Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Esther Nicholus Matiko
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ESTHER N. MATIKO K.n.y. MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza:- Je, ni maeneo gani ya kuweka mkazo ili Sekta nyingine zitekeleze na kuwa sehemu ya utekelezaji wa azma ya Ugatuzi wa Madaraka?
Supplementary Question 1
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Sasa hivi kumekuwa na taratibu kutoka Serikali Kuu kwa baadhi ya Wizara kutaka kunyofoa idara mbalimbali ambazo kimsingi ziliwekwa kwa dhana ya Ugatuzi wa Madaraka. Kwa mfano, kumekuwa na matamanio ya kuondoa Maafisa Kilimo na Maafisa Ardhi kutoka kwenye Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kiuhalisia hizi ziliwekwa ili kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi. Sasa ninataka kujua, ni nini kauli ya Serikali kuhakikisha kwamba Wizara zote zenye matamanio ya kuondoa zile idara zisiondoe ili kuweza kuimarisha dhana nzima ya Ugatuaji wa Madaraka?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Sera ya Kikodi ambayo kimsingi inazitaka Serikali za Mitaa kukusanya mapato yote na kuzipeleka Hazina, halafu ndiyo zirejeshwe kwa ajili ya operesheni mbalimbali za Serikali za Mitaa, zimekuwa zikitatiza kwa sababu kwanza, hazirudi kwa wakati, lakini wakati mwingine zinarudi kwa upungufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nini kauli ya Serikali kuhakikisha kwamba zinaimarisha na kuhakikisha fedha zote ambazo zinakusanywa kupelekwa Hazina zinarudishwa kulingana na bajeti na makadirio ya Serikali za Mitaa, na kwa wakati ili kuweza kuimarisha utendaji wa shughuli wa kila siku katika Serikali za Mitaa?
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa misingi ya Ugatuzi wa Mdaraka kutoka Serikali Kuu kwenda kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa umewekwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 145 na Ibara 146.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kujua umuhimu na msingi mzima wa dhana hii ya Ugatuzi wa Madaraka, kama nilivyotangulia kujibu katika majibu ya msingi, tayari imeshafanya hatua za kimsingi kabisa za kutengeneza Rasimu ya Sera Kamili ya Taifa ya Ugatuzi, na ipo katika hatua mbalimbali za majadiliano na kupitiwa ili mwisho wa siku iwe sera kamili.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Serikali ni kuendelea kuimarisha sera hii, kuimarisha dhana hii ya Ugatuzi wa Madaraka kutoka Serikali Kuu kwenda kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Esther Matiko, amezungumza kuhusiana na baadhi ya Wizara za Kisekta kuwa na matamanio ya kuhamisha Maafisa, mathalani Maafisa wa Kilimo; Maafisa wa Ardhi, kutoka kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa na kuwarudisha katika uwajibikaji moja kwa moja kwenye Wizara zao. Kazi kubwa na component muhimu ya Ugatuzi wa Madaraka kutoka Serikali Kuu kwenda kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa ni pamoja na kuwa na mahusiano kati ya Serikali Kuu na Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kazi yake mojawapo ni ku-coordinate au kutengeneza huo muunganiko wa sera zinazosimamiwa na Wizara za Kisekta katika utekelezaji huku kwenye mamlaka zetu za Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea na jitihada hizo ili kuendelea kuimarisha dhana hii kwa maana hata Hayati Baba wa Taifa aliweka msisitizo mkubwa sana katika uanzishwaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa na kuelezea umuhimu mkubwa sana wa ugatuzi kwa lengo la kuhakikisha kwamba wananchi ndio wanafanya maamuzi, wanashiriki moja kwa moja kwenye kupanga, kusimamia na kutathmini maendeleo katika maeneo yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kusimamia upande huu, sera ikikamilika itaendelea kuimarisha katika upande huu na kwa sasa hivi tayari mafunzo yanaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusiana na suala la pili, Mheshimiwa Esther Matiko amezungumza kuhusiana na Ugatuzi wa Fedha (Fiscal Decentralization), ambayo na yenyewe ni component muhimu sana katika Ugatuzi wa Madaraka (D by D). Serikali katika eneo hili inaendelea kuimarisha kwa kuziwezesha Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa kuwa bunifu kuibua miradi ambayo itaweza kuziwezesha mamlaka zetu kukusanya mapato ili ziweze kupanga maendeleo yake na kutekeleza maendeleo kwa ajili ya watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa zinaimarika kimapato, zinaweza kuwa na hiyo Fiscal Decentralization ambayo wote tunatamani ifikiwe ili ziweze kuimarika. Mahusiano kati ya fedha zinazotoka Serikali Kuu ambazo zenyewe kimsingi zinakuwa ni kwa ajili ya ku-supplement (kuongeza nguvu) katika kazi na wajibu wa msingi wa Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa ya kukusanya mapato na kupanga maendeleo, itaendelea kuimarisha pia upande huo kwa maana ya Serikali Kuu iweze kuunga mkono.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninadhani hoja ya Mheshimiwa Mbunge ni kwamba, fedha ziwe zinafika kwa wakati kwenye mamlaka zetu ili ziweze kutekeleza majukumu yake. Serikali itazingatia hilo.
Name
Prof. Patrick Alois Ndakidemi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Vijijini
Primary Question
MHE. ESTHER N. MATIKO K.n.y. MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza:- Je, ni maeneo gani ya kuweka mkazo ili Sekta nyingine zitekeleze na kuwa sehemu ya utekelezaji wa azma ya Ugatuzi wa Madaraka?
Supplementary Question 2
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Ili kufanikisha Ugatuzi wa Madaraka ambapo Serikali imefanya kutoka Serikali Kuu kwenda kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa, tunahitaji kuwa na wataalamu wa kutosha katika mamlaka hizi. Je, ni kwa kiasi gani uhaba wa wataalamu, kwa mfano Wahandisi umeathiri ufanisi wa Ugatuzi wa Madaraka?
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia umuhimu mkubwa sana wa Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa kuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu, utekelezaji wa Sera mbalimbali za Kisekta, Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba, kunakuwa na wataalamu wa kutosha kwenye hizi Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa kwa ajili ya backstopping.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali inaendelea kuhakikisha kwamba inaajiri wataalamu mbalimbali. Ukiacha tu Wahandisi ambao Mheshimiwa Prof. Ndakidemi amewataja, lakini wataalamu katika sekta mbalimbali kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wanatekeleza wajibu wa msingi wa backstopping kuwa na ile technical assistance kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wanatekeleza majukumu na kwamba Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa zinakuwa na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea na jitihada hizo kupitia Wizara ya Utumishi. Kila mwaka wanaajiriwa watumishi wa kada mbalimbali kwa ajili ya kupangwa katika Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa ili mamlaka zetu hizi ziweze kuwa na huduma nzuri kwa kuwa na wataalamu ambao wanasaidia katika utekelezaji wa majukumu.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved