Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Miraji Jumanne Mtaturu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Mashariki
Primary Question
MHE. MIRAJI J. MTATURU aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuondoa tembo ambao wanasumbua na kuharibu mashamba ya wananchi wa Singida Mashariki?
Supplementary Question 1
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishukuru sana Serikali kwa majibu mazuri ambayo wametupatia. Ninaomba nichukue nafasi hii kuishukuru sana Serikali kupitia Wizara, kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kufukuza tembo wale ambao walikuwa wasumbufu wakubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata usiku wa kuamkia tarehe moja ya mwezi wa Sita, kulitokea tena kundi ambalo lilienda kufukuzwa na vijana hawa wa TAWA. Ninaipongeza sana Serikali, ambapo Mheshimiwa Mzee Augustino Joseph nyumbani kwake pale waliharibu sana mazao. Sasa nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza. Kama alivyosema hapa, nini mkakati wa Serikali wa kudumu ili kuondokana na tatizo la tembo ambao wanaharibu sana uchumi wa wananchi katika haya maeneo yetu ambayo nimeyataja katika Vijiji vya Mkiwa, Issuna, Mang’onyi, pamoja na Ntuntu. Hali ni mbaya sana kwa sababu kila siku makundi haya yanakwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Toka mwaka 2021 mpaka tunavyoongea ni miaka takribani mitano, matukio au wananchi zaidi ya 400 wameharibiwa vitu vyao pamoja na mali zao na mashamba ikiwemo na wengine kupoteza maisha. Ni nini hatua ya Serikali kuwalipa kifuta machozi wananchi hawa ambao kwa kweli wengi wao bado wanalia mpaka leo, ukizingatia wiki iliyopita nilikwenda ofisini kwa Mheshimiwa Naibu Waziri akaniambia wanafanya tathmini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, tathmini hiyo imeisha? Kama imekamilika, ni nini hatua ya Serikali kuwalipa wananchi hawa ili kuwafuta machozi kwa kuondokewa na ndugu zao na mali zao ambazo mpaka leo hawajalipwa? Ahsante sana. (Makofi)
Name
Dunstan Luka Kitandula
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkinga
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, Serikali inajidhatiti kukabiliana na changamoto hii ambayo kwa kweli imesambaa katika maeneo yetu nchi nzima. Tunapambana na aina ya mnyama ambaye uwezo wake wa kiakili na maarifa ni mkubwa sana. Kwa hiyo, huwa anabadilikabadilika ili kuweza kukwepa ile mikakati ambayo tunaiweka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunachofanya kila siku inavyokwenda, tunabuni mbinu mpya na kubadilisha mifumo ya kukabiliana na wanyama hawa ili kuondokana na changamoto hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, tumeweka mkakati pale ambao umesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza Askari karibu na makazi ya watu. Vilevile tunao mkakati wa kutoa elimu kwa wananchi ili wajue tabia za wanyama hawa na jinsi ya kujilinda nao. Tatu, tumesema tunakwenda na mkakati wa kutumia teknolojia sasa, ndegenyuki, kufunga mikanda ili kudhibiti mienendo hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi ambalo elimu yetu tunaielekeza kwa wananchi ni kwamba, ni ukweli usiopingika kwamba kama Taifa idadi ya wananchi imeongezeka, maeneo ambayo zamani yalikuwa ni maeneo mahsusi kwa ajili ya wanyama hawa, shughuli za kibinadamu zimeongezeka kwenye maeneo yale, na migogoro hii imeongezeka. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali inachukua jitihada zote uhakikisha kwamba tunawanusuru wananchi na changamoto hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lake la pili, ni kweli nimpongeze, tulikuwa na kikao naye wiki mbili zilizopita ofisini. Tulimwahidi kwamba, tunakamilisha tathmini ya wale waliopata madhara, na tathmini ile imekamilika. Tunajua sasa tunahitajika kulipa zaidi ya shilingi milioni 104 kwenye Jimbo lake, kwa hiyo, ninamwomba awe na subira. Tayari tumeshaomba kibali kutoka Wizara ya Fedha, na mara tu baada ya fedha hizi kupatikana tutawalipa wahusika. (Makofi)
Name
Catherine Valentine Magige
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MIRAJI J. MTATURU aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuondoa tembo ambao wanasumbua na kuharibu mashamba ya wananchi wa Singida Mashariki?
Supplementary Question 2
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Hivi karibuni kumekuwa na viashiria vya udhalilishaji dhidi ya kabila la jamii ya Wahadzabe, kwa watoto wadogo na hata watu wazima wanaoishi porini. Wamekuwa wakirekodiwa kwa kudhalilishwa. Kwa mfano tu, unakuta anapewa soda hawezi kuifungua, anaitoboa wanawarekodi, au wanakaa kwenye kiti cha gari cha dereva wanataka wakae wawili. Je, nini kauli ya Serikali? (Makofi)
Name
Dunstan Luka Kitandula
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkinga
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa letu lina utajiri wa makabila zaidi ya 120. Kwa wingi huu wa makabila tuna utajiri wa mila, tamaduni, desturi, lakini na maarifa ya asili ambayo kama Taifa tuna wajibu wa kuyalinda kwa wivu mkubwa, na Serikali inajielekeza kwenye eneo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa viashiria vyovyote ambavyo vinafanywa na baadhi ya wananchi wenzetu, kutweza utu wa Mtanzania havikubaliki kisheria. Sheria zetu ziko wazi, tunakwenda zaidi pale ambapo sasa mitandao inatumika kusambaza maudhui yanayotweza utu wa Mtanzania, sheria zetu ziko wazi, ni makosa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitumie fursa hii kukemea vikali wale wote ambao wanasambaza, wanatengeneza maudhui ya kutweza utu wa Mtanzania. Serikali haitasita kuchukua hatua kali kwa wale wote watakaobainika kufanya vitendo hivi. (Makofi)
Name
Sylivia Francis Sigula
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MIRAJI J. MTATURU aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuondoa tembo ambao wanasumbua na kuharibu mashamba ya wananchi wa Singida Mashariki?
Supplementary Question 3
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na mikakati mizuri ya Serikali, bado kilio kikubwa cha wananchi wa Kabwe na Kirando ni uharibifu wa mazao kutokana na tembo. Tunavyoongea sasa hivi, uharibifu unaendelea. Ninataka kujua kauli ya Serikali ya haraka ya kuhakikisha uharibifu huu unaoendelea sasa hivi unakomeshwa. (Makofi)
Name
Dunstan Luka Kitandula
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkinga
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu kwenye maswali ya msingi, jambo hili ni jambo kubwa, ni jambo ambalo Serikali inapambana nalo kuhakikisha tunawahakikishia wananchi kwanza, usalama wa maisha yao, vilevile wa mali zao. Ninamwomba Mheshimiwa Mbunge, mara baada ya kipindi hiki cha maswali, nikutane naye anieleze eneo hilo ni nini hasa kinatokea ili timu zetu zilizopo uwandani ziweze kuchukua hatua kwa haraka. (Makofi)
Name
Cecilia Daniel Paresso
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MIRAJI J. MTATURU aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuondoa tembo ambao wanasumbua na kuharibu mashamba ya wananchi wa Singida Mashariki?
Supplementary Question 4
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Katika Kata ya Oldeani Wilayani Karatu, kumekuwa na matukio, na kila mwezi ni lazima tusikie vifo vya wananchi kutokana na nyati kutoka katika Hifadhi ya Ngorongoro kuingia kwenye maeneo ya watu na kujeruhi. Mwezi uliopita watu wawili wamefariki, na haya matukio tunayasikia kila siku, inafika mahali wananchi wamechoka. Nini kauli ya Serikali kudhibiti wanyama hawa wasiingie ili wananchi waishi kwa usalama? (Makofi)
Name
Dunstan Luka Kitandula
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkinga
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kauli ya Serikali ni kwamba tunalichukulia kwa uzito mkubwa jambo hili, na tunalishukuru Bunge lako Tukufu liliridhia kwamba, katika eneo lile sasa tuweze kwenda kuweka uzio wa umeme kwa ajili ya kuwanusuru wananchi. Ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutafanya kila linalowezekana kulinda uhai wa wananchi na mali zao. (Makofi)
Name
Yahaya Omary Massare
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manyoni Magharibi
Primary Question
MHE. MIRAJI J. MTATURU aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuondoa tembo ambao wanasumbua na kuharibu mashamba ya wananchi wa Singida Mashariki?
Supplementary Question 5
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Katika Jimbo langu la Itigi, Halmashauri ya Itigi, Vijiji vya Gurungu, Sanjaranda, Njirii, Kamenyanga, vina changamoto kubwa ya tembo kwa muda mrefu. Zamani Askari wa Wanyamapori, tembo wakishaingia makundi makubwa mara mbili, mara tatu, mara nne na sasa ni miaka mitano karibu, walikuwa wanapiga tembo mmoja, wale tembo wanarudi kwenye Hifadhi ya Muhesi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali sasa iko tayari kutoa kibali angalau tembo mmoja akapigwa ili wale warudi katika hifadhi na wananchi wapate angalau nyama, maana kwa muda mrefu wameliwa mazao yao?
Name
Dunstan Luka Kitandula
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkinga
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye majibu ya msingi, mnyama tembo ni mwenye maarifa mengi. Inawezekana mbinu iliyokuwa ikitumika miaka ya nyuma ya kuwawinda leo hii isiwe ni jibu. Ninaomba atupatie fursa hii, tutatuma timu yetu iende ikaangalie nini hasa kinaendelea kwenye eneo lile?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi katika eneo hili la Itigi, Manyoni mpaka kule Singida, eneo hili kiasili ni ushoroba wa hifadhi ya kutoka kule Ruaha kwenda kwenye mapori ya akiba ya Rungwa, Kigosi, Muhesi. Haya yalikuwa ni maeneo ambayo tembo walikuwa wanazagaa. Katika miaka ya karibuni shughuli za kibinadamu zimeongezeka kwenye eneo hili, na hiki ndicho chanzo kikubwa kinacholeta mgogoro huu. Tunaendelea kutoa elimu, tunaomba tusaidiane ili tulitatue jambo hili.