Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dr. Christine Gabriel Ishengoma
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani wa kumaliza migogoro ya wafugaji na wakulima Mkoani Morogoro?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza kabisa ninashukuru kwa majibu mazuri sana ya Naibu Waziri ambayo pia yanaridhisha, lakini nina maswali mawili ya ngongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza; Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi katika Mkoa wa Morogoro ulianzishwa katika baadhi ya wilaya zikiwemo Wilaya za Manyinyi, Ulanga, Kilombero, Kilosa pamoja na Mvomero; lakini kilichotokea ulisimama; je, ni lini mpango huu utaendelea kusudi wakulima na wafugaji waweze kuishi vizuri?
Swali langu la pili, je, kuna mkakati gani wa kutoa elimu kwa wote hasa kwa wakulima na wafugaji ili waweze kuishi kwa kutegemeana? Ahsante sana. (Makofi)
Name
Geophrey Mizengo Pinda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kavuu
Answer
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na nimshukuru sana Dkt. Christine Gabriel Ishengoma kwa maswali yake mawili ya nyongeza; kwamba je, lini mpango huu utaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwa sasa hivi baadhi ya wilaya tunaendelea nazo baada kupata fedha kidogo kutoka Serikalini na muda mfupi ujao baada ya kuwa mmetupitishia bajeti tutakapokwenda kuanza mwaka mpya ya fedha, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba zoezi hili litakuwa linakwenda tena kuanza na kumalizia maeneo yaliyobaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la elimu, hili ni lazima wote tusaidiane kwa sababu katika uhalisia, Wizara imeendelea kutoa elimu katika maeneo mbalimbali. Peke yake haitoshi, niwaombe na wenzetu TAMISEMI ambao ndiyo wanaosimamia namna bora ya matumizi bora ya ardhi kwenye maeneo hayo wazingatie yale maeneo ambayo yametengwa na wananchi wapate elimu ya kutosha ili muingiliano ule usiwepo mkubwa hata kusababisha mgongano wa wakulima na wafugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe wasiwasi tu Wizara inaendelea kutoa elimu kupitia redio, television, lakini kupitia mikutano ya hadhara na makongamano kwa ajili ya kuwaelimisha wananchi kujua umuhimu wa namna bora ya kutumia ardhi tuliyonayo ambayo kama nilivyosema huko awali hatuna mbadala wala hatuna namna tutakavyoweza kuiongeza ardhi hii tuliyonayo ambayo ni ya urithi wetu.
Name
Dr. Thea Medard Ntara
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani wa kumaliza migogoro ya wafugaji na wakulima Mkoani Morogoro?
Supplementary Question 2
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya ardhi yaani katika kila mikoa inaendelea na ipo; je, Wizara ya Ardhi hawaoni kwamba ipo haja sasa ya kuwatumia wanafunzi wanaotoka Tabora pale Ardhi pamoja na wanafunzi hawa wa Ardhi, Dar es Salaam wakafanya hiyo kampeni ya kumaliza hii migogoro, kwa sababu wale watoto wapo na na wengi, wakafanya hiyo angalau kwa miezi sita mkamaliza haya matatizo? Ahnsate.
Name
Geophrey Mizengo Pinda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kavuu
Answer
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nipende kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Ntara kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba migogoro hii tumeendelea kuipunguza kwa kasi kubwa sana na yeye mwenyewe atakubaliana na mimi kuwa wale wanafunzi wa vyuo hivi tumeendelea kuwatumia na si kwamba hawatumiki. Wametumika katika miradi mbalimbali, na hasa hii ya kwenda kubainisha matumizi bora ya ardhi katika maeneo mbalimbali. Walikwenda mpaka mikoa kadhaa na wametusaidia sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kwanza kabisa katika kumaliza migogoro hii ni wananchi wenyewe kutambua namna ya kutumia rasilimali ardhi waliyonayo katika kuzingatia yale matumizi waliyojipangia wao wenyewe. Hii itatusaidia sana kupunguza mgongano huu wa kimaslahi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwa wenzetu ambao ni wafugaji, sasa kuwa na ufugaji wa kisasa utakaokuwa unazingatia mazingira halisi ya thamani ya mifugo yao badala ya sasa ambapo wamekuwa wakifugia kama vile desturi, mila na kama hobby hivi ya ufugaji. Sasa matokeo ya wafugaji hawa bado hayajaweza kuwa na mchango mkubwa katika maisha yao ya kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo turudi kwenye uelewa wa pamoja, kwamba tuwe na ufugaji bora wenye malengo sahihi kabisa ya kuleta maendeleo kwenye jamii husika. (Makofi)
Name
Felista Deogratius Njau
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani wa kumaliza migogoro ya wafugaji na wakulima Mkoani Morogoro?
Supplementary Question 3
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na migogoro ya ardhi kati ya wawekezaji na wananchi katika Mkoa wa Kilimanjaro, hasa Jimbo la Moshi Vijijini, na imeonekana kuleta athari hasi kwa muda mrefu kwa sababu migogoro hii imedumu kwa muda mrefu bila suluhisho; je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba wanakwenda kutatua migororo hii ili wananchi waweze kuishi kwa amani? Ahsante.
Name
Geophrey Mizengo Pinda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kavuu
Answer
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kimsingi Mbunge wa Jimbo hili amekuwa karibu sana na sisi kwa ajili ya kufuatilia namna ambavyo tunaweza kwenda kuimaliza hii migogoro. Tunakumbuka kuna baadhi ya migogoro ambayo tayari tulishakutana na Mheshimiwa Mbunge, tumemwelekeza namna ya kwenda kulimaliza suala hili, na tunapata ushirikiano mkubwa sana kutoka kwa Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo. Mimi nikuhakikishie tu Mheshimiwa Njau ukishirikiana vizuri na Mheshimiwa Mbunge wa jimbo…
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba anijibu swali.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: …mtaelewa namna ambavyo tunashughulikia masuala haya.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved