Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mariamu Nassoro Kisangi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti ongezeko la Wagonjwa wa Kansa nchini?

Supplementary Question 1

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako kwanza ninapenda niipongeze Serikali kwa jinsi ilivyowekeza katika afya, ni suala ambalo hatuwezi, ni lazima tuongee. Tulikuwa na Kituo cha Kansa cha Ocean Road, lakini sasa Tanzania nzima katika hospitali za rufaa za kanda kuna matibabu ya kansa; na hata kwenye hospitali binafsi nazo zimepewa vibali navyo vinatoa matibabu ya kansa. Tunaipongeza sana Serikali kwa jambo hilo kubwa. Kwa kweli elimu wanayoitoa ni kubwa sana, kansa watu wameanza kuielewa na wanapona wanaoenda mapema.

Mheshimiwa Spika, mimi kwangu ni ushauri, Serikali sasa ina mpango gani wa kufanya tafiti wa hizo kansa nyingine kama vile walivyoweza kudhibiti kansa ya mlango wa kizazi kwa akina mama?

Name

Dr. Godwin Oloyce Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Siha

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kweli kwa kutambua uwekezaji mkubwa uliowekezwa na Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Taasisi yetu ya Ocean Road; lakini sio taasisi yetu tu ya Ocean Road, hata kwenye hospitali zetu za kata.

Mheshimiwa Spika, unajua kule Mbeya kwako umepigania sana, kuna kazi inakwenda kuanza na kazi ya ujenzi imeanza kwa ajili ya kuhakikisha kwamba watu wa Mbeya hawatahitaji kwenda Ocean Road, lakini wakati huo huo kule Kanda ya Kaskazini na sehemu nyingine; kwa kweli na kutuweka katika nchi tisa Afrika bora kabisa ambazo zinatoa huduma za kansa.

Mheshimiwa Spika, nimwambie, siyo tu kwa hili suala la kansa ya kizazi, kuna suala la kansa nyingine zote, Serikali inaendelea kuongeza. Ukiona wananunua vifaa hivi, siyo tu kwa ajili ya kutibu, pia vinasaidia kutambua magonjwa mapema na pia kusaidia utafiti ili ukijua vyanzo vingine vinavyosababisha kansa ili viweze kuzuiliwa.

Name

Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti ongezeko la Wagonjwa wa Kansa nchini?

Supplementary Question 2

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, ugonjwa wa kansa ni ugonjwa ambao ni gharama sana kwa matibabu yake. Kwa kuwa tumekuwa tukishuhudia Watanzania wengi ambao wameathirika na ugonjwa huu, wakichangisha ili kuweza kwenda kutibiwa bila mafanikio, je, Serikali haioni kwamba kuna haja sasa walao kwenye ile package ya bima ya kawaida kabisa, ile ya chini, waweze kuweka matibabu haya ili huko mbeleni muweze kuyafanya yawe ya bure kwa Watanzania?

Name

Dr. Godwin Oloyce Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Siha

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kweli dada yangu Mheshimiwa Matiko ameuliza swali zuri sana, na maana ya bima ya afya kwa wote ni hicho anachokisema. Mimi kama Mbunge, na sisi kama Jamii ya Watanzania, sisi jamii ya Watanzania ukioa ni rahisi watu kuchangia shilingi milioni 100 uoe, lakini ukizaa mtoto akapata tatizo la kansa watu hawakupi hata shilingi 10 kwa ajili hiyo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, moja, kuna suala la mila zetu na jinsi sisi wenyewe tunavyoishi. Ni rahisi watu kufanya sherehe, lakini kwenda kwenye tiba yake na kukata bima anaona ni tatizo, lakini sherehe anaona ni kitu cha maana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni kweli ni muhimu kufanya hivyo, lakini kwa sasa kuna room ile ambayo tumesema kama mtu hawezi kulipia matibabu, basi kupitia mtendaji wa kata anaandikiwa barua na anapata tiba zote bure; na ndiyo kikubwa anachofanya na ndiyo maana tunatenga fedha hapa hizi za MSD na nyingine ndiyo maana mara nyingi hatuulizani tumetenga shilingi bilioni 200 kwa ajili ya dawa na vitendanishi na vifaatiba mbona hazijarudi, hazionekani kwenye mzunguko? Ni kwa sababu kuna fedha nyingi zinaenda kwenye eneo hilo. Pia, ni kweli kwamba siyo wote wanaweza kuhudumiwa kwa kutumia bilioni 200.

Name

Dr. Thea Medard Ntara

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti ongezeko la Wagonjwa wa Kansa nchini?

Supplementary Question 3

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, tatizo la tezi dume limeendelea kuongezeka hasa kwa watu wazima. Je, Serikali imejipanga vipi kutoa elimu ya dalili na kinga ili watu waelewe na kujikinga?

Name

Dr. Godwin Oloyce Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Siha

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwa kweli Serikali imejipanga kueleza dalili za magojwa yote na kutoa elimu ya uelewa kwa magonjwa yote ikiwepo tezi dume. Kwa kweli kwa sisi wanaume tunahitaji kuhamasishana kwa nguvu zaidi, sio suala tu la kujua ugonjwa lakini kwenda kwa wakati wote hospitalini kila baada ya miezi sita au mara mbili kwa mwaka kuhakikisha unapima afya yako kwa ujumla ili kuhakikisha wakati wote unaijua, na kama kuna ugonjwa wowote unaotokea uweze kugundulika mapema na kutibiwa mapema.

Name

Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti ongezeko la Wagonjwa wa Kansa nchini?

Supplementary Question 4

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, ahsante. Lishe bora ni njia mojawapo pia ya kudhibiti kansa. Je, Serikali ipo tayari sasa kutoa elimu kwa vyakula ambavyo vinaweza vikatumika mara nyingi ili kuzuia tatizo hilo?

Name

Dr. Godwin Oloyce Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Siha

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, Serikali ipo tayari kutoa elimu. Mojawapo ya elimu ni namna ya kula, kwa sababu kuna baadhi ya vyakula ambavyo vina vitamin nyingine kama Vitamin E na nyingine ambazo zina tabia ya kukamata zile vitu ambazo vinazunguka ndani ya mwili wa binadamu vinavyoweza kugonga seli na kusababisha seli nyingine ziache sasa kuwa controlled na ubongo mwisho wa siku vinasababisha kansa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kuna vyakula ambavyo ukila unapata hivyo ambavyo vinaondoa vitu vinavyosababisha suala hilo. Kwa hiyo, tunaendelea kuelimishana.

Mheshimiwa Spika, kama unakumbuka tulikuwa tunazungumzia watu wanaokufa kwa kukosa chakula huko miaka ya nyuma, lakini sasa hivi tunazungumzia watu wanaokufa kwa kula kupita kiasi. Kwa hiyo, pia kwenye suala la ulaji kwa maana ya kiasi na kufanya mazoezi na mambo mengine, hayo ndiyo mambo ya msingi ya kuhakikisha tunazingatia wakati wowote na kufuatilia.

Name

Salma Rashid Kikwete

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mchinga

Primary Question

MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti ongezeko la Wagonjwa wa Kansa nchini?

Supplementary Question 5

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nikupongeze wewe kwa kazi kubwa na nzuri ambayo unaifanya. Vilevile nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya katika Taifa letu la Tanzania.

Mheshimiwa Spika, kansa ni maradhi makubwa, kansa ni maradhi magumu. Sambamba na hilo, Serikali imefanya kazi kubwa kuhakikisha kwamba wanapeleka mashine kwa ajili ya kutambua au kwa ajili ya kufanya matibabu kwenye hospitali zote za rufaa. Swali langu ni kwamba, je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka mashine hizi kwenye hospitali za wilaya kwa sababu watu wengi hawana uwezo wa kufikia hizo hospitali za rufaa na wengi wapo vijijini na wanakufa kwa ajili ya maradhi haya makubwa?

Name

Dr. Godwin Oloyce Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Siha

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze mama yetu kwa swali zuri lenye umakini wa hali ya juu. Mimi niseme tu kwamba Serikali inafanya hivyo. Ndiyo maana sasa hivi siyo tu kwamba tunajitahidi kuhakikisha kwamba ule upimaji wa awali na kutambua kuanzia ngazi ya zahanati mpaka Taifa unafanyika, lakini pia umeona kuna madaktari wanaoitwa Madaktari wa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambao wanazunguka nchi nzima.

Mheshimiwa Spika, wanazunguka kwa kazi, kwa maana wakienda kule wanajenga uwezo kwa wataalam waliopo pale kwa magojwa husika kulingana na ubigwa wao, lakini pia wanatibu na kuacha ujuzi ili watu waweze kutambuliwa mapema.

Mheshimiwa Spika, ni kweli, kwa maana ya teknolojia, teknolojia hizi kubwa za utambuzi zimeishia kwenye level ya Hospitali ya Mkoa. Sasa Serikali inajipanga kutengeneza wataalam baada ya hapo ili kupeleka sasa teknolojia hizo kubwa kwenye ngazi ya wilaya, na ikiwezekana vituo vya afya kwa vile teknolojia ambazo zinaweza kuwa handled ni kwenye eneo la kituo cha afya.

Name

Neema Kichiki Lugangira

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti ongezeko la Wagonjwa wa Kansa nchini?

Supplementary Question 6

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, hivi punde Mheshimiwa Naibu Waziri ameelezea kwamba kuna vyakula ambavyo vinachangia kwenye ongezeko la magojwa ya saratani. Sasa ningependa kufahamu, je, ni lini sasa Serikali itaamua kulinda haki na afya za Watanzania kwa kurejesha suala la usalama wa chakula kwa maana ya food safety kuwa chini ya Wizara ya Afya kwa sababu kimsingi ni Wizara ya Afya ndiyo ambayo ina dhamana ya kuhakikisha kwamba walaji wanalindwa? Ahsante.

Name

Dr. Godwin Oloyce Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Siha

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge Lugangira, kwani kwenye eneo hili la lishe amekuwa kama balozi mzuri sana kwenye kulipigania. Nimwambie tu, sijasema kwamba kuna vyakula ambavyo vinasababisha, lakini nadhani kuna baadhi ya mambo yakifanyika ya kwenye vyakula yanasababisha patokee matatizo kama hayo unayozungumza.

Mheshimiwa Spika, ni kweli pia kwamba kuna hili suala la lishe, kwa maana ya usimamizi wa chakula na vitu vingine ipo kwenye eneo gani badala ya Wizara ya Afya kama ambavyo tumekwishakusema hapa? Mjadala huu unaendelea ndani ya Serikali. Mimi naamini tutafikia muafaka mzuri kwa sababu kila mtu ni mwathirika kama hatutazingatia yale ambayo yatatufanya sisi wote tuwe salama.

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Primary Question

MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti ongezeko la Wagonjwa wa Kansa nchini?

Supplementary Question 7

MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Spika, ninapenda kumwuliza Mheshimiwa Waziri, wamewekeza pesa nyingi sana za kujenga majengo kwa ajili ya kuweka mashine za saratani katika Hospitali ya Bugando lengo ikiwa ni kukifanya kitu kile kuwa ni cha umahiri lakini mashine zilizopo ni pungufu. Je, ni lini wataweka mashine ili kutosheleza mahitaji ya pale, hasa mashine aina ya liner accelerator? Ahsante.

Name

Dr. Godwin Oloyce Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Siha

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza, kwa kweli nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo wakati wote anapambania wananchi wake. Maana yake hata hili swali ambalo analiuliza hapa, pia ameandika barua kwa ajili ya kuikumbusha Wizara ya Afya suala hilo la hiyo machine kwenye hospitali hiyo.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, wewe unajua Serikali imeshawekeza pale zaidi ya shilingi bilioni saba kwenye eneo hilo la cancer na maana yake majengo yanaenda na kuna baadhi ya machine zimenunuliwa, na kwa maana ya bajeti ya mwaka ujao tunajipanga kwa ajili ya kuona namna ya kuhakikisha na eneo hilo linajitosheleza, kwa sababu lengo ni kupunguza mkusanyiko wa watu kwenye hospitali yetu ya Ocean Road, watu wabaki kwenye kanda zao na ikiwezekana wabaki baadaye kwenye mikoa yao. (Makofi)