Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dr. Medard Matogolo Kalemani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chato
Primary Question
MHE. DKT. MEDARD M. KALEMANI aliuliza: - Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa vituo vya afya Kata za Nyamilembe, Kasenga na Ilyamachele vilivyoanza kujengwa kwa nguvu za Wananchi?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. MEDARD M. KALEMANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali. Pia, ninaomba nifikishe shukurani nyingi sana za wananchi wa Kasenga kwa Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia kwa kutoa fedha shilingi milioni 250. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa wananchi wa Ilyamchele, na Nyamilembe wana hamu sana na kujengewa vituo vya afya, lakini imechukua muda mrefu. Mheshimiwa Naibu Waziri, ni lini fedha hizi za ujenzi wa vituo vya afya vya Kata ya Nyamilembe na Ilyamchele zitatolewa?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa wananchi wana hamu na shauku kubwa kuona uhakika wa Serikali kwenye ujenzi wa vituo vya afya hivi viwili; ninamwomba Mheshimiwa Naibu Waziri kama yuko tayari awahakikishie wananchi wa Nyamilembe na Ilyamchele, ni lini yupo tayari tufuatane mimi na yeye tukaone hamu yao na kuhakikisha kwamba vituo vya afya vitajengwa kwa haraka? (Makofi)
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Medard Kalemani, kwa kweli anapaza sauti yake kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma bora kabisa za afya msingi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilipokuwa kwenye ziara katika jimbo lake, kwa kweli alizungumza na nikamhakikishia na ninaomba niendelee kumhakikishia kwamba Serikali ya Awamu ya Sita ipo kazini na ndiyo maana utaona fedha tayari zimeshaanza kuja.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii shilingi milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la kuhudumia wagonjwa (OPD) katika Kituo cha Afya cha Kasenga, tayari imekuja, lakini kuna fedha nyingine kupitia Mfuko wa TASAF ambayo itaenda kwenye Kituo cha Kata ya Nyamilembe na yenyewe inakuja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, kuna shilingi milioni 250 ambayo inaletwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mwaka huu wa bajeti kwa ajili ya kujenga kituo cha afya cha kimkakati katika Jimbo lako. Kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, ataona dhamira kabisa ya dhati kutokana na fedha hizi kwa kadiri zinavyokuja.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba Wananchi wa Chato wasikie kwamba katika Kata ya Ilyamchele pamoja Kasenga, Serikali italeta fedha kwa ajili ya kuhakikisha vituo hivi vya afya vinajengwa na vinaweza kuwahudumia wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili kwamba lini nipo tayari kuongozana naye katika Jimbo lake kwenda kuongea na wananchi wake, na kuonesha ni kwa kiasi gani Serikali ya Awamu ya Sita inafanya uwekezaji mkubwa sana katika upande huu wa afya msingi. Mheshimiwa Mbunge tutakaa tuzungumze tupange ili tuweze kufanya ziara hii. (Makofi)
Name
Sylivia Francis Sigula
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DKT. MEDARD M. KALEMANI aliuliza: - Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa vituo vya afya Kata za Nyamilembe, Kasenga na Ilyamachele vilivyoanza kujengwa kwa nguvu za Wananchi?
Supplementary Question 2
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Kata ya Kala, Wilaya ya Nkasi wanamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuwapatia shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya pamoja na gari la wagonjwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kituo ni kizuri sana na kimekamilika na gari lipo, ila hakijaanza kutoa huduma. Je, ni lini hasa huduma zitaanza kutolewa ili wananchi wapunguze adha ya kutembea kilometa 150 kufuata huduma makao makuu? (Makofi)
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Sylvia Sigula kwa swali lake hili zuri kabisa kwa maslahi ya wananchi wa Nkasi. Pia ninaomba nitumie nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kumwagiza Mkurugenzi akishirikiana na DMO na RMO waweze kufanya taratibu zote za Kiserikali ambazo zitawezesha vituo hivi kuanza kutoa huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama kuna compliance yoyote, wafanye mawasiliano na Wizara ya Afya kwa ajili ya kituo hiki muhimu kabisa ambacho kimejengwa na ambacho tayari Mheshimiwa Rais ameleta gari la wagonjwa kianze kutoa huduma bora za afya kwa wananchi. (Makofi)
Name
Saashisha Elinikyo Mafuwe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hai
Primary Question
MHE. DKT. MEDARD M. KALEMANI aliuliza: - Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa vituo vya afya Kata za Nyamilembe, Kasenga na Ilyamachele vilivyoanza kujengwa kwa nguvu za Wananchi?
Supplementary Question 3
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninawapa pole wananchi wa Jimbo la Hai kwa kuondokewa na Baba Askofu Dkt. Emmanuel Lazaro, Mwasisi wa Kanisa la TAG. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaishukuru Serikali ilituletea fedha shilingi milioni 250 tukaanza ujenzi wa Kituo cha Afya Nkwansira na sasa kinatoa huduma. Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta fedha shilingi milioni 250 awamu ya pili? (Makofi
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Saashisha Mafuwe ambaye amekuwa akifanya ufuatiliaji wa karibu sana kuhakikisha kwamba sekta ya afya msingi inaimarika katika jimbo lake.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali ilileta shilingi milioni 250 kwa ajili ya kuanza majengo ya awali ya kituo hiki cha afya na tayari kituo hiki cha afya kimeanza kutoa huduma. Sasa kazi ya Serikali ni kuendelea kuleta fedha, tutaleta shilingi milioni 250 kwa ajili ya majengo ya awamu ya pili ili kituo hicho cha afya kiwe kina majengo yote yanayohitajika kwa ajili ya kutoa huduma bora kabisa ya afya. (Makofi)
Name
Joseph Kasheku Musukuma
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita
Primary Question
MHE. DKT. MEDARD M. KALEMANI aliuliza: - Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa vituo vya afya Kata za Nyamilembe, Kasenga na Ilyamachele vilivyoanza kujengwa kwa nguvu za Wananchi?
Supplementary Question 4
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana. Tumepokea barua za ujenzi wa vituo vya afya shilingi milioni 250, lakini mpaka sasa fedha hazijaja na Mfumo wa Serikali ni kama bado una wiki mbili tu usitoe tena fedha mpaka mwakani. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri ni lini sasa fedha hizo zitaachiwa ili tukimbizane na kujenga vituo vya afya? (Makofi)
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Joseph Kasheku kwa swali lake hilo zuri kabisa lenye maslahi kwa ajili ya wananchi wake, lakini kwa ajili ya Wabunge wote waliomo humu. Ni kweli kabisa, Serikali ya Awamu ya Sita kwa kipekee kabisa imetenga bajeti ya shilingi bilioni 53.5 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya vya kimkakati katika majimbo 214.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nitoe taarifa hii kwamba katika mwaka huu wa bajeti, fedha hizi zitaanza kutoka kufika katika vituo hivi vya afya ili viweze kujengwa na viweze kutoa huduma bora ya afya kwa ajili ya wananchi. Ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Joseph Kasheku, kwamba kabla ya mwaka wa fedha haujaisha fedha hizi zitakuwa zimefika katika kituo hiki cha afya cha kimkakati katika jimbo lake kwa ajili ya kuanza kujenga majengo ya awali.
Mheshimiwa Naibu Spika, vivyo hivyo, kwa baadhi ya Waheshimiwa Wabunge pia na fedha hizo zitaanza kutoka kwa ajili ya majengo hayo ya awali katika hivi vituo vya afya ya kimkakati.