Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Tamima Haji Abass

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. TAMIMA HAJI ABASS aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani wa kutoa elimu kwa wajasiriamali wadogo ili kuwawezesha kuwa na vifungashio bora vya bidhaa zao? (Makofi)

Supplementary Question 1

MHE. TAMIMA HAJI ABASS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa vifungashio duni vinashusha hadhi ya bidhaa na pia huhatarisha usalama wa chakula. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuwashajiisha wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo wadogo walioko vijijini ili kuweza kutumia vifungashio bora? Ahsante. (Makofi)

Name

Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana, kwanza, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Tamima kwa ufuatiliaji na hasa kwenye sekta hii ya biashara na hasa kwa wajasiriamali amekuwa akifuatilia sana na kuwasemea, lakini zaidi nishukuru kwa sababu anatuongezea kuhakikisha tunaboresha huduma kwa wajasiriamali na hasa kwenye vifungashio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake, ni kweli vifungashio duni au ambavyo havina ubora vinapunguza ubora na ushindani wa bidhaa zetu na hasa za wajasiriamali. Sasa ametumia Kiswahili kizuri kwamba kwa nini tusiwashajiishe wajasiriamali, ninadhani anamaanisha tuendelee kuwafahamisha au kuwafundisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba kazi kubwa tunayofanya sasa na haya ni maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha bidhaa zetu au wajasiriamali au sekta binafsi ya ndani inakuwa shindani. Kwa hiyo, kupitia SIDO tunafanya kazi hiyo, kuwasaidia; kwanza, kuwafundisha lakini pili, kuwasaidia kutengeneza kama nilivyosema vifungashio hivyo vikiwa na ubora lakini pia kuweka label kwa sababu wengine walikuwa wanatengeneza vifungashio vile bila kuonesha kwamba imetengenezwa na nani na wapi, lakini pia kuwa na rangi kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaendelea kuusimamia ubora wa vifungashio ili kweli bidhaa zao ziweze kuwa na ubora, kwa sababu unavyofungasha bidhaa ndiyo itaonesha ubora wa bidhaa iliyo ndani kutokana na kifungashio ambacho umekitumia, nakushukuru sana. (Makofi)

Name

Asha Abdullah Juma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. TAMIMA HAJI ABASS aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani wa kutoa elimu kwa wajasiriamali wadogo ili kuwawezesha kuwa na vifungashio bora vya bidhaa zao? (Makofi)

Supplementary Question 2

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ni kweli SIDO wanatengeneza vifungashio vilivyo bora, lakini nini mkakati wa Serikali kuunganisha juhudi zake pamoja na Shirika la Viwango, kwa sababu vifungashio vinaweza kuwa bora, lakini zile contents zinapimwaje, kwa sababu nyingi ni za vyakula. Sasa Serikali mnafanya nini kuunganisha juhudi zenu na TBS kuwafahamisha kwamba hawa watu wana umuhimu pia hivyo wanavyovitia ndani vikapate ubora na kuhakikishwa na TBS?

Name

Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana, pia nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Asha Abdullah Juma kwa swali hili zuri, lakini na yeye amekuwa mdau mkubwa sana hasa kwenye sekta ya ubora wa bidhaa zinazozalishwa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali tuna mkakati maalum na hasa hili tunalisema kwa sababu bahati nzuri taasisi alizozitaja zote ziko chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara, SIDO na TBS kuna mkakati maalum ambao unatumika, kwanza kwa kuwatengea fedha wajasiriamali wadogo zaidi ya milioni 350 katika bajeti ya mwaka tunaweka kwa ajili ya wajasiriamali. Na mambo mengine ambayo yanaangaliwa ni ubora wa bidhaa ikiwemo na hizi za vifungashio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kwamba Serikali inafanya kazi kubwa kuhakikisha ubora wa bidhaa lakini pia na vifungashio unasimamiwa na TBS kwa kushirikiana na SIDO ili kuhakikisha yale mafunzo na bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali zinakidhi ubora na zinakuwa shindani.