Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Oran Manase Njeza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbeya Vijijini

Primary Question

MHE. ORAN M. NJEZA K.n.y. MHE. SUMA I. FYANDOMO aliuliza: - Je, lini Serikali itawapa makoti ya kujikinga na baridi Askari Polisi wanaofanya kazi katika Mkoa wa Mbeya?

Supplementary Question 1

MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naanza kwa kutoa pole kwa wafiwa pamoja na majeruhi waliotokana na ajali mbaya iliyotokea Mlima Iwambi, Mbalizi, Mbeya. Ninamwomba Mwenyezi Mungu awasaidie majeruhi wote waweze kupona kwa haraka na Marehemu wote azilaze roho zao mahali pema Peponi, Amen.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, Askari hawa mara nyingi wako kwenye doria na wengine wako kwenye sehemu za ukaguzi wa magari, je, ni lini Serikali itajenga vibanda vya ukaguzi katika maeneo hayo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Mbalizi, wananchi pamoja na Serikali wamejenga Kituo cha Polisi cha Wilaya. Je, ni lini sasa Serikali itajenga nyumba za Askari wa Kituo hiki cha Wilaya ya Mbalizi? Ahsante.

Name

Daniel Baran Sillo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Babati Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Askari wetu wanafanya kazi nzuri sana, kwa maana ya doria pamoja na ukaguzi na yapo baadhi ya maeneo tayari tumeshajenga mabanda hayo, kwa ajili ya Askari wetu. Ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge, maeneo aliyoyataja pia tutayaweka kwenye mpango kwa ajili ya kujenga mabanda hayo, ili Askari wetu wanaofanya doria na ukaguzi, wapate maeneo ya kujisitiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu swali la pili, kwanza, nampongeza Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Mbalizi kwa kazi kubwa waliyoifanya ya ujenzi wa Kituo cha Polisi. Ninakumbuka pia, Serikali iliunga mkono juhudi za wananchi hao kwa kutoa shilingi milioni 100 ambayo tayari ilishafika ya ujenzi wa Kituo cha Polisi. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali itaweka kwenye mpango sasa ujenzi wa nyumba za Askari wetu kwa ajili ya eneo la Mbalizi ambao wanafanya kazi nzuri, ahsante.

Name

Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ORAN M. NJEZA K.n.y. MHE. SUMA I. FYANDOMO aliuliza: - Je, lini Serikali itawapa makoti ya kujikinga na baridi Askari Polisi wanaofanya kazi katika Mkoa wa Mbeya?

Supplementary Question 2

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Polisi Kata ni kati ya Askari ambao wanasaidia sana ulinzi wa raia na mali zao katika kata zetu, hasa zile ambazo ziko maeneo ya vijijini, lakini wamekuwa wakifanya kazi kwa mazingira magumu sana; hawana usafiri, wanawajibika kutumia fedha zao kuzunguka katika kuhakikisha kwamba, wanaimarisha ulinzi na usalama, zaidi wanawajibika kushiriki kwenye shughuli za kijamii kwa kutumia fedha zao za mfukoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali haioni kwamba, kuna umuhimu sasa wa kuwatengea walau package allowance kidogo ya kuwawezesha kuzunguka kwenye shughuli za kijamii, ikiwemo kupeleka pikipiki kwa hao Polisi Kata kote nchini?

Name

Daniel Baran Sillo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Babati Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, Askari Kata wanafanya kazi nzuri sana kwa ushirikiano na jamii. Serikali kwa kutambua kazi kubwa wanayofanya tayari imeshasambaza pikipiki 105 kwa Askari Kata hapa nchini na bado mpango unaendelea kuhakikisha kwamba, kwanza tunajenga Ofisi za Polisi Kata kwenye kata zote pamoja na shehia kwa upande wa Zanzibar, lakini pia, tunawapatia vitendea kazi, kama pikipiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimesema, tayari tumeshatoa pikipiki 105. Kwenye bajeti hii tumetenga fedha, kwa ajili ya kuhakikisha tunawapatia pikipiki ili kurahisisha utendaji kazi wa hao Askari Kata. Ahsante sana.