Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Omari Mohamed Kigua
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilindi
Primary Question
MHE. OMARI M. KIGUA aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga daraja linalounganisha Kijiji cha Negero – Kilindi?
Supplementary Question 1
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naishukuru Serikali kwa kutoa fedha kiasi hicho kwa ajili ya kuweka daraja la muda, lakini ni ukweli kwamba eneo hilo lina uzalishaji mkubwa sana wa mahindi. Kwa hiyo, kwa kipindi chote hicho cha miaka mitatu mpaka sasa hivi ni kwamba ni pikipiki tu na wananchi ndiyo wanapita kwa miguu lakini magari hayapiti. Kwa hiyo, kwa kiasi kikubwa imeathiri uchumi wa wananchi wa maeneo hayo. Je, Serikali iko tayari kuongeza speed tupate fedha daraja hilo liweze kujengwa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwenye Kata ya Pagwi, mkandarasi ambaye alipewa kazi hiyo kwenye Vijiji vya Lomotio na Makelele alipewa kazi ya kujenga vivuko, lakini mpaka sasa hivi amekimbia site na hajulikani alipo. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kumwelekeza Meneja wa TARURA Mkoa wa Tanga aweze kumrejesha mkandarasi huyo? (Makofi)
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Omari Kigua amekuwa akifanya ufuatiliaji wa karibu sana wa kuhakikisha kwamba miundombinu ya barabara katika jimbo lake inaendelea kuimarika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la kwanza, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuhakikisha inaendelea kuboresha miundombinu ya barabara hizi muhimu kabisa ambazo zinawawezesha wananchi kufanya shughuli zao za kiuchumi na kuweza kufikia maeneo yenye huduma za msingi kabisa za kijamii. Ndiyo maana utaona katika kipindi cha miaka minne, katika Wilaya ya Kilindi, shilingi bilioni 10.17 zimeletwa kwa ajili ya kuendelea kuimarisha miundombinu ya barabara hizi zinazosimamiwa na TARURA
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa bajeti 2025/2026 tunatarajia kwamba, Wilaya ya Kilindi itakuwa ina bajeti ya shilingi bilioni 3.9, kwa ajili ya kuendelea kuimarisha miundombinu ya barabara katika Eneo la Kilindi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutahakikisha daraja hili linapatiwa fedha na linajengwa haraka iwezekanavyo ili liweze kuwanufaisha wananchi wake, wasikwame kwenye shughuli zao za uzalishaji, kama alivyoainisha kwamba wanafanya uzalishaji mkubwa sana wa mahindi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali la pili, naomba nitumie nafasi hii, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, kumwagiza Meneja wa TARURA wa Mkoa aweze kuhakikisha anafuatilia kwa ukaribu sana, kuhakikisha mkandarasi huyu anafika site kwa ajili ya kuhakikisha kivuko alichokitaja Mheshimiwa Mbunge kinawanufaisha wananchi wake kiuchumi na kuwasaidia wananchi kufikia huduma za msingi kabisa za kijamii.
Name
Prof. Patrick Alois Ndakidemi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Vijijini
Primary Question
MHE. OMARI M. KIGUA aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga daraja linalounganisha Kijiji cha Negero – Kilindi?
Supplementary Question 2
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Daraja linalojulikana kama Mohameid Mwita linalounganisha Vijiji vya Boro na Kindi katika Jimbo la Moshi Vijijini limekatika kutokana na mafuriko. Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusu kulijenga na kuifungua barabara hii?
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Prof. Ndakidemi amekuwa akifanya ufuatiliaji wa karibu sana wa Daraja hili la Mohameid Mwita, ambalo ni daraja lenye umuhimu sana katika jimbo lake. Daraja hili ni la chuma, lakini lina nguzo za mawe, nguzo moja imeharibika na tayari ma-engineer wetu wamefika kwenda kufanya tathmini ya kujua gharama, kwa ajili ya kurudishia nguzo hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Profesa Ndakidemi kwamba mkandarasi atapatikana na atakuja kujenga nguzo hiyo, kurekebisha daraja kwa utaratibu wa dharura, ili liweze kuwasaidia wananchi wake kufanya shughuli zao mbalimbali za kiuchumi na kufikia huduma za kijamii. (Makofi)
Name
Justin Lazaro Nyamoga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilolo
Primary Question
MHE. OMARI M. KIGUA aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga daraja linalounganisha Kijiji cha Negero – Kilindi?
Supplementary Question 3
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kijiji cha Idunda kilichopo Kata ya Kimala na Kijiji cha Kiwalamo kilichopo Kata ya Idete, vijiji hivi viwili havina mawasiliano kutokana na madaraja mawili yanayozunguka vijiji hivyo kubomoka toka mwaka 2024. Serikali inatoa kauli gani kwa sababu, hakuna mawasiliano kwenye maeneo haya na wananchi wanashindwa kusafiri wala kusafirisha mizigo yao?
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee kumpongeza Mheshimiwa Mbunge, kwa kweli, mara nyingi amekuwa akifanya ufuatiliaji wa karibu sana kuhakikisha kwamba, wananchi wake wa Kilolo wanaweza kupatiwa miundombinu bora zaidi ya barabara hizi ambazo zinasimamiwa na TARURA.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika Bajeti hii ambayo tunaendelea nayo ya mwaka 2024/2025 zimetengwa shilingi bilioni 71 kwa ajili ya dharura ya kurudisha mawasiliano kwenye maeneo ambayo barabara zimekatika, ili wananchi waweze kupata barabara nzuri, kufanya shughuli zao za kiuchumi na pia kufikia huduma za kijamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikuhakikishie katika maeneo haya aliyoyataja tutafika na kuhakikisha kwamba, tunarejesha mawasiliano ili wananchi wake waweze kupata miundombinu bora kabisa, ambayo itawawezesha kufanya shughuli zao za kiuchumi na itawawezesha pia kufika katika huduma za msingi kabisa za kijamii. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Justin Nyamoga apate taarifa hiyo.
Name
Dr. Christine Gabriel Ishengoma
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. OMARI M. KIGUA aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga daraja linalounganisha Kijiji cha Negero – Kilindi?
Supplementary Question 4
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi niulize swali la nyongeza. Je, Serikali ni lini itakarabati Daraja linalounganisha Kata ya Mwaya na Kata ya Mbuga, Ilonga na Ketaketa katika Halmashauri ya Ulanga, ambalo lilibomoka kwa sababu ya mafuriko?
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mazingira ambayo kutokana na mvua nyingi zinazonyesha, na hasa Mkoa wa Morogoro ambao unaathirika sana na mvua hizi, kuna baadhi ya maeneo mawasiliano yanakatika. Ndiyo maana utaona dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuendelea kurudisha mawasiliano kwenye maeneo ambayo mawasiliano yamekatika, kwa maana ya miundombinu hii ya barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Christine Ishengoma kwamba, kupitia bajeti ya shilingi bilioni 71 ya dharura ya TARURA, Serikali itafika katika daraja alilolitaja katika maeneo hayo aliyoyataja, kwa ajili ya kuhakikisha inarudisha mawasiliano, ili wananchi waweze kupata barabara ambazo zitawawezesha kufanya shughuli zao za kiuchumi na zitawawezesha kufikia huduma za msingi za kijamii.