Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Soud Mohammed Jumah
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Donge
Primary Question
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza: - Je, kuna mkakati gani kuimarisha uhifadhi wa mazingira ya Mradi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere ili kuhakikisha uendelevu wa Mradi huo?
Supplementary Question 1
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini ninayo maswali mawili kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza. Kwa kuzingatia umuhimu wa Bwawa la Mwalimu Nyerere na uhifadhi wake; je, Serikali ina mkakati gani wa kuwashirikisha wananchi wanaoishi pembezoni mwa Bwala la Mwalimu Nyerere ili kusaidia uhifadhi wa mazingira yake?
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Je, uwepo wa Bwawa la Mwalimu Nyerere umesaidia kwa kiasi gani kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama na kuweza kuepuka au kupunguza uharibifu wa misitu kutokana na matumizi ya kuni na mkaa? Ahsante sana.
Name
Khamis Hamza Khamis
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Uzini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Soud, amekuwa mdau mzuri sana wa mazingira na jambo kubwa la athari ya mabadiliko ya tabia ya nchi. Ushirikishwaji wa wananchi waliozunguka maeneo haya ya Bwawa la Mwalimu Nyerere ni wa kiasi kikubwa sana; na kwa sababu, tunafahamu wao ndio wapo karibu na bwawa hili, na kama ni wanufaika, basi wa mwanzo wanakuwa ni wao. Kwa hiyo, tumewapa jukumu la kuwashirikisha kusaidia katika kutunza na kuhifadhi mazingira ya maeneo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la kwanza ambalo tumelifanya ni kuwahimiza kupanda miti ambayo haikaushi vyanzo vya maji pembezoni mwa bwawa hili. Kwa kushirikiana na Maafisa wetu wa Mazingira, Mabolozi wetu wa Mazingira na wenzetu wa Halmashauri tumekuwa tukiwahimiza wenzetu hawa kwa kuwapa elimu ya mara kwa mara juu ya suala zima la usimamizi wa Sheria za Mazingira, lakini kubwa zaidi tumekuwa tunawaambia wawe wanafanya usafi. Lengo ni bwawa lile liendelee kuwa salama kwa sababu, tunachoamini ni kwamba maji ni mazingira, na mazingira ni maji.
Mheshimiwa Spika, kingine ni bwawa hili limesaidia ama linakwenda kusaidia kwa kiasi kikubwa matumizi ya nishati safi, hasa ya kupikia, na kuwaambia wananchi watoke katika matumizi ya nishati chafu. Kwanza, bwawa hili linakwenda kupeleka upatikanaji wa umeme wa uhakika, maana yake ni kwamba, watu ama wananchi wanakwenda kuacha kutumia kuni na mkaa na kutumia umeme, kama sehemu ya nishati.
Mheshimiwa Spika, sasa, kupitia bwawa hili, umeshafikishwa umeme mijini na vijijini, kitu ambacho wananchi wetu wanakwenda kuacha matumizi ya kuni na mkaa na kutumia nishati safi ya kupikia ambayo ni umeme. Nakushukuru. (Makofi)
Name
Prof. Patrick Alois Ndakidemi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Vijijini
Primary Question
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza: - Je, kuna mkakati gani kuimarisha uhifadhi wa mazingira ya Mradi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere ili kuhakikisha uendelevu wa Mradi huo?
Supplementary Question 2
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na juhudi za Serikali kuhifadhi Mlima Kilimanjaro, bado kuna changamoto kubwa ya kukata miti kwa kutumia chainsaw na kuranda mbao. Je, Serikali ina mikakati gani kukabiliana na hali hii?
Name
Khamis Hamza Khamis
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Uzini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Prof. Ndakidemi, kama ifuatavyo: Nataka nimwambie Mheshimiwa Mbunge, wananchi na Watanzania wote kwamba, suala la ukataji wa miti ni kosa kisheria, na suala la upandaji wa miti lipo kisheria.
Mheshimiwa Spika, nimwambie tu Mheshimiwa kwamba, Serikali ipo katika mkakati wa kuhakikisha tunawachukulia hatua wale wote ambao wanakata miti na misitu, ambayo ni sehemu ya mazingira, hasa maeneo yaliyozunguka katika vivutio na maeneo yaliyozunguka katika miradi mikubwa.
Mheshimiwa Spika, tutaendelea kuchukua hatua, lakini kubwa zaidi ni kuwaelimisha wananchi wasikate miti na badala yake wapande miti, hasa katika maeneo haya ya Kilimanjaro. Nakushukuru. (Makofi)
Name
Abdul Yussuf Maalim
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Amani
Primary Question
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza: - Je, kuna mkakati gani kuimarisha uhifadhi wa mazingira ya Mradi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere ili kuhakikisha uendelevu wa Mradi huo?
Supplementary Question 3
MHE. ABDUL YUSSUF MAALIM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nini mpango wa Serikali katika kutunza vyanzo vya maji, hasa vinavyopeleka maji katika Bwawa la Mwalimu Nyerere? (Makofi)
Name
Khamis Hamza Khamis
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Uzini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, upo mpango kabambe wa kutunza vyanzo vya maji vyote ambavyo vinapeleka maji katika Bwawa la Mwalimu Nyerere na vile ambavyo vinapeleka maji katika mabwawa, mito na maeneo mengine. Mpango wa kwanza ni kuhakikisha kwamba, tunawaambia wananchi wasimamie Mwongozo ule wa Mita 60 maana pale ndiyo kuna msingi wa uchafuzi na uharibifu wa vyanzo vya maji. Pale kuna wananchi wanalima, wanafanya shughuli za kilimo katika vyanzo vya maji, wengine wanafanya shughuli za viwanda katika vyanzo vya maji, wengine wanafuga katika vyanzo vya maji. Kwa hiyo, kwa kupitia mwongozo ule wa kusimamia sheria ya mita 60, tumekuwa tunaendelea kuwaelimisha wananchi sambamba na kuchukua hatua za kisheria kwa kuzingatia Sheria ya Mazingira. Nakushukuru. (Makofi)
Name
Abubakar Damian Asenga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilombero
Primary Question
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza: - Je, kuna mkakati gani kuimarisha uhifadhi wa mazingira ya Mradi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere ili kuhakikisha uendelevu wa Mradi huo?
Supplementary Question 4
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, je, Serikali inadhibiti vipi taasisi za mazingira zilizojitokeza kuchangisha wadau fedha na T-Shirt kwa madai ya kutunza mazingira ya bwawa, ili kuhakikisha taasisi hizo hazitumii michango hiyo kwa maslahi
binafsi?
SPIKA: Hebu rudia swali.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, je, Serikali inadhibiti vipi taasisi zetu hizi za mazingira ambazo zimejitokeza kule kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere, maana Jimbo la Kilombero lina sehemu ya Bwawa la Mwalimu Nyerere, kuchangisha fedha na vitu mbalimbali kwa madai ya kutunza mazingira kuhakikisha kweli zinatumika kwa kile wanachokichangisha?
Name
Khamis Hamza Khamis
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Uzini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abubakari Asenga. Ni kwamba, hili jambo tulikuwa hatuna taarifa nalo. Sasa nimwambie tu, tutalichukua, tutashirikiana na wenzetu wa nishati, halmashauri na mkuu wa wilaya tuone namna ambavyo tunalichulia hatua hili na kuwaambia Watanzania wote upandaji wa miti na suala la utunzaji wa mazingira lipo kisheria.
Mheshimiwa Spika, taasisi au mtu yeyote, ya/wa kitaifa au Kimataifa, ikiwa wanataka kupanda miti ni lazima wafuate sheria na utaratibu. Kwanza, waende Ofisi ya Mkuu wa Wilaya wakutane na maafisa wetu wa mazingira, waridhiwe, ndipo waje wafanye shughuli hiyo, siyo labda kupita kuchangisha kwa kisingizio cha jambo fulani, lakini hata hivyo tutalichukua twende tukalifanyie kazi. (Makofi)