Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Tarimba Gulam Abbas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Primary Question

MHE. TARIMBA G. ABBAS aliuliza: - Je, nini kauli ya Serikali juu ya changamoto ya maji maeneo ya Jimbo la Kinondoni hususani Kata za Mwananyamala na Makumbusho?

Supplementary Question 1

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Bunge hili wakati wote linafahamu juu ya juhudi ya Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba maji yanapatikana kwa wananchi wa Tanzania. Mheshimiwa Waziri anasema matatizo haya ya Mwananyamala na Makumbusho yatatatuliwa mwaka wa fedha ujao, 2025/2026. Maji siyo kama umeme kwamba unaweza ukawasha kibatari, ni lazima upate maji sasa.

Swali langu ni, hawa wananchi watakaa hivyo mpaka mwaka wa fedha unaokuja, ambao tarehe haijulikani, wanakwenda kupata kwa njia gani? Swali langu hilo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, changamoto hii sasa imekuwa hadi kufikia Mtaa wa Hananasif katika Kata ya Hananasif, ina maana matatizo yanaendelea kuwa mengi.

Swali langu, DAWASA inafanya biashara, hivi mnataka kutuambia sisi Wabunge kwamba DAWASA inashindwa kupata fedha hata za kukarabati miundombinu ambayo inaifanya maji yaweze kupatikana na wao waweze kuyauza hayo maji?

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, naanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Tarimba Abbas, Mbunge wa Kinondoni na tunamshukuru sana kwa kuendelea kuishauri Serikali katika sekta hii ya maji na sisi Serikali kupitia kwa wataalamu wetu tumekuwa tukipokea maoni hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa Mwananyamala na Makumbusho ni lazima kuwepo na mabadiliko ya miundombinu ambayo ilikuwa inatoa huduma ya maji. Uchakavu wake unaweza kuwa ni tatizo lingine pia, lakini kikubwa ni maji kutopatikana katika maeneo haya siyo tu kwa sababu ya uchakavu wa miundombinu, Jiji la Dar es Salaam wakazi wanapoingia na kutoka, wanapojenga na kubomoa, inatuathiri hata sisi katika miundombinu yetu ya maji. Kwa hiyo, kwa muktadha huo tatizo na changamoto ya miundombinu kwa upande wa Dar es Salaam kwa kuangalia jiografia ya ujenzi wa wake haitakwepeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa ni Serikali inatambua changamoto hiyo inayotokana na mazingira kama hayo na tumekuwa tunachukua hatua kulingana na aina ya changamoto iliyojitokeza. Lengo kubwa la Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia suala la ujenzi wa miundombinu chakavu, urekebishaji au uboreshaji unatokana bajeti ambayo tunaipitisha hapa Bungeni. Kama Serikali, si vyema sana tukawa tunatoa ahadi za uongo ambazo hazitaweza kwenda kutatua changamoto zaidi ya kuanzisha taharuki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunamhakikishia Mheshimiwa Mbunge katika bajeti ya 2025/2026, kama ambavyo nimejibu katika jibu la msingi, tutaenda kufanyia kazi eneo la Msikitini ambalo ndilo litaenda kusaidia upande wa Makumbusho pamoja na Mwananyamala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa DAWASA; hata gharama ambazo DAWASA anatoza, ukiangalia production cost ya DAWASA, ulipaji wa kemikali, watalaam wake kuzunguka kuangalia na kutathmini changamoto zilizopo, ni kweli kabisa kwamba tunaweza tukasema ni rahisi sana kupata mapato na kuanza kuyawekeza katika uboreshaji wa miundombinu, lakini gharama za uendeshaji ziko juu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama yake haijapitiwa takribani miaka sita ambapo hapa katikati kumekuwepo na mabadiliko ya dola na hizi kemikali tunazipata kutoka nje ya nchi, vipuri tunavipata kutoka nje ya nchi ambapo kuna mabadiliko, lakini gharama ya DAWASA bado imebaki ileile kiasi kwamba ni mzigo mkubwa. Ni lazima tuseme ukweli inapofikia kusema ukweli, lazima tuone namna gani ya kuisaidia DAWASA na kupitia bajeti hii ambayo tumeipata naamini kabisa kwamba tutaweza kwenda kutatua baadhi ya changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, kupitia kanuni ambazo zinaongoza Mfuko wa Taifa wa Maji, sasa 29% inaenda kusaidia ku-subsidize zile mamlaka zetu pale ambapo hawana uwezo wa kufanya jambo kupitia Mfuko wa Maji, yale makusanyo yake yataenda kusaidia ku-subsidize, lengo ni kwamba mamlaka hizi zisije zikakumbana na tatizo la kutotoa kabisa huduma ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokea ushauri wake na tutaendelea kuufanyia kazi, lakini ni vizuri pia, tukatoa taarifa Watanzania wafahamu gharama ya uzalishaji wa maji ni kubwa sana, hasa kwa Jiji ya Dar es Salaam, ahsante sana. (Makofi)

Name

Boniphace Nyangindu Butondo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kishapu

Primary Question

MHE. TARIMBA G. ABBAS aliuliza: - Je, nini kauli ya Serikali juu ya changamoto ya maji maeneo ya Jimbo la Kinondoni hususani Kata za Mwananyamala na Makumbusho?

Supplementary Question 2

MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwanza, nakupongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali na pia naipongeza Serikali ya mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo imekuwa inashughulikia changamoto kubwa hii ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Kishapu bado tuna changamoto ya zaidi ya kata tisa ambazo hazina maji. Nataka nipate majibu, ni lini sasa Serikali itapeleka maji katika Kata ya Shagihilu, Ndoleleji, Masanga, Mwamalasa na Somagendi ambazo zina changamoto kubwa sana ya maji? Ahsante sana. (Makofi)

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na nampongeza sana kaka yangu Mheshimiwa Butondo, Mbunge wa Kishapu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi ambapo Kishapu imebadilika kwa kasi sana katika sekta ya maji ni hiki cha 2020 – 2025. Upatikanaji wa maji kupitia bomba la kutoka Ziwa Victoria na ile extension yake umesaidia sana kupunguza makali ya ukosefu wa huduma ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kwamba ni kata hizi tisa ambazo Mheshimiwa Butondo ameendelea kuzipambania na sisi Serikali, tumeshasikia kilio cha Wana-Kishapu kupitia kwa mwakilishi wao mahiri kabisa. Wizara ya Maji katika bajeti iliyopitishwa ya shilingi trilioni 1.061, tunamhakikishia kwamba, hizi Kata tisa tunaenda kuzifanyia kazi na wananchi wa Kishapu watapata huduma ya maji safi na salama, ahsante. (Makofi)

Name

Daimu Iddi Mpakate

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kusini

Primary Question

MHE. TARIMBA G. ABBAS aliuliza: - Je, nini kauli ya Serikali juu ya changamoto ya maji maeneo ya Jimbo la Kinondoni hususani Kata za Mwananyamala na Makumbusho?

Supplementary Question 3

MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, RUWASA Wilaya ya Tunduru, walifanya upembuzi yakinifu wa mradi wa maji katika Mji Mdogo wa Nalasi, wenye vijiji vinne vya Lipepo, Nalasi, Chilundundu Kusini na Chilundundu Kaskazini. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kutekeleza mradi ule? (Makofi)

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na ninamshukuru sana kaka yangu kwa kazi nzuri na vile vijiji vinne kwa kweli, najua ni kipaumbele chako Mheshimiwa Mbunge na hakika unajua kwamba, eneo lile lina wakazi wengi ambao ni wapiga kura wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, wapiga kura wako na Madiwani pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapofanya upembuzi yakinifu hatua inayofuatia ni Serikali kupata fedha, kwa ajili ya kupata usanifu wa kina. Baada ya kufanya usanifu wa kina ndio tujue mradi huo utagharimu kiasi gani na baada ya kujua ndio utengewe fedha hiyo, kama haipo itafutwe, ili sasa twende kutekeleza mradi huo wananchi wa kata hizo nne waweze kupata huduma ya maji, safi na salama, ahsante sana.