Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Mohammed Said Issa
Sex
Male
Party
ACT
Constituent
Konde
Primary Question
MHE. MOHAMED SAID ISSA aliuliza: - Je, changamoto zipi zinazorotesha ukusanyaji wa mapato katika mfumo mpya wa kuchakata Kodi ya Forodha ambao ni "single window"?
Supplementary Question 1
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, ninaipongeza Serikali kupitia TRA kwa kupunguza changamoto nyingi za mfumo huu. Wakati ninauliza swali hili kulikuwa na changamoto nyingi ambazo zilikuwa zinawafanya watu kuchukua hadi wiki tatu kutoa mizigo bandarini, sasa hivi imeboreshwa. Sasa nina maswali yangu mawili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, mifumo hii imekuwa ikibadilika mara kwa mara. Tulianza na mfumo ambao siyo rasmi ambao ulikuwa ni kujaza data tu kwenye mfumo, lakini tukaja na mfumo wa pili uliokuwa unaitwa ASYCUDA ukabadilishwa tukaja na mfumo wa tatu ambao ulikuwa unaitwa TANCIS ambao ndiyo uko sasa, nao unabadilika maana yake baadaye uliitwa TASUS ambao ni huu Mheshimiwa Waziri amesema unakuwa ukiboreshwa na sasa hivi unaitwa TANESW. Maana yake, kila siku mifumo hii inabadilika.
Mheshimiwa Spika, sasa wakati wa kubadilika inakuwa inaleta changamoto katika utoaji wa mazigo bandarini. Je, ni kwa sababu gani inakuwa inabadilika mara kwa mara? Je, wataalamu wetu hawafanyi utafiti wa kutosha katika kuhakikisha tunakuwa na mifumo bora na imara?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwamba kwa upande wa Zanzibar imekuwa tunapofanya document kwa ajili ya kutoa mizigo ya forodha tunakuwa na changamoto kwamba bila kujaza mkoa ambao unatoka Tanzania Bara huwezi kuendelea na procedure. Maana yake huwezi kusema nipo Malindi, huwezi kusema niko Darajani, huwezi kusema niko Zanzibar; unapaswa useme niko Kariakoo, niko Arusha, niko wapi; je, ni kwa nini, Zanzibar haitambuliki katika mfumo huo? Ahsante.
Name
Hamad Hassan Chande
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kojani
Answer
NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, kwanza tunapokea pongezi zake kwa Serikali. Ni ukweli alichokisema kwamba changamoto zilikuwa nyingi, lakini baada ya mfumo huu, changamoto karibu 95% zimeondoka.
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali kupitia TRA inafanya tafiti za kila siku za mara kwa mara na kufuatilia mwenendo wa mfumo huu. Kwa hiyo, hapa Serikali iko makini sana, na nikutoe hofu kabisa kwamba hayo yaliyotokea nyuma hayatatokea tena kwa tafiti ambazo tuko nazo. Pia, Serikali imeunda timu maalumu, tuna tume maalumu ambayo inafuatilia masuala ya mfumo na iko vizuri kabisa.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili ambalo amelisema, tayari tumeanza kufuatilia changamoto hii, na nitoe maelekezo kwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania afuatilie kwa karibu sana. Kama bado inajitokeza changamoto hii, basi twende kuifanyia kazi na kuitatua kwa haraka ili kuondoa usumbufu kwa wafanyabiashara wa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved