Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Maimuna Salum Mtanda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Newala Vijijini

Primary Question

MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kutumia redio za kijamii kutoa elimu ya matumizi bora ya viuatilifu katika zao la korosho?

Supplementary Question 1

MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipatia nafasi. Niipongeze Serikali pamoja na zile redio 11 za jamii ambazo zimekuwa zikifanya kazi mbalimbali ikiwemo matangazo kuhusu kuhuisha kwa kanzidata ya wakulima ili kujua kila mkulima na mahitaji yake kwenye shamba lake, lakini pia kutoa tahadhari ya ugonjwa kwa mfano ugonjwa wa blight na magonjwa mengineyo ambayo yanashambulia korosho. Sasa nilikuwa nina maswali mawili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; ni pamoja na kwamba tunatoa hayo matangazo na namna ya kudhibiti hayo magonjwa ya mikorosho, lakini ninataka kufahamu, kwa sababu wapuliziaji wengi ambao sisi tunawaita operator kule kwetu huwa wanakwenda shambani wakiwa hawana kinga yoyote ya kuwadhibiti kutokana na athari ambazo wanaweza kuzipata zitokanazo na zile sumu ambazo wanapulizia kwenye nikorosho. Je, kwa nini hizi redio sasa zisitumike pia kutoa elimu kwa wale ambao wanapulizia namna ya kujikinga na madhara yanayoweza kutokea kutokana na sumu zile wanazopuliza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; wewe ni shahidi pia, sisi wakulima wa korosho ukienda shamba utaokota bibo unakula lakini pia unaweza kutengeneza juisi, ukapika uji ukanywa, lakini ukitumia kilevi kinaitwa uraka, unakamua ile juisi unaichachusha kesho unakunywa kama pombe. Mabibo yale yanaathiriwa kwa kiasi kikubwa sana na zile sumu za maji ambazo zinapulizwa kwenye mikorosho. Je, Serikali imejipangaje kufanya utafiti wa kubaini ni kwa kiasi gani athari zinaweza kuwapata watumiaji wa mabibo au matunda haya kutokana na zile dawa ambazo zinapulizwa kwenye mabibo ili kuweza kudhibiti athari zisiwe kubwa huko mbele?

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Maimuna Mtanda, Mbunge wa Newala Vijijini kwa kazi nzuri anazozifanya kwa wananchi wake hususani kufuatilia masuala ya udhibiti wa afya kwa wakulima wake. Nimwondoe shaka tu kwamba, moja, tutaendelea kutumia hizi redio za jamii katika kuendelea kutoa elimu dhidi ya kujikinga na magonjwa ama matumizi mabaya ya viuatilifu ambayo yametokana na zao la korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tumeongeza fedha katika Kitengo chetu cha Mawasiliano na Habari kwa Umma ili kuweza kuzifikia hizo redio na zifanye mara kwa mara. Vilevile, tutawafikia Maafisa Ugani pamoja na Maafisa Kilimo katika ngazi za halmashauri ili waendelee kutoa elimu kwa wakulima wetu wa zao la korosho waweze kujikinga na hizi athari ambazo umezianisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili, tumekwishaelekeza watu wa TARI pamoja na TPHPA kuendelea kufanya tafiti kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunapata njia bora ambayo itasaidia kuondoa adha katika matumizi ya mabibo ambayo yanaweza kuwa yameathiriwa na matumizi ya dawa, kwa maana ya Viutatilifu vile ambavyo vimepulizwa.