – Kipengele kilometa 42 tuliwaomba waipandishe kwenda TANROADS, na ninashukuru waliipandisha kwenda TANROADS. Tangu tarehe 12 mwezi wa Saba mwaka 2024 leo hii tunaizungumza ni tarehe 25 barabara hii haijaanza kujenga. Je, ni lini barabara hii itajengwa ili iwasaidie wananchi wa Lupila, Kipengele katika shughuli zao za kiuchumi kwa sababu ni barabara ya kimkakati?

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya barabara hii kupandishwa hadhi, sasa tumepata bajeti ya kuijenga. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Makete kwamba mwaka huu wa fedha, barabara hiyo kwanza baada ya kupandishwa hadhi itaongezwa upana, itakarabatiwa madaraja na pia itajengwa kwa kiwango cha changarawe, kwa maana ya standard ya barabara zetu za TANROADS.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri wa Fedha.

WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa. Nimesimama kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge, kwa sababu alinifuata mara kadhaa ofisini kufuatilia fedha za barabara ile ya kwanza ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri amejibu pamoja na hii, nimhakikishie kwamba, hata baada ya Bunge kuvunjwa, maombi yake aliyoyaleta kwa ajili ya wananchi wa Kata hizi alizozisema yataendelea kutekelezwa kwa fedha kwenda kwenye miradi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nilisema jana wakati nahitimisha, kwamba Waheshimiwa Wabunge ambao wameleta maombi yao kwa ajili ya miradi iliyoko majimboni mwao itaendelea kutekelezwa hata wakati uchaguzi inaendelea; na inshallah watakapomrudisha tena wakati anaapa atapita kwenye barabara hiyo ikiwa imeshatengenezwa.