Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Fatma Hassan Toufiq

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga reli ya kisasa kutoka Kituo Kikuu cha SGR Dodoma hadi Uwanja wa Ndege Msalato?

Supplementary Question 1

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa majibu ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza. Kwa kuwa Serikali imeanza utafutaji wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa reli hii, je, haioni upo umuhimu wa kupata wabia ili kuharakisha ujenzi wa reli hii?

MWENYEKITI: Mheshimiwa Naibu Waziri, majibu. Ah, okay, kuna swali la pili.

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili. Kwa kuwa Magufuli City ni eneo ambalo Wizara mbalimbali za Serikali pamoja na Idara za Serikali zipo kule na ufikaji wake nao umekuwa ni wa kusuasua, je, Serikali haioni kwamba miongoni mwa vipaumbele vya maeneo ya viunga vya Dodoma kujengewa reli kama hii ni pamoja na Magufuli City? (Makofi)

Name

David Mwakiposa Kihenzile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq kwa jinsi anavyofuatilia kwa ukaribu mapinduzi ya reli nchini na kipekee reli ya maeneo ya mijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ameuliza maswali mawili; la kwanza ni umuhimu wa kupata wabia. Serikali kwa kutambua umuhimu wa kuwa na wabia wa Sekta Binafsi katika ujenzi wa miundombinu ya reli na miundombinu mingine, mwaka 2023 ilifanya maboresho ya Sheria Na. 10 ya 2017 ambapo sasa tumeruhusu wawekezaji binafsi au wabia kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa reli yetu. Hivi ninavyozungumza, tumekwishaanza taratibu kwa ajili ya kupata wabia kwa ajili ya ujenzi wa reli hiyo katika Jiji la Dar es Salaam na Jiji la Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hiyo pia kuendelea kutangaza kwa yeyote mwenye mbia yeyote ambaye anapenda kushiriki katika maeneo haya mawili, nafasi na fursa ipo wazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, amezungumzia kwenye upande wa Magufuli City. Sote ni mashahidi kwamba huu ni mji mzuri na mkubwa ambao Serikali imetenga fedha nyingi kuuendeleza. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Magufuli City ni sehemu ya mradi wa Commuter train wa hapa Dodoma, hivyo basi, tumeshakamilisha usanifu, na sasa tunatafuta fedha. Tutakapopata fedha, hatua itakayofuata ni utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpe habari njema Mama yangu Mheshimiwa Toufiq, anakumbuka juzi tarehe 30 mwezi wa Tano hapa Dodoma, CCM ilizindua Ilani yake ya Miaka Mitano ijayo. Ukienda katika ukurasa wa 25 mpaka 31 imeainisha kwa kina miradi itakayokwenda kutekelezwa. Katika miradi hiyo ukisoma ukurasa wa 29, mradi huu umetaja kwa kina wa kujenga reli ya kisasa katika Miji ya Dar es Salaam na Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, tumwombee Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan aweze kuendelea kuongoza nchi yetu kwa kipindi cha pili kwa maana ya kwamba atakapochaguliwa itadhihirisha na kumaanisha tunakwenda kutekeleza miradi hii miwili ambayo nimeshaielezea hapo awali.