Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Oscar Ishengoma Kikoyo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba kusini

Primary Question

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO aliuliza: - Je, kwa nini watumiaji wa Daraja la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wanalipia kila wanapopita huku watumiaji wa Daraja la Tanzanite hawalipi? (Makofi)

Supplementary Question 1

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Daraja la Tanzanite linahudumia ukanda wa Kinondoni, watu wenye uwezo mkubwa kipesa. Wakati huo huo Daraja la Kigamboni linahudumia watu kawaida. Serikali haioni kwamba kuwatoza hao wenye kipato cha chini na kuwaacha wenye kipato kikubwa inaleta mkakanganyiko? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwa kuwa Serikali ina majukumu makubwa na mahitaji makubwa sana ya kipesa kwa ajili ya kujenga miundombinu hasa vijijini. Je, haioni ni busara kutoza kwenye lile Daraja la Tanzanite ukizingatia wanaopita wengi wana uwezo, tukatumia hizo pesa kulipa mkopo na wakati huo kujenga barabara ambazo tuna mahitaji makubwa hasa kwenye Jimbo langu la Muleba Kusini? (Makofi)

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali ilivyojibu jibu lake la msingi, hapa katika nchi yetu ya Tanzania, madaraja yote tumekuwa tukijenga kwa utaratibu wa kwamba yatatumika bure na ndivyo umekuwa utamaduni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye jibu langu la msingi nimesema, Daraja la Kigamboni lilijengwa kwa ubia; ambapo Serikali ilijenga pamoja na wenzetu wa NSSF ambao waliwekeza fedha na ndiyo maana kukishakuwa na ubia maana yake kuna tozo ama kuna malipo ambayo yatafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuhusu Daraja la Tanzanite pamoja na madaraja mengine, kumekuwa na maoni mbalimbali ikiwepo hata Kamati ya Miundombinu ambayo imekuwa inashauri kwamba yale madaraja makubwa ambayo Serikali imetumia fedha nyingi, pengine ifikie wakati wa sasa watumiaji kuanza kuyalipia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa Serikali imeendelea kupokea maoni na Bunge hili, pengine itafika mahali litatengeneza utaratibu ama litatoa mapendekezo ama maoni kwamba ni madaraja yapi ambayo sasa yaanze kulipiwa na Serikali itaendelea kukusanya maoni, kuona kama suala hilo lini lianze kutumika kutokana na maoni ya wananchi ili tuendelee kujenga madaraja mengine kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge.