Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Hussein Nassor Amar
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nyang'hwale
Primary Question
MHE. HUSSEIN N. AMAR K.n.y. MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza: - Je, Serikali haioni haja ya kukifufua Kiwanda cha Pamba na Mafuta Kasamwa kwa kuwa hivi karibuni nchi ilikabiliwa na uhaba wa mafuta?
Supplementary Question 1
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, kwa kuwa kiwanda kile kilikuwa kikitoa ajira kwa vijana wetu na upatikanaji wa mafuta kwa gharama nafuu, je, kiwanda hiki kitaanza lini matengenezo na kuanza kufanya kazi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa sababu Wilaya ya Nyang’hwale ni wakulima wazuri wa pamba, je, Serikali ina mpango gani wa kutafuta wawekezaji ili na sisi tuweze kujengewa kiwanda cha kuchambua pamba na kukamua mafuta Wilaya ya Nyang’hwale? (Makofi)
Name
Exaud Silaoneka Kigahe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake, lakini ufuatiliaji kuhusiana na viwanda hasa kwenye Wilaya ya Nyang’hwale na Jimboni kwake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, Serikali itavifufua viwanda karibu vyote vilivyobinafsishwa na vilivyokufa na hasa kwenye sekta hii ya pamba kupitia Ushirika. Vyama vya Ushirika tayari tumeshafanya tathmini na ndiyo maana tumewasaidia ili waweze kupata mikopo hii kwenye Benki zetu za Kilimo, lakini na hizi za Uwekezaji ikiwemo hii Azania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, siyo tu Kiwanda hiki cha Kasamwa lakini pia na viwanda vingine ambavyo vilikuwa vimefungwa, tunataka vifufuliwe vyote kwanza kama nilivyosema vya kuchambua pamba. Pili, mbegu zitakazopatikana kwenye kuchambuliwa pamba ndiyo zitakazopelekwa kuzalisha mafuta katika viwanda hivyo. Kwa hiyo, na viwanda hivi vingine vitafuata.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Wilaya yake ya Nyang’hwale, Serikali hasa itaendelea na utaratibu huu huu wa kuwasaidia, lakini na kuwahamasisha zaidi wakulima, kwa sababu changamoto tuliyonayo ni upatikanaji wa malighafi kwa ajili ya viwanda hivi. Kwa hiyo, nnawahakikishia Wananyang’hwale na Mheshimiwa Mbunge kwamba, Wizara ya kilimo imepanga kuongeza uzalishaji wa mbegu ili mbegu hizo zitumike kwenye hivi viwanda kuzalisha mafuta ya kula. (Makofi)
Name
Amandus Julius Chinguile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nachingwea
Primary Question
MHE. HUSSEIN N. AMAR K.n.y. MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza: - Je, Serikali haioni haja ya kukifufua Kiwanda cha Pamba na Mafuta Kasamwa kwa kuwa hivi karibuni nchi ilikabiliwa na uhaba wa mafuta?
Supplementary Question 2
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Serikali imefikia hatua gani kuhusu kufufua kiwanda cha kubangua korosho na kiwanda cha kuzalisha mafuta ya kula vilivyoko katika Jimbo langu la Nachingwea? (Makofi)
Name
Exaud Silaoneka Kigahe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pia, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Amandus kwa ufuatiliaji kuhusiana na viwanda vya korosho. Kwa kuwa tunajua Serikali inategemea sana zao la korosho kuingiza mapato, lakini pia na wananchi kwa maana ya wakulima na hasa kwenye hiyo Mikoa ya Kusini ikiwemo kule Nachingwea.
Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda hivi vya korosho na kile cha mafuta cha Ilulu ni moja ya viwanda ambavyo vilikuwa vimebinafsishwa, lakini kwa sababu vilikuwa havifanyi kazi vizuri, vilivirejeshwa Serikalini na kuviweka kwenye utaratibu wa usimamizi chini ya Mamlaka ya Uwekezaji na Mauzo ya Nje (EPZA).
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari tumeshapata wawekezaji chini ya utaratibu huo, kile cha kubangua korosho tuna Mwekezaji mmoja ANH & Raka Limited ambao wako chini ya EPZA; lakini kile Kiwanda cha Mafuta cha Ilulu nako pia tuna Mwekezaji mwingine mpya ambaye ameingia mkataba na EPZ ambaye anaitwa MCL Agro Company Limited nao hawa wanakwenda kuzalisha mafuta kupitia kukamua ufuta, karanga na mbegu nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutaendelea kuvifanyia kazi, kuvutia uwekezaji katika viwanda vya korosho Mikoa ya Kusini ikiwemo Nachingwea, ili tuhakikishe tunaongeza thamani badala ya kuuza malighafi hasa korosho ambayo tunaitegemea sana kama zao la biashara. (Makofi)
Name
Dr. John Danielson Pallangyo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Arumeru-Mashariki
Primary Question
MHE. HUSSEIN N. AMAR K.n.y. MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza: - Je, Serikali haioni haja ya kukifufua Kiwanda cha Pamba na Mafuta Kasamwa kwa kuwa hivi karibuni nchi ilikabiliwa na uhaba wa mafuta?
Supplementary Question 3
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Tunatambua kwamba, Serikali iko kwenye mpango wa kufufua zao la pareto Kisimiri Juu, ambako lilikuwa linalimwa kwa wingi miaka ya 1960 na 1970. Sasa, je, ni upi mpango wa Serikali kufufua kiwanda cha pareto kwa ajili ya kuchakata hilo zao, lakini pia kuhakikisha kwamba kunakuwa na soko na vijana wanapata ajira?
Name
Exaud Silaoneka Kigahe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nampongeza sana Mbunge Mheshimiwa Dkt. Pallangyo kwa ufuatiliaji kwenye hii sekta ya kilimo na mahsusi kwenye sekta ya pareto. Ni kweli zao hili miaka ya 1970 lilikuwa ni zao muhimu sana kwa ajili ya kuongeza kipato kwenye sekta ya kilimo na siyo tu kwake kule, lakini pia na kwa Mikoa ya Iringa, Mbeya, na maeneo yote ambayo yanalima pareto.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeshaanza kufanya juhudi kubwa za kufufua viwanda hivi ikiwemo kile kiwanda cha pareto pale Mafinga, ambacho nacho kinazalisha lakini bado hakipati malighafi ya kutosha. Pia na kwake kule, ambako tukishapata malighafi ya kutosha kwa maana ya pareto ikilimwa kwa wingi, tutahakikisha tunahamasisha wawekezaji ili waweze kuwekeza pale kwenye jimbo lake. Tayari tuna wengine ambao wamewekeza kule Mbeya, kwa maana ya kuchakata na kuongeza thamani pareto na wanapeleka hata Nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutalifanyia kazi na hasa niwahakikishie wakulima kama watalima pareto ya kutosha ili viwanda hivi viweze kupata malighafi ya kuchakata kwenye jimbo lake na maeneo mengine.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved