Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Kavejuru Eliadory Felix
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Buhigwe
Primary Question
MHE. KAVEJURU E. FELIX aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya Mkoa wa Kigoma kuwa lango la biashara?
Supplementary Question 1
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya kuuliza. Moja, wafanyabiashara wa Mkoa wa Kigoma wamekuwa wakilalamika kwa muda mrefu juu ya tozo mbalimbali za ufanyaji wa biashara za mipakani. Upi mkakati wa Serikali wa kupunguza tozo hizo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Je, Wizara ya Viwanda, Biashara na TAMISEMI wapo tayari kukaa pamoja na wafanyabiashara wa Kigoma ili waweze kusikiliza changamoto zao?
Name
Exaud Silaoneka Kigahe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Kavejuru kwa sababu amekuwa akifuatilia sana maendeleo ya Mkoa wa Kigoma mahususi kwa wafanyabiashara na kuhakikisha wananufaika kulingana na jiografia na mipaka ya nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu hili suala la tozo, kama Serikali kwa ujumla wake, tozo na kodi nyingine, kupitia mpango wa kuboresha wafanyaji biashara na wawekezaji nchini (MKUMBI), Serikali inaendelea kuangalia namna ya kupunguza kero mbalimbali ambazo zimeelezwa katika mpango ule na mojawapo ni hii ya tozo na ada na ushuru mbalimbali ambao siyo rafiki kwa wafanyabishara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali kwa ujumla wake pamoja na kwa maana ya Wizara ya Fedha, Wizara ya Viwanda na Serikali kwa jumla tunaangalia hilo ili kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la pili, Serikali tumekuwa tukikaa na wafanyabishara katika mikoa yote na huwa tunafanya hivyo ili kusikiliza; kwanza maoni yao, lakini pia kutatua kero zao. Wizara ya Viwanda na Biashara, mwenyewe nimekuwa nikipita katika mikoa mbalimbali, tunafanya vikao kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa maana ya TAMISEMI, lakini pia na wenzetu Wizara ya Fedha na taasisi zote ili kuhakikisha tunawasaidia wafanyabiashara waweze kuwa shindani, pia kutoa maoni namna ya kuboresha ufanyaji biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kufanya hivyo na hasa Kigoma kwa sababu ni mkoa wa kimkakati, kama tulivyosema, tutaufungua ili uweze kuingia kwenye masoko haya makubwa ya DRC, Burundi na Rwanda na Afrika ya Kati ambako tuna hakika tuna soko kubwa la bidhaa za Tanzania. Nakushukuru.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved