Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Festo Richard Sanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makete
Primary Question
MHE. FESTO R. SANGA K.n.y. MHE. ZUENA A. BUSHIRI aliuliza:- Je, lini skimu ya umwagiliaji itajengwa katika Kata ya Arusha Chini Moshi Vijijini?
Supplementary Question 1
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa sababu ni katika kipindi hiki Serikali imewekeza fedha nyingi sana katika sekta ya umwagiliaji. Hii ni kuonyesha kwamba Serikali imekusudia kufanya mapinduzi kwenye sekta ya kilimo. Nina maswali mawili.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, wananchi hawa wa Kata ya Arusha Chini wamekuwa wakisubiria sana hii skimu kuanza, kwa sababu kama unavyojua, Arusha ni moja kati ya mikoa ambayo uzalishaji wa mbogamboga ndiyo unaoendesha maisha ya kila siku. Sasa wanaiuliza Serikali, ni lini wataanza kuijenga skimu hii ili wananchi waweze kupata fedha?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili. Ni kwa ajili ya wananchi wa Jimbo la Makete Kata ya Mfumbi Skimu ya Mwamlenge tumewaomba shilingi bilioni 1.4 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa skimu hii ili iweze kufanya kazi kwa hekta 520. Je, ni lini Serikali itatoa fedha hizi ili wananchi hawa waweze kupata maji na kufanya kazi kwenye skimu hii katika uzalishaji wao wa shughuli za kiuchumi? (Makofi)
Name
Maryprisca Winfred Mahundi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI K.n.y. WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninampongeza sana Mheshimiwa Festo Sanga kwa maswali yake ya kizalendo. Mapinduzi katika sekta ya kilimo hakika yapo bayana. Tuna kila sababu ya kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, vilevile kumpongeza Mheshimiwa Waziri Bashe pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri wake Mheshimiwa Silinde.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza kwenye jibu langu la msingi, mwaka huu upembuzi yakinifu umefanyika na mwaka ujao wa fedha 2025/2026 tunatarajia tuweze kukamilisha kazi hii ya ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kwenye Skimu ya Mwamlenge katika Jimbo lake, mara Serikali itakapokamilisha taratibu zote hizi, skimu zote tunazitarajia mwaka ujao wa fedha ziweze kujengwa. Lengo kubwa ni kuendeleza mapinduzi ya kilimo na kuhakikisha wakulima wote nchini wananufaika na kazi nzuri inayofanywa na Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved