Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Primary Question

MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA aliuliza: - Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa kiwanja cha michezo (centre of excellence) Manispaa ya Ilemela chenye hekari 16.75 ambacho kina hati tayari?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na nishukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na nimpongeze sana Mheshimiwa Rais ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha michezo inainuka na tumepata pia fursa ya kuwa wenyeji wa michezo ya AFCON. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatambua dhamira njema ya Serikali ya kutaka kuendeleza michezo hasa kwa kuwa na hizi akademia za michezo, mojawapo hiyo ya Malya ambayo ameitaja; je, haoni kwamba kutoanza kujenga ule uwanja ambao tuliambiwa ungeweza kuanza mwaka huu wa Ilemela ni kuwavunja moyo wananchi wa Ilemela ambao walitoa kile kiwanja chao bure kwa Serikali bila masharti? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika viwanja vitano ambavyo vilitajwa kama kuwa wenyeji wa michezo ya AFCON, uwanja wa CCM Kirumba nao ulitajwa; je, ni lini Serikali itaanza ukarabati wa uwanja ule ili kuwa tayari kutumika kwa michezo ya AFCON 2027?

Name

Hamis Mohamed Mwinjuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Angeline Mabula kwa ufuatiliaji mzuri wa masuala ya Wana-Ilemela ikiwamo ufuatiliaji kwenye masuala ya michezo na hasa kituo hiki ambacho ameuliza swali lake la msingi leo; ninaamini Wana-Ilemela wanaliona hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye maswali yake mawili ya nyongeza, kwanza kuhusu kuchelewa kuanza kwa kituo hiki cha Ilemela; kama ambavyo nimejibu katika wakati najibu swali la msingi, sasa hivi emphasize ipo katika ujenzi wa miundombinu itakayotumika kwa ajili ya CHAN 2025 na AFCON 2027. Kituo hiki kipo katika mipango ya Serikali, hatujakiondoa na tunamwomba Mheshimiwa Mabula kwa niaba ya Wana-Ilemela waendelee kuwa na subira, tutakapomalizana na miundombinu kwa ajili ya CHAN 2025 na AFCON 2027 tutahamia kwenye ujenzi wa vituo mbalimbali kikiwemo Kituo cha Ilemela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimtoe wasiwasi, Serikali bado ina mpango nacho kituo hiki na itakifanyia kazi kadri hali itakavyoruhusu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na viwanja vitano ambavyo vilikuwa vimetengwa kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati, kwanza viwanja hivi vitano havitatumika moja kwa moja kwa ajili ya AFCON, viwanja vitakavyotumika itakuwa ni uwanja Benjamin Mkapa Dar es salaam, uwanja mpya unaojengwa Arusha na uwanja wa Amani Zanzibar. Viwanja hivi vitano tulikuwa tunavikarabati kwa ajili ya kuvifanya kama backup na uwanja wa CCM Kirumba ni miongoni mwa viwanja hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimtoe wasiwasi, mpango huu upo pale pale na tupo katika mazungumzo ambayo yapo katika hatua iliyosogea sana na mmiliki wa viwanja hivi ili kuona utaratibu bora wa kuvifanyia ukarabati, matumizi yake kwa maana ya uendeshaji na namna ambavyo thamani ya fedha ya umma itakayotumika kwenye ukarabati wa viwanja hivi itakavyopatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimtoe Mheshimiwa Mabula wasiwasi, uwanja wa CCM Kirumba bado upo katika mipango ya Serikali na hivi karibuni tutaanza ukarabati wake kama ambavyo tutaanza kwenye viwanja vingine vinne ambavyo vinakwenda kuungana na CCM Kirumba kwa ajili ya backup ya michezo ya AFCON 2027. (Makofi)

Name

Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA aliuliza: - Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa kiwanja cha michezo (centre of excellence) Manispaa ya Ilemela chenye hekari 16.75 ambacho kina hati tayari?

Supplementary Question 2

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mkoa wa Mara ni mkoa ambao anatoka muasisi wa Taifa letu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, lakini Mkoa wa Mara hauna uwanja wa mpira wenye hadhi ya kimataifa. Kwa kuwa uwepo wa uwanja huu ungeweza kutoa fursa mbalimbali kama ajira, kukuza utalii, maana tuna Mbunga ya Serengeti na kule Butiama kwa Baba wa Taifa na baadaye kukuza uchumi wa nchi yetu.

Je, Serikali haioni kwamba kuna haja sasa ya kuweka katika mpango wake ujenzi wa uwanja wa mpira wenye hadhi ya kimataifa na kulipa jina Mwalimu Nyerere katika Mkoa wetu wa Mara?

Name

Hamis Mohamed Mwinjuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa swali zuri la Mheshimiwa Esther Matiko; anayo hoja kimsingi na Serikali inaona haja ya kuwa na viwanja na miundombinu mbalimbali ya michezo nchi nzima. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ya kwamba tunaingiza katika mpango wa Serikali wazo lake na tutalifanyia kazi kadri rasilimali fedha itakaporuhusu na wakati utakapokuwa rafiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ni wazo zuri na mimi namuunga mkono ya kwamba ni muda wake sasa wa kufanyiwa kazi, ahsante. (Makofi)

Name

Abubakar Damian Asenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilombero

Primary Question

MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA aliuliza: - Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa kiwanja cha michezo (centre of excellence) Manispaa ya Ilemela chenye hekari 16.75 ambacho kina hati tayari?

Supplementary Question 3

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Kwa kuwa Halmashauri ya Mji wa Ifakara Jimbo la Kilombero ni halmashauri inayokua kwa kasi sana na ina vipaji vingi sana vya vijana vya michezo; mfano Aishi Manula anatoka Kilombero na tuna maeneo mengi sana ya ujenzi wa viwanja vya michezo, mfano eneo ambalo lipo karibu na Kituo cha Afya cha Kibaoni pale Ifakara, Mwaya na CCM kwa Tangani.

Je, ni lini Serikali itafanyia kazi ombi letu la kujenga uwanja wa kisasa wa michezo katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara ili kuendelea kukuza vipaji vya vijana wetu?

Name

Hamis Mohamed Mwinjuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Asenga kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuhakikisha masuala mbalimbali ya wanajimbo la Kilombero hayafumbiwi macho, yakiwemo masuala katika sekta ya michezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu katika maswali yaliyotangulia, lengo la Serikali na lengo la Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kwamba tunakuwa na miundombinu bora ya michezo nchi nzima ili kuweza kugundua vipaji na kuvilea na kuhakikisha vijana pengine wanakutana na riziki alizowaandikia Mwenyezi Mungu kwa kutumia vipaji hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Asenga, kwa sasa Serikali inafanya kila inaloweza kuhakikisha kwamba miundombinu kwa ajili ya CHAN 2025 na AFCON 2027 inakamilika, hali kadhalika Serikali inaunda mamlaka ya usimamizi wa miundombinu ya michezo ambayo itakuwa inaitwa SIMA ili kwenda kutekeleza kwa vitendo maono ya mwanamichezo namba moja wa nchi hii, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Miongoni mwa mambo ambayo itayafanya ni kuhakikisha tunakuwa na miundombinu bora ya michezo katika nchi nzima; na Jimbo la Kilombero halitoachwa nyuma. Ahsante.

Name

Yustina Arcadius Rahhi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA aliuliza: - Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa kiwanja cha michezo (centre of excellence) Manispaa ya Ilemela chenye hekari 16.75 ambacho kina hati tayari?

Supplementary Question 4

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na mimi kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itajenga uwanja wa mchezo katika Wilaya ya Mbulu ambapo ni eneo muhimu sana kukuza vipaji vya riadha; tukizingatia kwamba wanariadha mashuhuri kina John Steven wametokea eneo hilo?

Name

Hamis Mohamed Mwinjuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru na swali zuri la Mheshimiwa Yustina, ni kweli kwamba vipaji vingi vya riadha vinatokea katika ukanda anapotokea Mheshimiwa Mbunge na tumeweza kuona, faida kubwa imepatikana kwa wanariadha na medali nyingi ambazo wameshinda wakati wakiliwakilisha Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali bado ina mipango ya kuendelea kujenga miundombinu mbalimbali ya michezo na sasa hivi tumejenga kituo cha michezo katika ukanda huu wa eneo la Karatu. Hii ni kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunavigundua na kuvilea vipaji hivi anavyovitaja Mheshimiwa Mbunge na kadri hali itakavyoruhusu tutafika chini zaidi na kuhakikisha kwamba tunajenga kituo cha michezo kwenye eneo analolitaja Mheshimiwa Mbunge.

Name

Dr. Christina Christopher Mnzava

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA aliuliza: - Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa kiwanja cha michezo (centre of excellence) Manispaa ya Ilemela chenye hekari 16.75 ambacho kina hati tayari?

Supplementary Question 5

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, Mji wa Kahama ni mji ambao unakua sana na unakua kwa kasi na una vitu vingi vizuri na una vipaji vya watoto wa kike ambao wanacheza mpira wa miguu, lakini hakuna uwanja.

Je, nini kauli ya Serikali au mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba Halmashauri ya Manispaa ya Kahama inapata uwanja?

Name

Hamis Mohamed Mwinjuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimefika Kahama na Mheshimiwa Mnzava analifahamu. Ni kweli Mji wa Kahama unavyo vipaji vingi na mji unakua kwa kasi sana. Kwa sasa kama ambavyo nimetangulia kusema msisitizo uko kwenye viwanja ambavyo vitatumika kwa ajili ya CHAN na AFCON na nitoe rai kwa mamlaka husika za Wilaya na Mji wa Kahama kuhakikisha kwamba wanatenga fedha kutoka kwenye mapato yao ya ndani ili kuanza kutengeneza miundombinu bora ya michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Wizara nimhakikishie kuwa tuko tayari kutoa usimamizi wa kitaalamu kuhakikisha tunawaunga mkono na hali ya rasilimali fedha itakaporuhusu, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutawaunga mkono kwa kuhakikisha tunawasaidia kukamilisha miundombinu hiyo ya michezo. (Makofi)

Name

Eng. Stella Martin Manyanya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nyasa

Primary Question

MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA aliuliza: - Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa kiwanja cha michezo (centre of excellence) Manispaa ya Ilemela chenye hekari 16.75 ambacho kina hati tayari?

Supplementary Question 6

MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, niliwahi kuuliza na ninakumbusha kwamba ni lini Serikali itachukua sehemu ya mapato yanayopatikana wakati klabu kubwa za mpira kama Simba na Yanga zinapocheza na kupeleka maeneo ya pembezoni ambako kuna wapenzi wengi na hawana viwanja vya mpira? (Makofi)

Name

Hamis Mohamed Mwinjuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru na ninalikumbuka swali hili la Mheshimiwa Engineer Stella Manyanya, Mbunge, bado tunapata wakati mgumu wa kuona namna ambavyo tunaweza tukachukua mapato haya na kuyapeleka katika sehemu ambayo Mheshimiwa Mbunge anataja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapato ambayo yanapatikana kwenye michezo ambayo klabu hizi zinacheza bado ni makubwa sana mpaka sasa hivi na tunaangalia namna ya kuyapunguza ili klabu hizi ziendelee kunufaika ama zinufaike zaidi. Kwa hiyo, utakapofika wakati ambapo tunawakata zaidi sasa kwa ajili ya kupeleka kwenye miundombinu ya michezo kwa sehemu za pembezoni, ninafikiri kutaleta malalamiko makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho tunajaribu kufanya sasa hivi ni kuhakikisha Serikali inaendelea kutenga asilimia tano kutoka katika michezo ya kubahatisha ili kuhakikisha kwamba tunafanya shughuli mbalimbali za maendeleo ya michezo zikiwemo ambazo Mheshimiwa Engineer Stella Manyanya amezitaja, lakini kwenye kuzikata club ninafikiri kwa sasa itakuwa ngumu. Siyo jambo ambalo linaweza kuongeleka kirahisi. (Makofi)