Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Maimuna Salum Mtanda
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Newala Vijijini
Primary Question
MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kukabiliana na upungufu wa watumishi hususan Walimu na Watoa Huduma za Afya - Newala Vijijini?
Supplementary Question 1
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Serikali kwa majibu yake mazuri na pia katika ajira mpya ambazo inategemea kutangazwa, sisi wana Newala Vijijini tutakuwa wanufaika.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmashauri ya Wilaya ya Newala, na halmashauri nyingi za pembezoni, watumishi wengi wanaoenda kuajiriwa, wanaenda kupata cheque number, baada ya kupata cheque number wanaanza uhamisho na kurudi. Kwa hiyo, unakuta upungufu ni mkubwa sana. Hali hiyo inaathiri utendaji kwa kiasi kikubwa. Nilikuwa na maswali mawili ya nyongeza katika hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali haioni haja sasa kuchukuwa maoni ya wadau mbalimbali wakiwemo Waheshimiwa Wabunge kwamba, watumishi wanaoajiriwa hasa maeneo ya pembezoni, basi wawe wale wanaotoka katika maeneo yale ili kuondoa hii kadhia ya hamahama ya kila siku?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kwa kuwa hamisho nyingi ni za kubadilishana, lakini unakuta wanaoathirika ni sisi wana Newala Vijijini kwa maana ya Halmashauri ya Newala DC wa kwetu wanaondoka, lakini mbadala wake hawarudi. Je, Serikali haioni haja sasa wanapotoa kibali cha ruhusa ya kuhama inatoa barua zote mbili ili kuondoa lile gap ambalo linajitokeza katika maeneo yetu na kutoathiri utendaji kazi? Ahsante.
Name
Deus Clement Sangu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kwela
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Maimuna Mtanda, kwanza nimpongeze, amekuwa na jitihada kubwa sana ya kufuatilia mambo ya watumishi kwenye jimbo lake.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiyajibu maswali yote mawili kwa pamoja, ni kwamba kuna mambo mawili ambayo tumefanya Ofisi ya Rais Utumishi, kwanza tunafanya jambo linaitwa Human Resource Assessment kuona mahali ambapo watumishi wapo wengi na kufanya msawazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, zoezi hili tumefikia mwishoni na tunakwenda kufanya msawazo hasa kupeleka maeneo yale ya pembezoni ambayo yana watumishi wechache. Kuna maeneo kama ya mjini kuna watumishi wamejaa, na bado majukumu yao mengine hawatekelezi ipaswavyo wakati mahali pengine haswa mikoa ya pembezoni watumishi ni wachache.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la uhamisho, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tumeweka mfumo wa E-Uhamisho ambao kupitia mfumo huo huwezi kuhama. Kwanza kwa sasa mtumishi anayeajiriwa katika kituo kipya ni lazima ahudumu siyo chini ya miaka mitatu ndiyo aanze kuomba uhamisho. Ukiingia kwenye mfumo unakukatalia, unasema bado hau-qualify kupata uhamisho. Kwa hiyo, kwa sasa usumbufu uliokuwa unatokea huko nyuma, tatizo hili tumetafuta suluhisho la kudumu na watumishi wote watakaokuwa wanafika huko.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe rai kwa vijana wetu, wanapoomba ajira wanasema tupo tayari kufanya kazi mahali popote. Wanapopata tu barua ya kupewa kazi, wanaanza kulalamika kwamba tunataka twende mijini. Sasa hili jambo kama Serikali tumelidhibiti hasa kuokoa changamoto ya wafanyakazi kwa mikoa ile ya pembezoni ambayo vijana wengi wamekuwa wakiomba uhamisho kwenda mijini.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved