Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Festo Richard Sanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makete
Primary Question
MHE. FESTO R. SANGA aliuliza: - Je, lini Serikali itafikia makubaliano na kampuni zinazotoa huduma ya Internet kwa Satellite duniani kutoa huduma hapa nchini?
Supplementary Question 1
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, Mheshimiwa Waziri utakubalina nami kwamba, siyo maeneo yote ya nchi hii network inashika. Naweza nikasafiri kutoka Dodoma hadi nafika Makete kuna maeneo mengi network haishiki, lakini hiyo ni pamoja na maeneo mengine nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja kati ya maelekezo ya Rais ya tarehe 13 Mwezi Mei, 2023 yalikuwa siyo muhimu kuendelea kujenga minara kwenye nchi nzima, sasa twende kwenye satellite. Ni ipi kauli ya Serikali kuwa na satellite yake kwenye suala la internet kwenye Taifa letu la Tanzania?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lingine, internet inakuja na mambo mema na inakuja na mambo mabaya. Siku ya jana na leo ...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Sanga, subiri. Waheshimiwa Wabunge, naomba utulivu! Waheshimiwa Wabunge, tunaomba utulivu ndani ya Bunge!
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, internet inakuja na mambo mema na mambo mabaya. Siku ya jana na leo tumeona page rasmi za taasisi mbalimbali za Serikali zimekuwa zikipata mtikisiko. Sasa kwa nafasi hii ya swali hili, ni ipi kauli ya Wizara ya Mawasiliano kwa Watanzania kuelekea tukio hili ambalo limekuwa likichafua taasisi na viongozi wetu wa Serikali kwa kipindi hiki?
Name
Jerry William Silaa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ukonga
Answer
WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa na ninaomba kwa ruhusa yako nimjibu Mheshimiwa Sanga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, moja, ni dhahiri Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa maelekezo ya nchi yetu kurusha satellite yake. Kwenye Hotuba yangu ya Bajeti hapa wiki iliyopita nilielezea ziko hatua ambazo tumeanza, kuzichukua ikiwemo kuanza mchakato wa uridhiaji wa mikataba miwili: Mkataba wa Sheria za Kanuni za Nchi za Utafiti wa Anga ya Juu wa Mwaka 1967, na Mkataba unaosimamia Usajili wa Vyombo vya Anga za Juu wa Mwaka 1975. Kwa hiyo, maelekezo ya Mheshimiwa Rais, yanatekelezwa, na ninalihakikishia Bunge lako kwamba, nchi yetu itarusha satellite yake yenyewe kusaidia mawasiliano ikiwemo mawasiliano ya internet. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, ni suala la usalama wa mitandao yetu na mifumo yake. Naomba kulithibitishia Bunge lako kwamba, Serikali kupitia TCRA inasimamia usalama wa mifumo yetu na mifumo yetu ipo salama salimini. Siku ya jana, page za Mitandao ya Kijamii chache, mbili za taasisi za Serikali ziliingiliwa, na tunaposema account ya mtandao wa kijamii siyo mfumo perse wa TEHAMA wa taasisi ya Serikali. Ni account ambayo hata mimi na wewe tunayo, ni account ambazo taasisi hizi kupitia Maafisa wake wengine wa ngazi za chini wanaweza kutumia hata simu ya mkononi ku-login kwa ajili ya kufanya habari mbalimbali za taasisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, zile taratibu zao za kiusalama zilikuwa siyo thabiti na ikasababisha kuingiliwa. Mitandao hiyo ama account hizo zimesharejeshwa, na Wizara yangu na taasisi nyingine za Kiserikali zinaendelea kufanya kazi kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali, kuhakikisha accounts za Mitandao ya Kijamii ziko salama, lakini kifumo yetu yote iko salama. Serikali itaendelea kusimamia jambo hili kwa kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa salama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved