Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Josephine Johnson Genzabuke
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga Barabara ya kutoka Kasulu hadi Uvinza kwa kiwango cha lami?
Supplementary Question 1
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa ujenzi wa barabara unaoendelea ndani ya Mkoa wa Kigoma. Swali langu la kwanza, je, ni lini sasa ujenzi wa barabara hiyo utaanza?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili. Ni lini Serikali itajenga Barabara ya kutoka Simbo mpaka Kalya kwa kiwango cha lami? (Makofi)
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Uvinza kwenda Kanyani ni muhimu, ni kati ya barabara kuu. Tayari tumeshakamilisha usanifu, na ndiyo kipande pekee kitakachokuwa kimebaki katika Mkoa wa Kigoma, barabara kuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mambo mawili ambayo tunayafanya. Moja ni kutafuta fedha za ndani kujenga hicho kipande cha kilometa 60, lakini pia, yapo mazungumzo ambayo yanaendelea na Benki ya Maendeleo ya Afrika, ambao wameonesha uwezekano wa kuweza kutoa fedha, ili tuweze kuijenga hiyo barabara kwa mkopo nafuu. Kwa hiyo, Serikali inaifanyia kazi kwa kiasi kikubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Barabara ya Simbo kwenda Kalya. Barabara hii najua ina changamoto kubwa, na Serikali baada ya kuona ina changamoto kubwa, hasa kwenye Mto Malagarasi, tunachofanya mwaka huu, 2025, ni kufanya ujenzi wa Daraja la Mto Malagarasi, ambapo kuna kivuko. Ndiyo imekuwa changamoto kubwa, na tayari usanifu umekamilika, tupo kwenye hatua za mwisho na wenzetu wa World Bank kulijenga hilo daraja wakati tukifanya maandalizi ya kuijenga hiyo barabara yote kwa kiwango cha lami kutoka Simbo hadi Kalya, ahsante.
Name
Mwita Mwikwabe Waitara
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Primary Question
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga Barabara ya kutoka Kasulu hadi Uvinza kwa kiwango cha lami?
Supplementary Question 2
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, tunamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kutupatia barabara ya kutoka Tarime Mjini mpaka kule Serengeti, Mugumu na imeanza kujengwa kilometa 25. Tayari kilometa 10 wananchi wanatumia barabara ya lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni kwamba, Mkandarasi kipande ambacho kimebaki aliingia site, halafu ameondoka, mvua inanyesha, magari hayapiti. Nini kauli ya Serikali kwa sasa, ya dharura, ili wananchi waweze kutoka Nyamongo kwenda mjini na Mugumu, Serengeti, bila ya usumbufu? Ahsante.
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa maelekezo kwa Meneja wa Mkoa wa Mara kuhakikisha kwamba, Mkandarasi huyu anarudi site kuhakikisha zile njia za mchepuko, kwa maana ya diversion, anazitengeneza, ili watu wa Tarime, Nyamwaga hadi Nyamongo waweze kufanya shughuli zao za kimaendeleo na kijamii bila matatizo, kwa sababu, mkataba unamwambia mkandarasi aliyeko site ni lazima ahakikishe barabara ambayo anaifanyia kazi inapitika, ahsante.
Name
Deo Kasenyenda Sanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makambako
Primary Question
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga Barabara ya kutoka Kasulu hadi Uvinza kwa kiwango cha lami?
Supplementary Question 3
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa, barabara ya kutoka Kibena - Lupembe hadi Madeke, Mbunge wa eneo hilo Mheshimiwa Swalle, amekuwa akiulizia kila wakati. Ni lini barabara hii itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami?
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli barabara ambayo inatoka Njombe, kwa maana ya Kibena Junction, Madeke, Mlimba hadi Ifakara, tumeshaanza kuijenga kwa upande wa Ifakara. Kwa upande wa kutoka Njombe - Kibena - Lupembe hadi Kidigembe, yalikuwa pia ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais. Kilometa 40 tayari ipo kwenye hatua za manunuzi, ili ianze kujengwa kwa awamu, ahsante.
Name
Subira Khamis Mgalu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga Barabara ya kutoka Kasulu hadi Uvinza kwa kiwango cha lami?
Supplementary Question 4
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa na mimi kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa, hali ya barabara ya Makofia, - Mlandizi - Nzenga mpaka Vikumburu kwa sasa kutokana na mvua zilizonyesha ni mbaya sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, tuna matumaini ya kwamba, barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami, je, Serikali inatupa matumaini gani mapya ya barabara hii kujengwa kwa kiwango cha lami pamoja na kuhuisha fidia ya maeneo ya Makofia - Mlandizi na Nzenga? Ahsante sana.
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Makofia hadi Mlandizi, barabara ilishafanyiwa usanifu, na tayari tunasubiri wenzetu wa Hazina kuweza kutoa fidia, ili kazi ya ujenzi ianze kujengwa. Kutoka Mlandizi – Mzenga kwenda Vikumburu, kwanza ipo kwenye bajeti kwa maana ya kuanza ujenzi, lakini kipande ambacho kinakwenda kutoka Mlandizi hadi kwenye Reli tayari tumeshatangaza zabuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwelekeza tu Meneja wa Mkoa wa Pwani kwamba, kama mvua imeshakatika, ahakikishe kwamba, barabara hiyo inatengenezwa ili iweze kupitika wakati tunasubiri kuanza kwa ujenzi wa lami kwa vipande ambavyo tutaanza mwaka huu wa fedha, 2025/2026, ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved