Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Abeid Ighondo Ramadhani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ilongero
Primary Question
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani wa kutoa elimu ya Mfumo wa Stakabadhi Ghalani kwa Wakulima ili kuondoa changamoto zilizopo - Singida Kaskazini?
Supplementary Question 1
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa niulize maswali mawili ya nyongeza, pamoja na hayo majibu ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza. Pamoja na juhudi hizo ambazo zimefanywa na Serikali, lakini kuna AMCOS ambazo hazikulipwa kwa hiyo, kumekuwa na kucheleweshwa kwa malipo ambayo kwa msimu uliopita wa 2024, mpaka sasa bado wananchi wanadai, ikiwemo AMCOS ya Ngamu pamoja na ya Ngimu. Sasa ni utaratibu upi uliopo kwa ajili ya kuhakikisha suala hili la kuchelewesha malipo linaondolewa, lakini pia, na hawa ambao hawajalipwa walipwe?
Mheshimiwa mwenyekiti, swali la pili. Kuna maghala mengi hayajasajiliwa, suala ambalo linawapa usumbufu mkubwa sana wananchi. Ni ghala moja tu la Mtingo limesajiliwa, lakini Maghala ya Mdeda, Makulo, Kinyeto, Ngimu, Mwasauya hayajasajiliwa, kwa hiyo, wananchi wanapata shida kuweza kwenda kupeleka mazao yao.
Mheshimiwa mwenyekiti, sasa ni utaratibu upi unafanyika kwa haraka kuweza kuyasajili maghala haya tunapoelekea kwenye msimu wa mwaka huu wa mauzo ya biashara, ikiwa ni pamoja na kuweka uwazi kwenye minada, kwa sababu, minada ile inafanywa kwenye mtandao na wananchi wengi wanatumia viswaswadu, ambavyo haviwezi kupata access to information? Ahsante.
Name
Dr. Selemani Said Jafo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisarawe
Answer
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba kumpongeza ndugu yangu, Mheshimiwa Abeid, Mbunge, kwa kazi kubwa anayoifanya. Kwanza naomba niweke rekodi vizuri. Katika kipindi kilichopita waliuza tani 16,900 ambapo hii ilikuwa ni dengu peke yake. Zaidi ya shilingi bilioni 30.5 zilienda kwa wananchi, kwa hiyo, hii ni faraja kubwa sana. Hivi karibuni, mpaka juzi, suala zima la ufuta tayari wameshakusanya karibu tani 1,800 ambazo zina gharama ya shilingi bilioni 4.4. Hizi zote ni fedha kwa upande wa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika upande huu sasa AMCOS ambazo wananchi bado hawajalipwa, ngoja tulifanyie kazi kwa sababu, katika rekodi zetu tulikuwa tunafanya compliance maeneo yote na ilionekana katika kipindi kilichopita, maeneo ya Kyela ndiyo yalikuwa na changamoto kidogo, hata hivyo, yalifanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hili suala la Singida ngoja tulifanyie kazi tuone wapi changamoto ilijitokeza. Lengo ni kuhakikisha watu wanapata haki yao ya msingi. Naomba nimwagize Mtendaji Mkuu wa Maghala, Asengi Bangwa, afuatilie haraka na anipe mrejesho ili wananchi waweze kupata fursa yao ya kimaendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini upande wa maghala ambayo hayajasajiliwa, Taasisi yetu ya Bodi ya Stakabadhi Ghalani inafanya hii kazi na sasa hivi tumesajili maghala mengi. Maghala ambayo tumeyasajili mengine sasa hivi tumeyawekea CCTV Camera kwa lengo la ku-track information zote katika real time data.
Mheshimiwa mwenyekiti, kwa upande wa Singida, namwagiza tena Mkurugenzi, Bwana Bangwa, afuatilie kwa haraka kuhakikisha maghala yote ambayo hayajasajiliwa yanaingizwa katika mfumo. Lengo letu kubwa ni wananchi waweze kuuza mazao yao kupitia mfumo huo ambao una faida kubwa sana katika nchi yetu, ahsante.
Name
Yustina Arcadius Rahhi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani wa kutoa elimu ya Mfumo wa Stakabadhi Ghalani kwa Wakulima ili kuondoa changamoto zilizopo - Singida Kaskazini?
Supplementary Question 2
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza. Je, Serikali ina mpango gani wa kutumia maghala yanayomilikiwa na watu binafsi kununua mazao ya wakulima, hasa kwa maeneo ambayo haina maghala, ili kuongeza ushindani kwa wakulima?
Name
Dr. Selemani Said Jafo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisarawe
Answer
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu hili swali la Mheshimiwa Mbunge, ambaye ni mtaalamu mzuri sana wa kilimo, kutoka pale SUA. Suala la usajili wa maghala binafsi tumeshalifanyia kazi, hata na Kamati ya Bunge, ninakumbuka tulivyoenda Shinyanga pale kwa sababu, siyo maghala yote, ni ya Serikali, sasa hivi mengi yametengezwa na private sectors.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba watu binafsi, kwanza waendeleze juhudi hii ya utengenezaji wa maghala kwa sababu ni biashara, lakini hata hivyo, Serikali imefungua milango maghala haya yasajiliwe kwa lengo la kuhakikisha kwamba, bidhaa hizo zinaingizwa katika maghala haya na biashara ifanyike. Kwa hiyo, nakuhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, hili linafanyika hivi sasa na maghala haya mengi kutoka katika sekta binafsi yanasajiliwa, ahsante sana.
Name
Daimu Iddi Mpakate
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduru Kusini
Primary Question
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani wa kutoa elimu ya Mfumo wa Stakabadhi Ghalani kwa Wakulima ili kuondoa changamoto zilizopo - Singida Kaskazini?
Supplementary Question 3
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya changamoto ya Mfumo wa Stakabadhi Ghalani ni suala la account za wakulima kulala ndani ya miezi sita bila ku-operate. Je, kwa mazingira ya wakulima, Serikali haioni umuhimu wa kuondoa sheria hii kuifanya account ya mkulima iweze ku-operate bila kulala?
Name
Dr. Selemani Said Jafo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisarawe
Answer
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaomba nimpongeze Mheshimiwa Mpakate. Miongoni mwa mikoa ambayo inafanya vizuri ni Mkoa wa Ruvuma ambao uko katika jimbo la ndugu yangu Mheshimiwa Mpakate. Kwenye hili Serikali ni lazima tu-appreciate kazi kubwa na inayoendelea vizuri. Niwaombe wananchi wa kule wamwone vizuri ndugu yangu Mheshimiwa Mpakate kwa kazi hii kubwa anayoendelea kuifanya, na hasa kipindi hiki cha lala salama kuamkia gazetini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili la account tunalifanyia kazi. Lengo letu ni kwamba tuone kama kuna changamoto yoyote ya kifedha. Lengo letu ni kuhakikisha kwamba kila mwananchi account yake inafanya kazi. Hili Mheshimiwa Mpakate tuonane baadaye ili tuelezane vizuri changamoto iko wapi, tuboreshe vizuri ili wananchi wetu wapate fursa ya kufanya biashara yao katika mazingira mazuri, ahsante sana.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved