Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Boniphace Mwita Getere
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda
Primary Question
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:- Je, kwa nini vijiji vyenye maeneo ya mnada havipati mgao wa 20% ya mapato ya mnada?
Supplementary Question 1
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu haya ya Serikali, Kijiji cha Mgeta kimekuwa na mnada kwa muda mrefu sana na kimekuwa na madai ya zaidi ya shilingi milioni 221. Sheria ya Halmashauri Na. 08 inataja wazi kwamba vijiji vyenye maeneo yanayotoa mradi wanapewa 20%, maana yake asilimia nne ya kata na 16% ya vijiji na itakwenda kwenye vitongoji. Sasa ni lini Serikali itatoa maelekezo ya Mnada wa Mgeta ili Wanakijiji wa Serikali ya Kijiji cha Mgeta kupewa fedha zao? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Mnada wa Hunyari hauna uzio, ni lini sasa Serikali itajenga uzio kwenye mnada wa Hunyari? (Makofi)
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Boniphace Getere kwa maswali yake haya mawili mazuri. Ninaomba nitumie nafasi hii kuendelea kuwakumbusha Wakurugenzi katika Mamlaka zetu za Serikali za mitaa kuzingatia Mwongozo wa Bajeti ambao unazitaka halmashauri kutenga fedha kupitia mapato ya ndani kuzirudisha katika vijiji vyetu katika kata kwa kuzingatia daraja la halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mpaka wakati huu fedha za uendeshaji ambazo tayari zimetoka na kwenda katika Kata, Vijiji na mitaa ni shilingi bilioni 4.69, lakini tunataka tuendelee kuhakikisha kwamba vijiji vyetu hivi, kata, mitaa na vitongoji havikosi fedha kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli zake ndogo ndogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba nitoe msisitizo huo, Wakurugenzi wote wa Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa waweze kuzingatia mwongozo huu wa bajeti uliotolewa na warudishe hizi fedha katika ngazi hizo kwa ajili ya kuendesha shughuli zao. Maelekezo haya yanaenda pia katika Kijiji cha Mgeta na chenyewe kiweze kupelekewa fedha inazostahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na eneo la Mnada wa Hunyari, ninaomba pia nitumie nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kumwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri aweze kuweka katika mipango na bajeti kupitia mapato ya ndani ya halmashauri ili waweze kuona namna gani wanajenga uzio katika eneo hili la mnada. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved