Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Oran Manase Njeza
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbeya Vijijini
Primary Question
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, je, Serikali inaonaje umuhimu wa kuchukua mikopo kwenye taasisi mbalimbali ili waweze kuwafungia wananchi ambao hawana uwezo wa kulipa kwa mkupuo mmoja shilingi 320,000.00 mpaka 350,000.00, halafu baadaye wakaweka kwenye gharama za kutoa umeme kwa hawa wateja wakawa wanalipa kidogo kidogo? Je, Serikali inasemaje kuhusu hoja hiyo. (Makofi)
Supplementary Question 1
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwa kuwa, Bandari yetu ya Dar es Salaam inafanya vizuri, na magari ya mizigo ikiwemo ya mafuta yameongezeka sana kwenye barabara hiyo ambayo inapita katikati ya jiji, je, sasa ni lini wananchi waliopisha ujenzi wa hiyo barabara wakiwemo wa Kata ya Inyala, Kata ya Ijombe, Kata ya Swaya, Kata ya Igale, Kata ya Lwindi na Kata ya Bonde la Songwe watalipwa fidia?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa kipande cha kilomita 22 wa barabara ya Isyonje – Kikondo?
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI K.n.y. WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru Mheshimiwa Oran Njeza kwa maswali yake ya nyongeza mawili ambayo ameyauliza ambayo kimsingi yanasadiki umuhimu wa barabara yetu hii kubwa katika kusaidia Bandari yetu ya Dar es Salaam na kuinua sekta ya uchukuzi nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, amezungumza kuhusiana na upande wa fidia. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hiyo, uthamini umekamilika kwenye barabara ya Mbeya bypass na tayari tumeshaanza kulipa fidia. Tumelipa shilingi bilioni 10 kwa ajili ya wananchi wa maeneo hayo. Hivyo, nawaomba wananchi wote wanaonisikiliza wa Kata alizozitaja ikiwemo Kata ya Ijombe, Swaya, Igale, Lwindi na Songwe kwamba Serikali inaendelea kutafuta fedha na inao mpango wa dhati wa kuwalipa fidia ili wapishe eneo hilo au eneo hilo liende kutumika kwa ajili ya barabara yetu ambayo tumeizungumza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia amezungumza kuhusu jambo la pili barabara ya Isyonje – Kikondo kilomita 22 hadi Makete kwamba ni lini pengine ujenzi wake utakamilika? Nimpe uhakika Mheshimiwa Mbunge pamoja na Waheshimiwa Wabunge wa Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama tunavyofahamu mpaka sasa Serikali imekamilisha ujenzi wa kilomita za lami zaidi ya 12,000 na katika Awamu ya Sita peke yake; miaka minne zaidi ya asilimia 10, zaidi ya kilometa 1,300 barabara za lami zimejengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi, kutokana na umuhimu mkubwa wa barabara hii aliyoizungumza, inayounganisha Mikoa miwili katika Mkoa wa Njombe pamoja na Mkoa wa Mbeya, tayari usanifu wa kina umeshakamilika na ujenzi umeshaanza kuanzia kwenye Mkoa wa Njombe.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwape matumaini wananchi wa Mbeya na watu wa mikoa yote hii miwili na maeneo mengine kwamba tunakwenda kujenga barabara hiyo kama ambavyo tumekuwa tukiwaeleza, kwa sababu tayari kazi imeshaanza.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved