Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Salim Mussa Omar
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Gando
Primary Question
MHE. SALIM MUSSA OMAR aliuliza: - Je, Serikali haioni haja ya kutengeneza Kanuni zitakazoweka kima cha chini cha mishahara ya Wafanyakazi wa Majumbani?
Supplementary Question 1
MHE. SALIM MUSSA OMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana kwa majibu ya Serikali yenye kutia matumaini. Hata hivyo, ni dhahiri kwamba wafanyakazi wa ndani wanaendelea kunyanyasika sana kwa asilimia kubwa. Wafanyakazi hawa unakuta wanafanya kazi usiku, mchana, mwezi mzima na kiwango anacholipwa hakiridhishi, inafikia mahali mtu ambaye ana mfanyakazi huyo ana kipato zaidi ya shilingi milioni 20 kwa mwezi, lakini mfanyakazi huyo anapokea siyo zaidi ya shilingi 60,000. Huu siyo utu, hii ni biashara ya utumwa ambayo imekwishapitwa na wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ruhusa yako ninaomba sasa Serikali iangalie hili jambo serious, kwa sababu unyanyasaji unaoendelea nyumbani ni mkubwa sana na ndugu zetu wanaumia sana. Ahsante sana.
Name
Paschal Katambi Patrobas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Shinyanga Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Salim Mussa Omar.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa swali hilo zuri na kuonesha kujali, hasa kwenye manyanyaso ambayo yanafanyika kwa wafanyakazi wa ndani. Hata hivyo Serikali yetu imekuwa na sheria, ukiacha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzani, kuhusiana na haki na usawa wa kazi kwa mujibu wa Ibara ya 23, lakini pia kuzuia unyanyasaji na ubaguzi kwa mujibu wa Ibara ya 12 na 13 ya Katiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, vivyo hivyo, tunayo Sheria ya Kazi, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, ambayo inatoa mwongozo wa namna gani kazi ziwe za staha na pia kuwe na sehemu ya afya na usalama mahali pa kazi, kwa maana ya misingi hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufanya hivyo, kwanza kwenye eneo la malipo tunayo amri ya kima cha chini cha mshahara ambayo tuliitunga na kuitoa mwaka 2022 na pia sambamba nayo tuna utaratibu sasa ambao tumeanza kwenye hatua ya kusaini na ku-ratify convention Na. 189 ambao ni Mkataba wa Kimataifa, ambao utazungumzia kuhusiana na uwepo wa haki za wafanyakazi wa nyumbani.
Mheshimiwa Naibu Spika, mojawapo ya haki zinazoangaliwa ni pamoja na masaa ya kazi, kuwa na mikataba ya kazi na pia kuhakikisha kwa wakati wote wanapata haki na stahiki zao na malipo yanayostahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, masuala ya unyanyasaji yamekuwa yakijitokeza; wapo wafanyakazi wa ndani ambao wanapewa ujauzito na kufukuzwa, wapo wanaonyimwa chakula, na pia wapo wanaofanya kazi masaa yote. Hayo yote tumekuwa tukiyaangalia na kuyazingatia kwa kutumia Sheria yetu ya Kanuni za Adhabu Sura Namba 16.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hatua hii ya kwenda kufunga mkataba huu kupitia Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan na jitihada kubwa zinazofanywa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, chini ya Mheshimiwa Gwajima, pia nikitambua kazi kubwa inayofanywa na Umoja wa Wanawake Tanzania wa Chama cha Mapinduzi, kupitia Mheshimiwa Mama Chatanda na Wabunge Wanawake, wamekuwa pioneers wa kupigania haki za wafanyakazi wa nyumbani, wa kike na kiume, ni ili kuweza kuhakikisha haki zao na stahiki zao wanazipata kwa mujibu wa sheria. Ahsante.
Name
Rashid Abdallah Shangazi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlalo
Primary Question
MHE. SALIM MUSSA OMAR aliuliza: - Je, Serikali haioni haja ya kutengeneza Kanuni zitakazoweka kima cha chini cha mishahara ya Wafanyakazi wa Majumbani?
Supplementary Question 2
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kujua haki za wafanyakazi hawa, siyo mishahara pekee, bali ni pamoja na haki nyinginezo, ikiwemo likizo, matibabu na kadhalika. Je, ni kwa kiasi gani Serikali inahakikisha kwamba haki hizi inazisimamia na kuhakikisha kwamba wafanyakazi hawa wanazipata?
Name
Paschal Katambi Patrobas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Shinyanga Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba katika haki ambazo nilizitaja hapo awali, zitakuwa ni haki ambatano za kimkataba wa Kimataifa, lakini pia na domestic laws, kwa maana ya sheria zetu za ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya stahiki za haki hizi za wafanyakazi wa ndani, watakuwa na haki sawa kama wafanyakazi wengine tu kwenye sekta mbalimbali. Zitaangalia masuala pia hata ya umri wa kufanya kazi, masaa ya kufanya kazi, mazingira ya kufanya kazi na pia masuala ya likizo, ikiwa ni pamoja na matibabu, na kuchangiwa fedha zao kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, itakuwa ni haki ambatano ambazo zitakuwa tumezifanya na hasa tukishaingia katika mchakato huu wa kusaini na ku-ratify Mkataba wa Kimataifa Na. 189 na kuweza kubadilisha sheria zetu za ndani ili kuweza kuhakikisha kwamba tunasimamia kikamilifu haki zao. Ahsante.
Name
Catherine Valentine Magige
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. SALIM MUSSA OMAR aliuliza: - Je, Serikali haioni haja ya kutengeneza Kanuni zitakazoweka kima cha chini cha mishahara ya Wafanyakazi wa Majumbani?
Supplementary Question 3
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Pamoja na kwamba viongozi wetu wa UWT Taifa wakiongozwa na mama Mary Chatanda wamekuwa mstari wa mbele kupinga ukatili dhidi ya wanawake, watoto na hata wanaume, je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha ukatili huu wa wasaidizi wa ndani unakoma kabisa, kwa sababu kuna wengine wanabakwa, wananyimwa chakula na hata kupigwa?
Name
Paschal Katambi Patrobas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Shinyanga Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, nijibu swali la Mheshimiwa Catherine Magige, kwamba ni kweli mazingira hayo yamekuwa yakijitokeza katika nyakati tofauti, lakini tumeendelea kama Serikali kuchukua hatua kupitia sheria ya kanuni za adhabu.
Mheshimiwa Naibu Spika, makosa yoyote ya unyanyasaji, makosa yoyote ya kuvunja haki za binadamu, yanaelezwa na kusimamiwa na sheria ya kanuni za adhabu. Ikitokea imebainika mfanyakazi wa ndani amenyanyaswa kwa namna yoyote ile, hatua kali za kisheria zinachukuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba na kutoa rai kwa niaba ya Ofisi ya Waziri Mkuu, kwamba ikitokea kuna manyanyaso maeneo yoyote, ni wajibu wa jamii sasa kuripoti jambo hilo katika uongozi wa Serikali za Mitaa ama Polisi ili taarifa hizo ziweze kuchukuliwa na kwenda kufanyiwa kazi kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa na kudhibiti makosa hayo.
Name
Neema Kichiki Lugangira
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. SALIM MUSSA OMAR aliuliza: - Je, Serikali haioni haja ya kutengeneza Kanuni zitakazoweka kima cha chini cha mishahara ya Wafanyakazi wa Majumbani?
Supplementary Question 4
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nimemsikia Mheshimiwa Naibu Waziri, amesema Tanzania tunajipanga kwenda kufanya ratification ya ule Mkataba wa Kimataifa (ILO Convention 189), lakini Convention hii toka ipitishwe ni tangu mwaka 2011. Kwa hiyo, mpaka leo ni takribani miaka 22. Je, ni lini sasa mchakato huu utakamilika na Tanzania tutaridhia huu mkataba wa ILO 189 ili tusijikute tunasubiri tena miaka 22 mingine?
Name
Paschal Katambi Patrobas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Shinyanga Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, nijibu swali la Mheshimiwa Lugangira kwamba, kuna msemo wa wahenga, wanasema what is common to others is not common to all. Ni kwamba, ni kweli mkataba huu wa Kimataifa unaweza ukawa umepitishwa kwa nchi za wenzetu miaka ya 2011, lakini katika kuingia mikataba ya Kimataifa ambalo Mheshimiwa Mbunge anapaswa ajue kuna masuala mengi ya kuangalia customs zetu kwa maana ya mila, tamaduni na desturi, tunaangalia na pia relevance ya nchi na nchi, na pia tunaangalia masuala ya kiuchumi na mambo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba kwenye mambo yale ambayo yameingia kwenye mkataba ule, yapo ambayo tayari sheria zetu yanazitambua hata kabla ya wao kuingia mwaka 2011. Sisi tumeanza, ukiangalai kwa mfano Sheria ya Kazi iliyokuwepo ya Mwaka 1981, tayari ilikuwa inazingatia kazi za staha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kuna mambo mengi ambayo tayari kabla hata ya convention sisi tulikuwa tuko mbele zaidi, tumebakiza machache sana ambayo tunaendelea kuyafanyia kazi tuingie kwenye saini na ratification.
Name
Dr. Thea Medard Ntara
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. SALIM MUSSA OMAR aliuliza: - Je, Serikali haioni haja ya kutengeneza Kanuni zitakazoweka kima cha chini cha mishahara ya Wafanyakazi wa Majumbani?
Supplementary Question 5
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana. Ninarudia, ni miaka minne tumelizungumza hilo suala ndani ya hili Bunge, Mkataba wa C 189 mtauleta lini ndani ya hili Bunge?
Name
Paschal Katambi Patrobas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Shinyanga Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, nijibu swali la Mheshimiwa Thea, tayari Serikali imeshalifanyia kazi na tumeshafanya uchambuzi kwenye ngazi ya Wizara, inaenda kwenye mamlaka nyingine kwa mujibu wa sheria ili kuweza kuhakikisha kwamba mkataba huo, tuliokuwa tunatarajia kuuleta kwa Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Bunge hili, kwa hiyo, kama hatua ambazo tumezipeleka kwenye ngazi nyingine wakifanya haraka, basi tutaweza kuupitisha mkataba huo.