Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Naghenjwa Livingstone Kaboyoka
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha usafi wa mazingira kwenye makazi ya watu hasa mijini?
Supplementary Question 1
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa magari mengi yanayozoa taka ni mabovu, na yakipita barabarani yanamwaga taka chafu zinazonuka, na kwa kuwa tunajua Mawaziri wengi mnaenda nchi za nje na mnaona wenzetu wanavyozoa taka, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba magari haya yanakuwa mazuri na yanabeba taka zile kwa ustadi mzuri, badala ya kwenda kuzimwaga njiani kwenye kila barabara inayopita? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili. Kwa kuwa ubora wa miji siyo kuzoa taka tu, tunajua kwamba mitaro yetu mingi imetengenezwa, lakini imejaa taka, barabara zetu zimejaa taka, vibanda vingi vimetengenezwa ovyo ovyo kila mahali ukipita unakuta huyu anauza hapa mchanga, huyu anauza chakula, huyu anauza vitu ambavyo haviendani kabisa na matakwa ya mipango miji; na kwa kuwa tumeona Serikali yetu ina Wizara tatu ambazo zote zinahusiana na mazingira, kwa mfano, Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maendeleo ya Makazi, Wizara ya TAMISEMI ambayo ni halmashauri, na Wizara hii ya Makamu wa Rais, ...
MWENYEKITI: Ninaomba uulize swali.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Je, Serikali haioni ni wakati mwafaka kuangalia tuwe na taasisi moja ambayo itaangalia jinsi ya kuboresha miji yetu iwe mizuri na ya kisasa, ambapo hata watalii wakija wanaona kweli nchi ya Tanzania ni nzuri? (Makofi)
Name
Paschal Katambi Patrobas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Shinyanga Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA, NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Kaboyoka, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, ninakubaliana naye kwamba kuna wakati mwingine yapo magari ambayo yanaonekana ni mabovu yanayohusiana na takataka; lakini nieleze tu Bunge lako Tukufu kwamba tunazo sheria mahususi za utaratibu wa usimamizi wa masuala ya mazingira na usafi wa mazingira pamoja na afya. Kwenye halmashauri zetu, tunayo Sheria ya Mamlaka za Miji na Majiji ya Sura Namba 288.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Sheria hii inaruhusu kutungwa kwa sheria ndogo kwenye kila halmashauri nchini, kuweza kuhakikisha kwamba wanakuwa na sheria ndogo za masuala ya afya na usafi wa mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, katika sheria hii inaelekeza kwamba, kupitia halmashauri, Mkurugenzi wa Jiji au Mji atakuwa na haki au anao wajibu wa kutengeneza vikundi ambavyo vitakuwa ni vikundi mahususi kwa ajili ya ukusanyaji wa taka. Pia, anapewa power za kisheria za kuweza kuingia mikataba na watu wanaoweza kufanya kazi (kandarasi) za kusafisha majiji yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wakati mwingine kumekuwa na udhaifu katika namna ya kuingia mikataba ile au wale wanaopewa kazi hiyo wanajikuta hawana vifaa vya kutosha au utoshelevu kulingana na mikataba inavyotaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitumie fursa hii kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira kuhamasisha sasa mamlaka zetu za Serikali za Mitaa huko chini kuendelea kusimamia vizuri, kwa sababu tunazo na sheria ndogo hizi zinazohusu hifadhi ya usafi na mazingira, zinaeleza ndani ya hiyo sheria, inaeleza namna gani ambavyo masuala ya utoaji wa huduma za chakula, usafi uweje na kunakuwa na mkaguzi ambaye anapewa idhini na Mkurugenzi kufanya kaguzi. Hata wale wahudumu wale wanaotoa huduma wanahitaji hata kupimwa kila baada ya miezi sita afya zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vivyo hivyo upo wajibu kwa upande wa wananchi kufanya usafi kila kipindi kulingana na sheria hizi ndogo. Kuna siku maalum ambazo zimetengwa kulingana na halmashauri husika. Kwa hiyo, mkazi, mmiliki wa biashara au mmiliki wa nyumba au eneo la wazi, anao wajibu wa kuhakikisha anafanya usafi kwenye mitaro, mifereji lakini pia maeneo yote yanayozunguka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hizi ndogo katika kila halmashauri zinatoa pia adhabu ya faini au kifungo cha miezi sita... (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, majibu yako ni marefu sana. Nadhani ameelewa. Ni usimamizi zaidi...
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA, NA WENYE ULEMAVU K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sheria tunazo, tunachohitaji ni usimamizi zaidi ili kuweza kuhakikisha kwamba tunachukua hatua na kuhakikisha mazingira yetu yanakuwa salama. (Makofi)
Name
Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Primary Question
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha usafi wa mazingira kwenye makazi ya watu hasa mijini?
Supplementary Question 2
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa katika maeneo mengi ya miji hasa kwa wananchi wanaokaa karibu na mito na mifereji, wamekuwa wakitupa mara kwa mara taka katika mifereji ile na kusababisha kuziba kwa maeneo mengi na kuleta mafuriko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, magugumaji pia yametambaa katika maeneo ya ziwa kiasi kwamba yanakwenda kufifisha mazalia ya Samaki. Nini mpango wa Serikali wa kuhakikisha kwamba magugumaji yote yanatoka, na pia watu hawa wanaotupa takataka katika mifereji wanadhibitiwa?
Name
Paschal Katambi Patrobas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Shinyanga Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA, NA WENYE ULEMAVU K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la utupaji taka ovyo ni rai yangu nitoe, lakini pia ni kwa mujibu wa sheria. Ni marufuku kwa mwananchi yeyote kutupa taka tofauti na maeneo yaliyoainishwa kwa ajili ya ukusanyaji taka. Kwenye maeneo hayo ndiyo inapopaswa kwenda kutupa taka. Kwa mfano, sheria inahamasisha hata kwenye familia zetu na maeneo ya biashara, maeneo ya viwanda kuwa na sehemu maalum na vyombo maalum kwa ajili ya utupaji wa taka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni kosa kisheria na kuna adhabu hapa ya faini au kifungo kwa yeyote ambaye atafanya tofauti na hivyo na nihamasishe sheria itekelezwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu magugumaji. Ofisi ya Makamu wa Rais inazo programu tayari za ukuhakikisha kwamba kwenye maeneo yote ya Bahari, na pia ziwa, mito na maeneo yote ambayo yamekuwa na huo uoto wa magugumaji, kuna jitihada na programu ambazo zimekuwa zikifanyika mahususi kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kuhakikisha kwamba yanatolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi hii imeshafanyika Babati, Mwanza, pia kazi hiyo inaendelea chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, ahsante.
Name
Eng. Stella Martin Manyanya
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nyasa
Primary Question
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha usafi wa mazingira kwenye makazi ya watu hasa mijini?
Supplementary Question 3
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Hivi unavyoniona, masikio yangu sasa hivi hayako vizuri kutokana na pikipiki zinazoweka sauti kali sana pamoja na magari. Kuna siku nimepatwa na hilo tatizo. Nini mpango wa Serikali kudhibiti hatua hii ya uharibifu wa sauti katika maeneo yetu? (Makofi)
Name
Paschal Katambi Patrobas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Shinyanga Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA, NA WENYE ULEMAVU K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Jambo hili ni kweli, yapo magari na pikipiki ambazo wanazihuisha au kuharibu ile muffler ili itoe sauti ambayo ni kinyume na sauti ambayo imetengenezwa au muungurumo tofauti. Hili ni kosa kwa sababu kwanza ni noise pollution na kwa mujibu wa sheria, hili linaweza kuchukuliwa hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba sana kwa sababu tunafanya kazi kwa pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani, waweze kutusaidia kwa sababu vyombo hivi vya moto vina utaratibu wake na sheria ipo, waweze kuchukua hatua. Hasa kwa vijana walio wengi sasa hivi, imeendelea kuwa fashion kwenye kuharibu mazingira, lakini pia kuleta hali ya kukosa utulivu hasa kwa wale walio na magonjwa ya mshtuko kama ugonjwa wa moyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuombe Wizara ya Mambo ya Ndani, kwa pamoja tushirikiane nao kuweza kuhakikisha tunatatua tatizo hili.