Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Shally Josepha Raymond
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. SHALLY J. RAYMOND K.n.y. MHE. TOUFIQ SALIM TURKY aliuliza: - Je, Serikali imejipangaje kutatua changamoto ya ucheleweshwaji wa kupandisha hadhi vituo vya afya na zahanati zinazookoa maisha ya wananchi nchini?
Supplementary Question 1
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; ili kituo cha afya au zahanati ikidhi kigezo cha kupandishwa hadhi ni pamoja na zahanati hiyo kuwa na miundombinu yote ya kupandishwa.
Mheshimiwa Spika, ninaishukuru sana Serikali kwa jinsi ambayo imetoa mwongozo. Je, ni lini Zahanati ya Rononi iliyopo Uru Kaskazini itamalizika kwa kupata vyoo na samani ili iweze kuwa katika hali ya kuwa zahanati kwa hakika?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, pamoja na zahanati hiyo kuna zahanati nyingine ya Fumbuni ambayo kwa kweli tangu imejengwa miundombinu yote imechakaa na haiwezi tena kuwa katika hali nzuri. Je, Mheshimiwa Waziri anaweza kufuatana na mimi tukimaliza Bunge hili ili akatutatulie matatizo hayo katika eneo letu?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza, ninaomba nimhakikishie mama yangu Mheshimiwa Shally Raymond kwamba, Serikali inatambua kwamba zahanati hiyo ambayo ipo Uru Kaskazini ya Runoni haijakamilika na inahitaji kukamilisha miundombinu na vifaatiba.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie kwamba, kupitia halmashauri pamoja na fedha ya Serikali Kuu, tutaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba zahanati hiyo inakamilika mapema na inaanza kutoa huduma zote muhimu kwa ngazi ya zahanati.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, hoja hiyo tumeichukua na mara baada ya kutoka hapa nitawasiliana na Mkoa wa Kilimanjaro ili tuweze kuweka utaratibu na kujua gharama inayohitajika kwa ajili ya ukamilishaji wa zahanati hiyo.
Mheshimiwa Spika, kwa swali la pili, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, zipo zahanati ambazo ni kweli ni chakavu, kongwe na za siku nyingi. Tumeainisha zahanati zote chakavu na vituo vya afya vyote chakavu. Tunakamilisha ukarabati wa Hospitali za Halmashauri 50 kongwe na chakavu; na mara baada ya ukamilishaji huo, tutaanza ukarabati wa vituo vya afya na zahanati zote kongwe, na zahanati hiyo tutaipatia kipaumbele.
Name
Priscus Jacob Tarimo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Mjini
Primary Question
MHE. SHALLY J. RAYMOND K.n.y. MHE. TOUFIQ SALIM TURKY aliuliza: - Je, Serikali imejipangaje kutatua changamoto ya ucheleweshwaji wa kupandisha hadhi vituo vya afya na zahanati zinazookoa maisha ya wananchi nchini?
Supplementary Question 2
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, ninashukuru sana. Ninaomba kumwuliza Mheshimiwa Waziri, zahanati ya Kiboriloni ndiyo tuliyoichagua kama Kituo cha Afya cha Kimkakati. Je, ni lini fedha zitakwenda kwa ajili ajili ya Kituo hicho cha Afya cha Kiboriloni?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ni kweli Mheshimiwa Mbunge alishawasilisha Kata ya Kiboriloni katika Zahanati ya Kiboriloni kuwa ni kata ya kimkakati kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya. Tayari Mheshimiwa Rais ameshatenga fedha ya dharura shilingi bilioni 53,500. Tayari shilingi bilioni 30 zimeshatolewa kwa ajili ya majimbo 120 ya awali na zipo katika halmashauri zetu.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutahakikisha pia tunapeleka fedha hizo kwa ajili ya kwenda kujenga Kituo cha Afya Kiboriloni ili tusogeze huduma za ngazi ya kituo cha afya kwa wananchi.
Name
Dr. Charles Stephen Kimei
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vunjo
Primary Question
MHE. SHALLY J. RAYMOND K.n.y. MHE. TOUFIQ SALIM TURKY aliuliza: - Je, Serikali imejipangaje kutatua changamoto ya ucheleweshwaji wa kupandisha hadhi vituo vya afya na zahanati zinazookoa maisha ya wananchi nchini?
Supplementary Question 3
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ardhi katika Jimbo la Vunjo ni ghali sana na ni adimu sana. Je, ni lini Serikali itatoa mwongozo wa kuruhusu kujenga vituo vya afya kwa mfumo wa ghorofa kwenye maeneo ambayo ardhi ni adimu?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kwamba yapo baadhi ya maeneo hususan ya miji na majiji ambayo ardhi ni finyu, pia ni ya ghali zaidi. Tayari ilishatoa mwongozo na michoro kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya kwa utaratibu wa maghorofa; na tayari imeshajengwa katika maeneo mbalimbali. Ukienda Dar es Salaam, Mbeya na maeneo mengine ya Arusha na kadhalika, tunajenga vituo vya afya, hospitali na mara nyingine hata zahanati katika mfumo wa maghorofa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Dkt. Charles Kimei, kwamba tupate tu maombi kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Moshi, kwamba eneo hilo linahitaji kujengwa kituo cha afya kwa mfumo wa ghorofa ili tuweze kuipitia michoro, kukubaliana na tuanze kujenga fedha kwa awamu kwa ajili ya kuhakikisha kwamba kituo hicho cha afya kinajengwa.
Name
Saashisha Elinikyo Mafuwe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hai
Primary Question
MHE. SHALLY J. RAYMOND K.n.y. MHE. TOUFIQ SALIM TURKY aliuliza: - Je, Serikali imejipangaje kutatua changamoto ya ucheleweshwaji wa kupandisha hadhi vituo vya afya na zahanati zinazookoa maisha ya wananchi nchini?
Supplementary Question 4
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, Zahanati ya Shirimgungani, Kata ya Mnadani tuliomba kupandishwa hadhi kuwa kituo cha afya. Je, Serikali ina mpango gani wa kuipandisha hadhi ikizingatia Kata ya Mgungani haina kituo cha afya?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka utaratibu kwa halmashauri husika kutuma maombi ya kupandisha hadhi zahanati kuwa kituo cha afya. Utaratibu huo sasa umeboreshwa zaidi tofauti na siku za nyuma ambazo walikuwa wanalazima kuandika barua kuja kwa Katibu Mkuu, TAMISEMI kwa ajili ya maombi hayo, ambapo ilikuwa inachukua muda mrefu hadi siku 60.
Mheshimiwa Spika, sasa tuna mfumo ambao ni wa kidigitali (Health Facilities Registration System) ambayo inawezesha Halmashauri kutuma maombi yao online. Timu ya ukaguzi kutoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kushirikiana na mkoa kufanya ukaguzi wa majengo katika zahanati ile, eneo na idadi ya wananchi ambao wanatarajiwa kuhudumiwa ili kama inakidhi vigezo tuweze kuipandisha hadhi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninaomba kumwambia Mheshimiwa Saashisha, kwamba jambo hili tumelichukua Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tutafuatilia na tuone kama inakidhi vigezo ili tuweze kuanza utaratibu wa kuipandisha hadhi.