Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Rashid Abdallah Shangazi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlalo
Primary Question
MHE. RASHID A. SHANGAZI K.n.y. MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA aliuliza: - Je, lini Serikali itaanzisha Vijiji vipya kwenye maeneo ya Songea, Mkamani, Kwaluma Masimba na Sekioga – Korogwe Vijijini?
Supplementary Question 1
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa miongoni mwa vigezo ni kuandaa pamoja na maeneo ya kiutawala na vijiji hivi vya Songea, Mkamani, Kwaruma, Masimba na Sekioga vyote vina shule za msingi zaidi ya mbili na zahanati zaidi ya mbili. Kwa hiyo, kwa maana kwamba maeneo ya huduma yamekamilika. Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kutoa upendeleo maalum kwa maeneo hayo ili yaweze kupata huduma za kiutawala?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Katika Wilaya ya Lushoto Kata ya Manolo kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 ina idadi ya watu 25,000 na ndiyo iliyoongoza katika Wilaya nzima, lakini ina sekondari tatu, vijiji sita na shule za msingi tisa. Serikali haioni kwamba ni wakati mwafaka kugawa kata hii ili tuweze kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi kwa urahisi? (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Serikali inatambua kwamba kuna uhitaji wa kugawa baadhi ya vijiji ili kurahisisha huduma za kiutawala na huduma za kijamii lakini kwa vijiji hivi vya Songea, Mkamani, Kwaruma, Masimba na Sekioga katika Halmashauri ya Korogwe Vijijini, bado havijakidhi vigezo vya idadi ya watu kwa maana ya kwamba lazima kijiji ambacho kinazaliwa kiwe na idadi ya watu wasiopungua 5,000 na kile kijiji mama kiwe na watu wasiopungua 10,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sensa ya watu na makazi ya 2022 bado vijiji mama havijakidhi idadi ya watu 15,000 ili kuwezesha vijiji vingine hivi kuweza kugawika. Kwa hiyo, naomba nitumie nafasi hii nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Vijijini kwamba Serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu idadi ya watu na vigezo vingine ili ikiwezekana muda ukifika viweze kupata hadhi ya vijiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, kuhusiana na Kata ya Manolo katika Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, tunafahamu kwamba ni kata kubwa ina watu wapatao 25,000 kwa taarifa za sensa na makazi 2022; na vijiji sita na shule za sekondari tatu, lakini bado haijafikisha idadi ya watu angalau 30,000 ili tukigawa kata ile, kata mama ipate angalau watu 20,000 na kata mpya ipate watu angalau 10,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Shangazi kwamba tunatambua umuhimu wa kugawa kata hiyo, lakini namwomba tuendelee kufuatilia vigezo hivyo vya idadi ya watu na baadaye Serikali itaona utaratibu mzuri wa kugawa kata hiyo.
Name
Mwita Mwikwabe Waitara
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Primary Question
MHE. RASHID A. SHANGAZI K.n.y. MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA aliuliza: - Je, lini Serikali itaanzisha Vijiji vipya kwenye maeneo ya Songea, Mkamani, Kwaluma Masimba na Sekioga – Korogwe Vijijini?
Supplementary Question 2
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, eneo la Sirari na Nyamongo, wana sekondari za kutosha, shule za msingi, Mahakama, idadi ya watu, eneo la kiutawala, vigezo vyote vilikamilika maeneo yote mawili, lakini majibu yaliyopita alisema kwamba hawajaanzisha...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waitara, uliza swali.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo swali, kwamba maeneo mapya yatasubiri maeneo mengine ya mwanzo...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waitara, uliza swali. Swali la nyongeza lina utaratibu wake.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa majibu haya, Naibu Waziri yupo tayari akanisaidie kutoa maelezo Sirari na Nyamongo ili kuondoa mkanganyiko? Kwa sababu waliwaambia wasubiri maeneo mengine yaimarike ndiyo yaanzishwe mapya, leo anasema vigezo na idadi ya watu. (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Mwita Waitara, nafikiri hakunielewa wakati najibu swali la msingi. Taarifa na kauli ya Serikali ni moja, haijawahi kubadilika kwamba tunafahamu kuna uhitaji wa kugawa maeneo ya kiutawala, lakini tumeweka kipaumbele namba moja katika kuboresha kwanza miundombinu katika maeneo ya utawala yaliyopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu tunazo kata ambazo hazina Ofisi za Watendaji wa Kata, tunavyo vijiji ambavyo havina Ofisi za Serikali za Vijiji, hakuna Ofisi za Watendaji, tunazo halmashauri hazina majengo ya halmashauri, Ofisi za Wakuu wa Wilaya na Mikoa vivyo hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kipaumbele namba moja ni kuhakikisha kwanza miundombinu muhimu ya kutoa huduma kwenye mamlaka zilizopo inaboreshwa, lakini tunafahamu yapo maeneo kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge, Sirari, Nyamongo ambayo tayari yamekidhi vigezo, na ni kipaumbele tunasubiri sasa tukikamilisha kipaumbele cha kwanza tutakwenda kuona namna ambavyo tunaanza kuchukua hatua kwa ajili ya kupandisha hadhi maeneo hayo.
Name
Abdallah Jafari Chaurembo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbagala
Primary Question
MHE. RASHID A. SHANGAZI K.n.y. MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA aliuliza: - Je, lini Serikali itaanzisha Vijiji vipya kwenye maeneo ya Songea, Mkamani, Kwaluma Masimba na Sekioga – Korogwe Vijijini?
Supplementary Question 3
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Chamazi ina wakazi wapatao 226,000. Je, Serikali ina mpango gani wa kukata kata hiyo huku ikiwa imetimiza vigezo vyote vya shule, hospitali, ofisi za mitaa na ofisi za kata? (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Kata ya Chamazi imekidhi vigezo vyote kwa idadi ya watu pamoja na miundombinu na huduma mbalimbali. Pia, ni moja ya kata ambazo tayari Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumeiainisha kwenye kata za kipaumbele ambazo mara baada ya kukamilisha kipaumbele namba moja cha kuboresha miundombinu, tutahakikisha Kata ya Chamazi inagawika na kupata kata nyingine ili kusogeza zaidi huduma kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Chaurembo na wananchi wa Kata ya Chamazi waendelee kuwa wavumilivu, Serikali hii sikivu tayari imeshalichukua jambo hilo, inaendelea kulifanyia kazi.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved