Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Hussein Nassor Amar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyang'hwale

Primary Question

MHE. HUSSEIN M. AMAR aliuliza: - Je, lini Mshauri Elekezi atatangazwa kuanza kazi ya Upembuzi Yakinifu barabara ya Kahama – Kharumwa – Nyang’hwale hadi Busisi ambayo ni ahadi ya muda mrefu?

Supplementary Question 1

MHE. HUSSEIN M. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niipongeze Serikali kwa kupokea ombi langu la kumtafuta mpembuzi yakinifu na kuianza kazi hiyo. Swali langu la kwanza, je, kazi hiyo itaanza lini na kukamilika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa kuwa tunakwenda kulifungua Daraja la Kitaifa na Kimataifa Busisi - Kigongo Feri kwa kutokea Mwanza kwenda Shinyanga mpaka Kahama na kutokea Kahama kwenda Mwanza kwa kupitia Nyang’hwale, tofauti yake ni kilomita 90; tunatarajia baada ya kufunguliwa daraja hilo kutakuwa na magari mengi sana ambayo yatapita Daraja la Kigongo kwenda Kahama kwa kupitia Nyang’hwale; Je, Serikali iko tayari kuongeza fedha za matengenezo ya mara kwa mara kwenye barabara hiyo?

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Nassor, Mbunge wa Nyang’hwale, kwa kufuatilia hii kazi na mara kadhaa ameulizia, lakini tumefika tamati. Ni suala la muda tu lini tuisaini hiyo barabara ili iweze kuanza kufanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu na ni kuanzia Mkoa wa Geita - Nyang’hwale, Nyang’hwale - Busisi na Nyang’hwale kwenda Kahama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili, ninataka nitumie nafasi hii kwamba ni kweli Daraja la Kigongo Busisi maarufu kama Daraja la John Pombe Magufuli (JPM) litafunguliwa rasmi tarehe 19. Tunategemea Mheshimiwa Rais mwenyewe atakuwepo kufungua mradi huu wa kielelezo. Nitumie nafasi hii kuwaalika wananchi wote wa Tanzania pamoja na Wabunge kwenda kushuhudia tukio hilo la kihistoria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sambamba na hilo tunatambua kwamba ni kweli kutoka Kahama kwenda Mwanza itakuwa ni karibu sana kupitia hiyo njia. Nimhakikishie Mheshimiwa Nassor, Mbunge wa Nyang’hwale, kwamba kama Wizara na TANROADS tushawaelekeza kwamba wahakikishe kwanza wanaimarisha hiyo barabara kwa sababu tunajua itakuwa na magari makubwa yatakayobeba mizigo baadaye. Pengine yatapungua sana kwenda Kahama ili wakati tunafanya usanifu lakini tuwe na uwezo pia wa kupitisha magari makubwa katika hiyo njia. Ahsante. (Makofi)

Name

Felista Deogratius Njau

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. HUSSEIN M. AMAR aliuliza: - Je, lini Mshauri Elekezi atatangazwa kuanza kazi ya Upembuzi Yakinifu barabara ya Kahama – Kharumwa – Nyang’hwale hadi Busisi ambayo ni ahadi ya muda mrefu?

Supplementary Question 2

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Je, ni lini Serikali itamlipa mkandarasi anayejenga Barabara ya Kibosho Shine, Kwa Rafael mpaka International School ambapo ameondoka site baada ya kudai pesa shilingi 1,700,000,000 kwa muda mrefu na hivyo barabara ile ime-stack na wananchi wanapata adha kubwa? (Makofi)

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali ilimweka huyo mkandarasi na tunavyoongea tumeshapokea hati zake za malipo na tumeshawasilisha kwa wenzetu wa Wizara ya Fedha na wametuambia kipindi hiki cha mwezi huu Juni, certificate nyingi (hati za malipo) zitalipwa ikiwa ni pamoja na ya mkandarasi huyu wa Kibosho Shine ili aweze kurudi na kukamilisha kazi ambayo alishaianza.