Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Zahor Mohamed Haji

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwera

Primary Question

MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI aliuliza: - Je, ni lini Serikali italeta muswada wa sheria kuhusu changamoto za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi ili sasa ziwe kwa mujibu wa sheria?

Supplementary Question 1

MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru, kwanza ninaomba niishukuru Serikali kwa majibu yake mazuri, lakini ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, kwa sababu bado Tanzania ipo na itaendelea kuwepo, Muungano upo na utaendelea kuwepo. Je, ni vipi hasa vigezo vinavyotumiwa na Serikali kuweza ku-identify kwamba hii ni changamoto ya Muungano, kwa sababu kila siku zinakuja mpya?

Swali la pili, je, Serikali sasa iko tayari seriously kuanza kutoa elimu kwa wananchi wa Tanzania ili waweze kuelewa changamoto zote ambazo zimepatiwa ufumbuzi? Ninakushukuru sana.

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zahor Mohammed Haji, Mbunge wa Jimbo la Mwera, lakini kabla ya hapo nichukue fursa hii kumpongeza na kumshukuru sana kwa kuwa amekuwa mdau mzuri na ni mmoja wa miongoni mwa watu ambao wanaendeleza, kuutunza na kuuenzi Muungano huu kwa vitendo kwa kutaka kujua mambo mbalimbali ya Muungano huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka niseme tu kwamba, kabla ya yote ninataka nichukue fursa hii niwambie Watanzania kwamba si kila changamoto ni changamoto ya Muungano. Zipo changamoto ambazo tunasema hizi tuzipeleke tukazijadili, lakini zipo nyingine ni changamoto za sekta zenyewe kukaa zikalimaliza ili zisiwe changamoto ya Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vipo vigezo ambavyo huwa tunavichukua; cha kwanza ni kigezo cha kisekta, endapo kumetokea changamoto na sekta zimekaa lakini zimeshindwa kufikia muafaka, hapo zinakuja kwetu kama Ofisi ya Makamu wa Rais tunaosimamia Muungano, halafu sisi tunazijadili, tunazipeleka ngazi ya watalaam, ngazi ya Makatibu Wakuu, Mawaziri halafu zinakwenda kwenye ngazi ya kutatuliwa, kwa hiyo, hicho ni kigezo kimoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kigezo cha pili ni kigezo cha hali ya wakati ule. Kuna hali fulani zinajitokeza hizo zinakuwa ni kigezo kwamba hatuna namna ya kufanya, lazima tuzifanye sasa iwe ni sehemu ya kusema hiki ni kigezo cha kupelekwa kwenye hoja za kujadiliwa kama hoja za Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni uzito wa hoja yenyewe, na ndiyo pale niliposema kwamba siyo kila hoja au changamoto itakuwa ni changamoto ya Muungano. Ziko hoja nzito ambazo tunasema hizi tuzijadili, zipo zingine tunasema hizi tuzimalize katika namna ambayo hazitoingia katika orodha ya changamoto za Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali iko tayari na kazi hii imeshaanza. Tumefanya kazi kubwa katika kuielimisha jamii juu ya suala zima la Muungano huu, faida, fursa, asili na chimbuko la Muungano huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyombo vya habati vimetusaidia sana, magazeti, televisheni, radio, mitandao ya kijamii, na makongamano mbalimbali. Tumetoa vitabu vya Muungano, mijadala mbalimbali, majarida na ziara za mafunzo zinazowafanya watu wajifunze kuhusu Muungano, ninakushukuru. (Makofi)

Name

Tarimba Gulam Abbas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Primary Question

MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI aliuliza: - Je, ni lini Serikali italeta muswada wa sheria kuhusu changamoto za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi ili sasa ziwe kwa mujibu wa sheria?

Supplementary Question 2

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, hakika ni lazima tujivunie Muungano tulionao kati ya Zanzibar na Tanganyika na kuweza kuifanya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni miaka 60 sasa tangu tumekuwa na Muungano huu, hivi sasa Serikali haioni kwamba, inao uzoefu wa kutosha pale inapobaini changamoto na kujipa muda mchache sana wa kuweza kuzitatua badala ya kukaa kipindi kirefu mpaka hoja inakuwa ni changamoto?

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Tarimba Abbas, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru na kumpongeza kwa kazi kubwa anayoifanya hasa kwenye haya mambo ya Muungano. Ninataka niwaambie Mheshimiwa Mbunge, Wabunge na Watanzania wote kwamba Muungano huu ni wa nchi mbili, Muungano huu ni wa Tanganyika na Zanzibar. Muungano unapoitwa Muungano maana yake siyo hoja iibuke tu tuijadili kwa muda mfupi tuimalize, kinyume na hapo tunaweza tukatengeneza changamoto ndani ya changamoto, ndiyo maana tunakwenda hatua kwa hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatoka hatua za kisekta, tunakuja hatua za Makatibu Wakuu, tunapita kwa wataalam, tunakuja hatua za Mawaziri na tunakuja sasa hatua kubwa ambayo Mwenyekiti wake ni Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais na Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri, lengo na madhumuni ni kwamba tunapotatua changamoto iwe tumeitatua na tusonge mbele ili tufanye mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kuchukua ushauri wake ili zile zinazochukua muda hazitachukua muda na zile ambazo tunahisi zitachukua muda mrefu tutakwenda nazo kwa mujibu wa taratibu, lakini zile ambazo tunahisi ni za kufanya tu haraka tufanya, ninakushukuru. (Makofi)