Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Festo Richard Sanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makete
Primary Question
MHE FESTO R. SANGA K.n.y. MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka huduma ya bure ya mtandao kwenye vyuo na shule zote nchini?
Supplementary Question 1
MHE FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naipongeza Serikali kwa jitihada hizi kubwa ambazo inazifanya za kuhakikisha kwamba inasogeza huduma ya internet kwenye maeneo yetu ya vyuo na kwa wanafunzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Kuchauka ana swali lake la kwanza, anasema; kwenye Jimbo la Liwale shule nyingi hazina access ya internet na maeneo mengi hayana kwa sababu mitandao mingi iliyofungwa pale inatumia solar. Kwa hiyo, nyakati za usiku na nyakati za jioni ambapo umeme umepungua kunakuwa na kukosekana kwa mawasiliano. Je, ni lini Serikali itahakikisha imefikisha umeme kwenye maeneo hayo ili internet iweze kupatikana kwa wakati?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili ni kwa ajili ya wananchi wa Jimbo la Makete ambalo mimi ndio Mbunge wao. Tunaomba kuuliza, ni lini minara ambayo haijakamilika ya UCSAF ambayo tulipatiwa kwa mfano Usalimu One na kule Ruhumbu, ni lini minara hii itakuwa imekamilika kujengwa ili wananchi wa maeneo haya waweze kupata internet ya kutosheleza na waweze kufurahia maisha ya Taifa lao?
Name
Maryprisca Winfred Mahundi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Festo Sanga kwa uwajibikaji wake na namna ambavyo ameweza kumwakilisha Mheshimiwa Kuchauka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Liwale mitandao mingi inatumia power ya solar na wakati mwingine, hasa wa jioni wanapotea, lakini tumshukuru sana Mheshimiwa Rais tayari REA ina inaendelea kusogeza huduma ya umeme maeneo hayo yote ambayo umeme wa uhakika wa Grid ya Taifa haujawafikia. Kwa hiyo, niwaondoe hofu, muda siyo mrefu ninaamini na wao watapelekewa umeme wa REA katika maeneo yote haya pamoja na makazi ya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake kwamba ni lini minara itakamilika katika jimbo lake Mheshimiwa Festo Sanga; kazi zinaendelea. Kadiri tunavyopata fedha tutaendelea kuhakikisha kwamba minara hii ambayo tuliiweka katika maeneo ambayo walikubaliana inatakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile hata kwenye maeneo mengine ambayo hayajapatiwa bado uelekezi wa ujenzi wa minara, nimtoe hofu, kote tutafikia. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba maeneo yote yanapatiwa huduma ya mawasiliano ya uhakika.
Name
Tarimba Gulam Abbas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kinondoni
Primary Question
MHE FESTO R. SANGA K.n.y. MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka huduma ya bure ya mtandao kwenye vyuo na shule zote nchini?
Supplementary Question 2
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi. Naomba nimwulize Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba suala la mitandao kwa maana ya internet ya bure katika vyuo vyetu ni jambo muhimu sana. Hivi haoni kwamba ni muhimu sana kwa Serikali kuja na program and plan of actions (mpango kazi) kuonyesha mkoa gani utaweza kufanyiwa lini, ili watu wakajitayarisha na kuweza kupata manufaa ya kupata internet ya bure katika vyuo vyetu?
Name
Maryprisca Winfred Mahundi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa swali kutoka kwa Mheshimiwa Abbas Tarimba. Mpango kazi upo. Ukinisikiliza katika jibu langu la msingi nimesema nje na haya ambayo yameshafanyiwa, lakini tuna maeneo mengine 17 ambayo UCSAF imesha-spot kwenda kufanya. Kwa hiyo kuonyesha lini, wapi kitafanyika, niwe nimepokea. Waheshimiwa Wabunge, wataletewa mpango kazi huo ili kila mmoja aweze kufahamu.
Name
Katani Ahmadi Katani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tandahimba
Primary Question
MHE FESTO R. SANGA K.n.y. MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka huduma ya bure ya mtandao kwenye vyuo na shule zote nchini?
Supplementary Question 3
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini minara ya Kata ya Litehu, Ngunja na Michenjele itajengwa, kwa sababu mwanzo Waziri aliyekuwa mwenye dhamana aliahidi kupeleka minara maeneo haya?
Name
Maryprisca Winfred Mahundi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Katani, lini minara itajengwa? Ahadi ya Serikali ni lazima itekelezwe. Kama Mheshimiwa aliyepita aliagiza, maana yake wataalam wana taarifa hizi. Nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge mwaka ujao wa fedha tutahakikisha kwamba tunaanza ujenzi katika maeneo hayo aliyoyataja.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved