Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dr. Charles Stephen Kimei
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vunjo
Primary Question
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI K.n.y. MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza:- Je, lini Serikali itatenga bajeti ya ujenzi wa barabara za lami katika mitaa ya Namtumbo?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mheshimiwa Vita Kawawa amefurahia na anaishukuru Serikali kwa kazi nzuri waliyofanya katika Jimbo lake. Pamoja na kufurahia yeye, mimi naomba kupachika hapo swali langu la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchukua fursa hii kuishukuru TARURA kwa kuweza kuweka taa kwenye Mji wa Himo, taa kama thelathini hivi, nashukuru sana. Naomba kumwuliza Mheshimiwa Waziri kwamba barabara hii ya Uchira – Kisomachi anaifahamu sana, tulikuwa tumeahidiwa kwamba wangekamilisha ujenzi wa kilometa 2.8 kwa kiwango cha lami katika kipindi hiki, lakini juzi nimepita kule bado yule mkandarasi hajafanya chochote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Naibu Waziri tutegemee nini au una kauli gani kuhusiana na suala hili? (Makofi)
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Charles Kimei amekuwa akifanya ufuatiliaji wa karibu kabisa wa barabara hii ya kutokea Uchira yenye urefu wa kilometa 2.8 ambayo ipo katika Mji wa Himo, na tayari tumeshakaa naye. Alifika ofisini; Ofisi ya Rais, TAMISEMI na tukazungumza na kukubaliana kimsingi kuhusiana na ukamilishaji wa ujenzi wa barabara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali itahakikisha barabara hii inajengwa, ila nitumie nafasi hii kumkumbusha Meneja wa TARURA wa Mkoa na wa Wilaya waweze kufanya usimamiaji na ufuatiliaji wa karibu kuhakikisha kwamba mkandarasi aliyepewa kazi ya ujenzi wa barabara hii anaweza kutimiza wajibu wake kwa mujibu wa mkataba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ile ratiba iliyowekwa ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara hii iweze kusimamiwa ili barabara hii iweze kukamilika kwa wakati na iweze kuwanufaisha wananchi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge Serikali itafanya ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha barabara hii inakamilika iweze kuwa na manufaa makubwa kwa ajili ya wananchi wako. (Makofi)
Name
Maimuna Salum Mtanda
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Newala Vijijini
Primary Question
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI K.n.y. MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza:- Je, lini Serikali itatenga bajeti ya ujenzi wa barabara za lami katika mitaa ya Namtumbo?
Supplementary Question 2
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipatia nafasi. Ni lini Serikali itatenga bajeti kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ambazo zinapita milimani katika Jimbo la Newala, hasa kutoka Mikumbi kwenda Mpanyani, Mkomatuu kwenda Chimemena, na Lihanga kwenda Chikalule? (Makofi)
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Sita imefanya na inaendelea kufanya uwekezaji mkubwa sana katika kuimarisha miundombinu ya barabara zetu hizi za wilaya zinazosimamiwa na TARURA. Pia, utaona kwamba katika kipindi hiki cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita bajeti ya TARURA imeongezeka mara dufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2020/2021, bajeti ya TARURA ilikuwa ni shilingi bilioni 275 kwa mwaka, lakini muda huu tunavyozungumza mwaka wa fedha 2025/2026, bajeti ya TARURA itakuwa ni shilingi trilioni 1.18.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ongezeko hili la bajeti linaonekana katika kila wilaya. Kila wilaya imepata ongezeko la bajeti kwa ajili ya kuhakikisha miundombinu muhimu kabisa ya barabara hizi za wilaya inaendelea kuimarika. Kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Maimuna Mtanda kwamba barabara hizi alizozitaja ambazo ni za milimani katika Jimbo la Newala zitafikiwa na Serikali na zitakuja kujengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwakumbushe Mameneja wa TARURA ngazi ya Mkoa na Meneja wa TARURA Wilaya waweze kufanya tathmini na waweke katika mipango ili ziweze kujengwa barabara hizi, kwa maana zitengewe bajeti ziweze kujengwa barabara hizi na ziweze kuwanufaisha wananchi wa Newala. Mheshimiwa Maimuna Mtanda, Serikali inakuja kujenga barabara hizi ulizozitaja.
Name
Nicodemas Henry Maganga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbogwe
Primary Question
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI K.n.y. MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza:- Je, lini Serikali itatenga bajeti ya ujenzi wa barabara za lami katika mitaa ya Namtumbo?
Supplementary Question 3
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza Naibu Waziri ninawashukuru TARURA jinsi mnavyofanya kazi. Swali langu la msingi, makao makuu ya Wilaya ya Mbogwe yako Kasosobe Bwerwa pale. Tuna jengo pale la halmashauri, lakini pia hata nyumba za watumishi zipo pale Makao Makuu ya wilaya mpya. Ni lini Serikali itatoa fedha ili angalau tuweke kilometa tatu za lami katika eneo lile? (Makofi)
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaipokea pongezi za kutoka kwa Mheshimiwa Nicodemas Maganga kuja TARURA. Pili, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kipaumbele kikubwa cha Serikali ni kuhakikisha kwamba kwenye makao makuu ya wilaya barabara za lami zinajengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nimhakikishie kwamba, katika makao makuu ya wilaya hii na hasa katika eneo lile la Kasosobe tayari Serikali imeweka katika mipango na bajeti kwa ajili ya ujenzi wa barabara hizi katika eneo hilo kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, eneo hili linakuja kujengwa lami kwa ajili ya kuwanufaisha wananchi wake. (Makofi)
Name
Hussein Nassor Amar
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nyang'hwale
Primary Question
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI K.n.y. MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza:- Je, lini Serikali itatenga bajeti ya ujenzi wa barabara za lami katika mitaa ya Namtumbo?
Supplementary Question 4
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa Serikali ilitujengea kilometa moja ya lami makao makuu pale Kalumwa, na nimewahi kukuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba ni lini tutajengewa mitaro kwa sababu ile kilometa moja kuna nyumba pembezoni, inaponyesha mvua, maji yale huwa yanaenda kuharibu mali za watu ndani ya majengo hayo. Ni lini sasa utatoa fedha hizo ili mitaro hiyo iweze kujengwa? (Makofi)
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaweka kipaumbele kikubwa sana katika kuhakikisha inapojenga barabara, hizi barabara tunazozijenga zijengwe pamoja na mitaro na ziwekewe na taa juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la msingi la ujenzi wa mitaro ni kwa sababu maji ni adui namba moja wa barabara zetu hizi. Kwa hiyo, ili barabara zetu ziweze kuishi kwa muda unaokubalika, tunatengeneza mitaro ili ku-drain maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tayari Serikali ilifika ikaanza ujenzi wa barabara katika makao makuu ya wilaya kwa kilometa moja, na tayari tumeweka katika mipango na bajeti ujenzi wa mitaro ili kuhakikisha barabara hiyo inakuwa na mitaro, lakini mwisho wa siku pia inakuwa ina taa juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba nimwambie Mheshimiwa Hussein Amar, Serikali itafika kwa ajili ya kuhakikisha inaimarisha miundombinu ya barabara hii. (Makofi)