Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Prof. Patrick Alois Ndakidemi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Vijijini
Primary Question
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI aliuliza: - Je, Serikali imejiandaa vipi kukabiliana na mabadiliko ya sera za baadhi ya nchi tajiri kulisaidia Taifa letu kukuza uchumi?
Supplementary Question 1
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Nianze kwa kumwuliza Mheshimiwa Waziri, ni kwa kiasi gani Amri za Kimamlaka (Executive Orders) alizotoa Rais Trump wa Marekani kusitisha misaada katika nchi yetu imeathiri miradi iliyokuwa inaendelea hapa nchini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tunajua maendeleo ya nchi yetu yako mikononi mwetu sisi Watanzania na siyo vinginevyo, wala sio kwa wageni. Je, ni kwa kiasi gani nchi yetu imejipanga kutumia rasilimali zetu za asili ambazo zina utajiri mkubwa kukabiliana na mkwamo huu ambao unaendelea kujitokeza? (Makofi)
Name
Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Iramba Magharibi
Answer
WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa maswali mazuri aliyoyauliza, maswali ya kiprofesa kabisa hayo. Ameuliza orders zilizotolewa na nchi ya Marekani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, Serikali ya Tanzania haikuwa ina ushirikiano wa Kiserikali kwa Serikali kwenye masuala ya fedha za miradi ya maendeleo na Serikali ya Marekani. Fedha nyingi za miradi ya maendeleo kutoka Serikali ya Marekani zilikuwa zinatumia taasisi zake za Marekani, baina ya taasisi mbalimbali za Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, kwa upande wa kibajeti ya moja kwa moja hakukuwepo na athari hizo, na kwa upande wa taasisi zilizokuwa zinapokea fedha tayari Serikali ya Tanzania imeshafanya tathmini, siyo tu kwa tamko la Marekani, bali ni kwa mwenendo wote unaohusisha fedha zinazotoka kwa development partners.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu imepiga hatua nyingi za masuala ya aina hiyo, ikianza zamani sana ambapo kulikuwepo na fedha za misaada zinazokwenda kwenye bajeti, ambazo zilishaisha, na Serikali ina-finance miradi ya maendeleo kutumia fedha za ndani kufidia pengo lile ambalo lilikuwa bajeti inapata fedha kutoka kwa nchi wahisani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, sasa hivi Serikali baada ya kufanya tathmini kutokufuatana na jambo hili lililotokea siku hizi za hivi karibuni, Serikali tayari imepangilia upya matumizi yake kwa bajeti hii inayoendelea na kupata zaidi ya shilingi bilioni 220 ambazo zilikuwa zinahitajika, na hasa maeneo ambayo yalionekana kuathirika, kama maeneo ya afya ambayo tayari tulishapeleka zaidi ya shilingi bilioni 88 na zimeendelea na utekelezaji wa miradi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia tathmini hiyo, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo ilikuwa inapata fedha kutokana na ushirika huo pamoja na maeneo mengine, ili kuweza kuhakikisha kuwa miradi ya maendeleo pamoja na maisha ya Watanzania hayaathiriki kutokana na mabadiliko ya kisera ya mbia yeyote wa maendeleo kutoka nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kujipanga kutumia rasilimali zetu, Mheshimiwa umeleta swali zuri sana. Serikali inaendelea na mkakati wa kuweza kufanya miradi ya ndani, ile iliyo mikubwa inayotumia rasilimali za ndani kuweza kuanza kufanya kazi ili kuhakikisha tunaongeza mapato ya ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya miradi hiyo kama ambavyo taarifa ya Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na taarifa ya Wizara ya Mipango na Uwekezaji wakati wa Bajeti za Kisekta ilibainisha kwamba Serikali imelipa fidia kwenye maeneo mengi ambayo ni ya kimkakati kiuwekezaji ili kuweza sasa kuanza kuwekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, Serikali imepiga hatua kwenye majadiliano ya miradi mikubwa ya kimkakati ambayo inaweza ikaingizia mapato makubwa nchi yetu ili kuweza na yenyewe kuanza kutekelezeka. Pia, Serikali inajipanga kuanza uzalishaji zaidi wa bidhaa zinazoweza kuzalishwa ndani ya nchi ili kuondokana na uagizaji wa bidhaa za aina hiyo ambazo Serikali ama nchi inaweza kuzalisha ndani ya nchi. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved