Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Francis Isack Mtinga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Iramba Mashariki
Primary Question
MHE. FRANCIS I. MTINGA aliuliza: - Je, lini Serikali itatekeleza ahadi ya ukarabati wa Vituo vya Afya Mkalama na Kinyangiri ambavyo ni chakavu?
Supplementary Question 1
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu yanayotia moyo kiasi ya Serikali, Kituo cha Afya Kinyangiri na Kituo cha Afya Mkalama nikisema vikongwe ni vikongwe kweli kweli, hata hadhi ya zahanati za sasa haina.
Mheshimiwa Naibu Spika, Makamu wa Rais, wakati huo ambaye sasa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano, aliahidi ukarabati kwenye vituo hivi, akaja Katibu Mkuu wa CCM akawaahidi wananchi ukarabati wa vituo hivi, na wananchi wamekuwa wakisubiri kwa hamu sana muda mrefu mno.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali sasa haioni kwamba vituo hivi viwili vinapaswa kupewa udharura na vitolewe kwenye utaratibu huu alioujibu wa kusubiri kwanza hospitali 50 na viingizwe kwenye ukarabati angalau kwenye vituo vya afya vya sasa vya kimkakati, ipate angalau shilingi milioni 250 kila kituo ili kutimiza ahadi ya wananchi hawa ambao wamesubiri kwa muda mrefu sana?
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nimpongeze Mheshimiwa, Francis Mtinga kwa swali lake linalolenga kuboresha sekta ya afya msingi katika jimbo lake. Kwa hakika amekuwa akipaza sauti. Ninaomba nimhakikishie kwamba Serikali ya Awamu ya Sita ina dhamira ya dhati ya kuendelea kuimarisha sekta hii muhimu ya afya msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na uhitaji wake wa vituo hivi vya Afya vya Mkalama na Kinyangiri ambavyo ni chakavu, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwanza Bunge hili Tukufu limepitisha nyongeza ya bajeti, ambapo kuna shilingi bilioni 53.5 ambazo zinatoka kwa ajili ya kuhakikisha kwamba milioni 250 inaenda katika kila jimbo kwa ajili ya kuanza kujenga vituo vya afya vya kimkakati, na Mheshimiwa Mbunge, amekuwa akisemea kwa upande huu. Kwa hiyo, ninaomba apate taarifa kwamba katika jimbo lake inakuja shilingi milioni 250 kwa ajili ya kujenga kituo cha afya cha kimkakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na ukarabati wa hivi vituo vya afya viwili alivyovitaja, kwa sababu Serikali tayari imeanza kutenga fedha, imeanza kujenga vituo vya afya vya kimkakati, ninaomba nimhakikishie kwamba tayari hospitali kongwe zinafika mwisho wa kukarabatiwa na sasa tunaingia katika kukarabati vituo vya afya, na vituo vya afya hivi viwili tutavifikia kwa ajili ya kuhakikisha kwamba vinakarabatiwa na vinakuwa katika hali nzuri ili viweze kutoa huduma bora kwa wananchi wako.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved