Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Selemani Jumanne Zedi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukene
Primary Question
MHE. SELEMANI J. ZEDI aliuliza: - Je, lini Serikali itamaliza tatizo la upungufu wa Watumishi wa Kada ya Afya – Bukene?
Supplementary Question 1
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa Serikali kutupatia watumishi wa kada ya afya 59 kwenye Jimbo la Bukene, lakini nina swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zahanati mpya tulizojenga na ambazo zimeanza kutoa huduma za vijiji vya Gulyambi, Buhulyu, Mogwa, Iboja, Ilagaja, Kasanga na Mboga, zote hizi zina mtumishi mmoja mmoja tu. Nyingine zina Mganga peke yake, hazina nurse, nyingine zina nurse peke yake hazina Mganga, kiasi ambacho huyu mtumishi mmoja akipata dharura tu zahanati inafungwa, kunakuwa hakuna huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba kila zahanati mpya hasa hizi zinazoanza iwe angalau na watumishi wasiopungua wawili, mganga na nurse ili angalau hata mmoja akipata dharura kituo kisifungwe kabisa? Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha hiyo minimum ya watumishi inakuwepo kwenye kila kituo?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea na kutekeleza kipaumbele chake na sera yake ya kusogeza huduma ya afya karibu zaidi na wananchi kwa kujenga zahanati ili kupunguza umbali wa wananchi kupata huduma za afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha miaka hii minne ya Serikali ya Awamu ya Sita jumla ya zahanazti zaidi ya 1,300 mpya zimejengwa zikiwemo zahanati ambazo zipo katika Jimbo la Bukene. Maana yake ni kwamba, tumeendelea kuongeza sana idadi ya vituo vya afya na automatically idadi ya watumishi wanaohitajika pia imeendelea kuongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Bukene, Mheshimiwa Selemani Zedi kwamba tunafahamu katika zahanati hizo kuna upungufu wa watumishi, lakini kwa sababu zahanati hizo ni mpya, tumeendelea kuajiri watumishi na kuwapeleka kwa ajili ya kuziba pengo la watumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumkumbusha Mkurugenzi wa Halmashauri na Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora kwamba, katika maeneo yote ambayo yana watumishi mmoja katika zahanati, wafanye msawazo wa ndani wa watumishi, iwe kutoka Halmashauri nyingine yenye nafuu kupeleka hapo pia ndani ya Halmashauri yenyewe kutoka kwenye vituo vingine vyenye watumishi wengi ili angalau huduma muhimu ziendelee kutolewa wakati Serikali inaendelea kutoa vibali vya ajira ili kwenda kuziba mapengo hayo.(Makofi)
Name
Saashisha Elinikyo Mafuwe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hai
Primary Question
MHE. SELEMANI J. ZEDI aliuliza: - Je, lini Serikali itamaliza tatizo la upungufu wa Watumishi wa Kada ya Afya – Bukene?
Supplementary Question 2
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru Serikali imetujengea vituo vipya vya kutoa huduma za afya (zahanati na vituo vya afya) pamoja na ukarabati wa hospitali ya wilaya, lakini tuna changamoto kubwa ya watumishi kwenye eneo hili la afya. Je, Serikali ina mpango gani wa kutuletea watumishi wa afya kwenye maeneo haya?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kwamba katika kipindi hiki cha miaka minne wataalamu wa Sekta ya Afya walioajiriwa ni wengi sana (wataalmu 34,720) lakini wataalamu hawa bado hawatoshi kwa sababu pia kasi ya ujenzi wa vituo imekuwa kubwa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali inakwenda na utekelezaji wa afua zote za ujenzi wa vituo vya afya angalau visogee karibu na wananchi, lakini pia afua za kupeleka watumishi wa Sekta ya Afya kwa awamu ili kuhakikisha sasa ikama ya watumishi katika vituo hivyo inatosheleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mafuwe, katika Jimbo la Hai tunafahamu vipo hivyo vituo vya afya ambavyo vimejengwa vipya, vimeongezeka lakini na Serikali inaendelea kupeleka wataalamu kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wanatimiza majukumu yao ipasavyo na wananchi wapate huduma bora zaidi za afya.
Name
Tunza Issa Malapo
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. SELEMANI J. ZEDI aliuliza: - Je, lini Serikali itamaliza tatizo la upungufu wa Watumishi wa Kada ya Afya – Bukene?
Supplementary Question 3
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Katika Mkoa wa Mtwara tumekuwa na tatizo kubwa sana la watumishi wa kada ya afya, lakini pamoja na mambo mengine ni tatizo la kuwahamisha watumishi bila kuwaleta wengine. Ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha wale ambao wanawaleta wanabaki kutuhudumia sisi watu wa Mtwara? (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Mtwara ni miongoni wa mikoa 10 ambayo Serikali tumeainisha kwamba ina changamoto kubwa zaidi ya upungufu wa watumishi wa kada ya afya, elimu, na pia watumishi wa kada nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kila kibali cha ajira, watumishi wengi zaidi wanapangiwa kwa kipaumbele kwenye mikoa hii 10 yenye upungufu mkubwa zaidi wa watumishi wa Sekta ya Afya. Kwa hiyo, kwanza ninaomba nikuhakikishie Mheshimiwa Tunza Malapo kwamba kila kibali cha ajira kitakapojitokeza tutahakikisha watumishi wengi zaidi wanapelekwa kwenye Mkoa wa Mtwara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ni kweli kumekuwa kuna wimbi la baadhi ya watumishi kuhamishwa kutoka kwenye halmashauri za vijijini au baadhi ya mikoa hasa hiyo 10 na kukimbilia maeneo ya mjini. Tumeweka utaratibu kwanza watumishi wanaohama lazima wapate kibali cha Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, TAMISEMI na kujiridhisha sababu za uhamisho na hasa sababu zile za ugonjwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, tumewaelekeza Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha wanajiridhisha pale watumishi wanapokuja na barua za uhamisho wajiridhishe kwamba barua hizo zimepitishwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI lakini pia wajiridhishe kama wameshatimiza ile miaka mitatu angalau baada ya kuajiriwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vinginevyo, lazima kuwe na maelekezo maalum kutoka kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili kudhibiti wimbi la watumishi kuhama maeneo ya pembezoni kwenda katika maeneo ya mijini.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved