Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Boniphace Mwita Getere
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda
Primary Question
MHE. BONIPHACE M. GETERE K.n.y. MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza: - Je, lini ujenzi wa Kituo cha Afya Rabour - Rorya utakamilika?
Supplementary Question 1
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru.
Swali la kwanza, tumekuwa na ujenzi wa vituo vya afya kwenye maeneo mbalimbali, lakini havikamiliki. Kituo cha Afya cha Rabour kimekamilika, lakini sasa hata vitanda tu, hakina. Sasa, ni lini Serikali itapeleka vitanda kwenye kituo hicho?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kituo cha Afya Unyari kimejengwa na wananchi, wamejitahidi sana kujenga theatre, lakini mpaka leo hiyo theatre bado hakijakamilika na wala hakina vitanda. Je, ni lini Serikali itapeleka vifaatiba kwenye Kituo cha Unyari na kumaliza hiyo theatre? (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea na ujenzi wa vituo vya afya. Ujenzi wa vituo hivi unafanyika kwa awamu. Tulianza na ujenzi wa majengo matano ya awamu ya kwanza, lakini tutakwenda kwenye ujenzi wa majengo yanayosalia awamu ya pili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, jambo la kwanza ninaomba nianze kwa kumhakikishia Mheshimiwa Getere kwamba Serikali inatambua kwamba katika majengo matano ya awamu ya kwanza ya Kituo cha Afya cha Rabour katika Halmashauri ya Rorya, majengo matatu yamekamilika, majengo mawili yapo zaidi ya 80% na tayari Serikali imetenga fedha katika mwaka wa fedha ujao shilingi milioni 226 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi na ukamilishaji wa majengo hayo ya awamu ya kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Halmashauri ya Rorya kuhusiana na vifaatiba na hususan vitanda, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amepeleka shilingi 1,150,000,000.00 ndani ya huu mwaka wa fedha na mwaka wa fedha uliopita katika Halmashauri ya Rorya. Fedha hiyo ni fedha nyingi inatosha kununua vitanda na vifaatiba vyote kwa ajili ya vituo vya afya na Hospitali ya Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba nitumie nafasi hii kumsisitiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Rorya kuhakikisha kwamba, fedha hiyo shilingi 1,150,000,000.00 ambayo tayari imepelekwa kwenye Halmashauri yake inunue vitanda na vifaatiba kwa ajili ya kuanza kutoa huduma katika kituo hiki cha afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusiana na Kituo cha Afya cha Unyari nayo pia katika Halmashauri ya Bunda Serikali ilishapeleka fedha kwa ajili ya vifaatiba. Ni wajibu wa Mkurugenzi, Mganga Mkuu wa Halmashauri na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara kuhakikisha wanaweka kipaumbele kuwasiliana na MSD na kupata vifaa hivyo mapema ili wodi hizo zianze kutoa huduma stahiki. (Makofi)
Name
Jackson Gedion Kiswaga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalenga
Primary Question
MHE. BONIPHACE M. GETERE K.n.y. MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza: - Je, lini ujenzi wa Kituo cha Afya Rabour - Rorya utakamilika?
Supplementary Question 2
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka miwili iliyopita tulijaza fomu za kupewa vituo vya kimkakati. Jimbo la Kalenga tulijaza katika Kata ya Kihanga. Wiki tatu zilizopita nilipigiwa simu kwamba wamepokea fedha na nikawaelekeza mahali pa Kwenda, lakini juzi ninapigiwa simu na Afisa Mipango kwamba fedha hiyo haikwenda Kalenga. Je, ni lini sasa Serikali italeta fedha kwenye Kituo cha Afya cha Kihanga na Waziri anaweza kunihakikishia hapa ninaweza kufuatilia na kunipatia majibu kwa nini nilipigiwa na sasa ninaambiwa kinyume chake? Ahsante sana.
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kufuatia maombi ya Waheshimiwa Wabunge wa Majimbo yote 214 kupata vituo vya afya vya kimkakati kwenye Kata ambazo ziliainishwa, Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Mheshimiwa Kiswaga aliwasilisha Kata ya Kihanga na tayari Mheshimiwa Rais ametenga fedha kwenye bajeti ya dharura zaidi ya shilingi 53,500,000,000.00 na tayari ameshatoa shilingi 30,000,000,000.00 kwa ajili ya majimbo 120 ya mwanzo awamu ya kwanza na baadaye tutamalizia yale majimbo 94 yanayobakia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Kiswaga kwamba, yale majimbo awamu ya kwanza 120 tayari yameshapokea fedha mpaka wiki iliyopita, lakini Jimbo la Kalenga lipo awamu ya pili na alipigiwa simu kwa sababu walikuwa wanajiridhisha kwamba amependekeza Kata ya Kihanga na Serikali inaendelea kutafuta hiyo fedha iliyobaki kwa ajili ya majimbo yote 94 liliwemo Jimbo la Kalenga kwa maana ya kupelekewa awamu ya pili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itatekeleza ahadi yake na kazi inaendelea. (Makofi)
Name
Ester Amos Bulaya
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. BONIPHACE M. GETERE K.n.y. MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza: - Je, lini ujenzi wa Kituo cha Afya Rabour - Rorya utakamilika?
Supplementary Question 3
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi. Halmashauri ya Mji wa Bunda tunajenga hospitali yetu, na hii ni mara ya pili, ninaliuliza hili swali humu Bungeni. Kuna shilingi milioni 800 ilikuja ikamezwa na Mheshimiwa Naibu Waziri anaijua ile hospitali ambayo tunaijenga katika Kata ya Bunda Store, sasa hivi ime-stuck. Je, ni lini Serikali itatuletea fedha ili tumalize hospitali yetu ya Halmashauri ya Mji wa Bunda ili wananchi wetu kwenye Halmashauri ya Mji wa Bunda wapate huduma zinazostahili? (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali ilipeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Bunda. Ni kweli pia kwamba Mheshimiwa Ester Bulaya amefuatilia mara kadhaa kwamba tupeleke fedha ile na hasa ile shilingi milioni 800 ambayo ilirejeshwa kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti ya 2015 baada ya kuvuka 30 Juni, katika huu mwaka wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimhakikishie tu kwamba, fedha ile ambayo ilirejeshwa, Serikali tumeitenga tena kwenye bajeti ya fedha ya 2025/2026, pia tumeongeza fedha kwa sababu tunafahamu shilingi milioni 800 haitatosha kukamilisha yale majengo. Kwa hiyo, ninaomba nikuhakikishie tu Mheshimiwa Bulaya kwamba, tunajua umuhimu wa kukamilisha hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Bunda na ndiyo maana fedha zilipelekwa, tumetenga kwenye mwaka wa fedha ujao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Jimbo la Bunda Mjini kwamba Serikali ni Sikivu, itahakikisha inapeleka fedha kwa ajili ya kukamilisha Hospitali ya Halmashauri ya Mji. (Makofi)
Name
Charles Muguta Kajege
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mwibara
Primary Question
MHE. BONIPHACE M. GETERE K.n.y. MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza: - Je, lini ujenzi wa Kituo cha Afya Rabour - Rorya utakamilika?
Supplementary Question 4
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Wakati wa ziara ya Waziri Mkuu katika Jimbo la Mwibara mwaka juzi alielekeza kuwa Kituo cha Afya kijengwe Bulamba.
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, vipo vituo vya afya ambavyo ni ahadi za viongozi wakuu wa Kitaifa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI katika mipango yetu tunaweka kipaumbele cha hali ya juu katika maeneo hayo ikiwemo katika Kata hiyo Bulambo ambayo ipo katika Jimbo la Mwibara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Kajenge kwamba, utekelezaji tayari tumeanza kwa kuingiza kwenye orodha ya vituo vya afya vya kimkakati na tutahakikisha kwamba fedha inapelekwa kwa ajili ya kujenga kituo hicho cha afya. (Makofi)