Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Nusrat Shaaban Hanje
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza:- Je, Serikali inafanya maandalizi gani kuhakikisha nchi yetu inafanya vizuri katika Mashindano ya AFCON 2027?
Supplementary Question 1
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza ni kuhusiana na utaratibu wa kupata vijana kwa ajili ya kucheza kwenye timu ya Taifa. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba wanafanya scouting ili waweze kutambua vijana ambao wanafanya vizuri sana sana katika vilabu vidogo, vidogo huko mikoani, ukiangalia hata kwetu pale Ikungi Mashariki kuna timu ya Kikio Boys wanafanya vizuri sana pamoja na Matongo FC ya Ikungi; kwa hiyo wanafanya utaratibu gani ili na hawa vijana na wao waweze kupata nafasi ya kushiriki kuwepo kwenye timu ya Taifa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali langu la pili, kuhusiana na ubora wa viwanja vyetu nchini. Tumeona kwenye vyombo vya habari kwamba Serikali wanafanya marekebisho ya viwanja, ikiwemo Kiwanja cha Benjamin Mkapa. Tuliona wanabadilisha viti pale Benjami Mkapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe unafahamu kwamba pale kuna shida ya pitch. Yaani mvua ikinyesha ile pitch pale uwanja wa Taifa, Benjamin Mkapa inajaa maji. Sasa ninataka kufahamu, kwa nini Serikali wasishughulike na jambo la uwanja kwenye pitch? Pamoja na mambo mengine wanayoyafanya. Je, wanafanya utaratibu gani ili kuhakikisha kwamba ile pitch inakuwa bora kama ambavyo tunategemea, kwa sababu tunategemea uwanja wa Benjamin Mkapa sasa hivi?
Name
Hamis Mohamed Mwinjuma
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muheza
Answer
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Maswali mazuri kutoka kwa Mheshimiwa Nusrat Hanje. Hili la scouting Serikali kupitia Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania imekuwa ikiendelea kufanya scouting na kubainisha vijana ambao wana uwezo, wana vipaji vya kutosha kuchezea timu zetu mbalimbali za Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na hivi ninavyojibu haya maswali hapa, TFF tayari wana vijana takribani 150 katika Kituo cha Maendeleo ya Michezo kule Tanga na vijana hawa wamekusanywa kutoka maeneo mbalimbali ya mikoani ili kuhakikisha kwamba vipaji vyao siyo tu vinalelewa, lakini wanakwenda shule wakitokea pale kwenye Kituo chetu cha Maendeleo ya Mpira wa Miguu Mianjani Tanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakachofanya kwa vijana wake wa Ikungi, nitawaelekeza moja kwa moja TFF ili waende kwa ajili ya kufanya scouting kuangalia vipaji anavyosema vipo kule Ikungi na kuhakikisha kwamba kama kuna vijana wanafaa kwa ajili ya kuchezea timu zetu za Taifa na wao wanapata hii fursa ya kuitwa kwenye timu zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali lake la pili, hili la Benjamin Mkapa; tumekuwa tukifanya ukarabati wa Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa na maeneo yote ambayo tulikuwa tunafanya ukarabati hayakuwa yakihusisha eneo la pitch. Eneo la pitch lilikarabatiwa na CAF walipokuja kuendesha mechi ya African Football League kati ya Simba na Al Ahly mwaka juzi (2023) mwishoni na walitupatia miaka miwili kwa maandishi kwamba tunaweza kuitumia pitch ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengine ambayo tulikuwa tunayafanyia ukarabati yalikuwa yanahusisha viti kama anavyosema; ubao wa matangazo; mfumo wa umeme; ubadilishaji wa taa; mfumo wa hewa na mambo mengine mengi, lakini haikuwa inahusisha pitch. Sasa tumepata bahati mbaya wakati wa mechi ya Simba na Al Masry mvua kubwa ikanyesha na uwanja ukajaa maji. Serikali imechukua hatua za dharura kuhakikisha pitch ile inatengemaa kwa ajili ya mchezo wa fainali kati ya Simba na Berkane ambao utafanyika tarehe 27 ya mwezi huu wa tano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyosema tumeshaajiri Kampuni ya Kituruki na ipo kazini na watatukabidhi ile kazi yetu tarehe 15 ya mwezi huu, siku 12 kabla ya mechi ile. Kwa hiyo tunashughulika na jambo hili, na tutaiondoa pitch nzima baada ya Mashindano ya CHAN mwishoni mwa mwezi Agosti na kuweka pitch mpya wakati huo utakapofaa kwa vile ndivyo ambavyo tulikuwa tumeelekezwa na CAF kabla ya kupata hii bahati mbaya. Ninakushukuru.
Name
Rashid Abdallah Shangazi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlalo
Primary Question
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza:- Je, Serikali inafanya maandalizi gani kuhakikisha nchi yetu inafanya vizuri katika Mashindano ya AFCON 2027?
Supplementary Question 2
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kumekuwa na udhaifu na ucheleweshwaji mkubwa wa kiutendaji katika ukarabati unaoendelea kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, kiasi cha kutishia mchezo wa fainali kati ya Simba pamoja na Berkane, lakini pia kutishia mechi ya ufunguzi wa michuano ya CHAN ambayo itaanza mwezi Agosti. Je, Serikali inatoa commitment gani kuhakikisha kwamba mchezo huu muhimu wa fainali unachezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, lakini pia ufunguzi wa mashindano haya ya CHAN yanafanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa? Ahsante.
Name
Hamis Mohamed Mwinjuma
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muheza
Answer
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu swali lililopita la nyongeza la Mheshimiwa Hanje, commitment ya Serikali ni ileile kuhakikisha mechi hii ya fainali kati ya Simba na Berkane ya tarehe 27 ya mwezi huu, ambayo ni mechi ya kihistoria sana inachezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa. Hatutakuwa tayari kupokea kitu chochote chini ya hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimesema, Serikali imefanya kila inaloweza ikiwemo kuajiri kwa dharura mkandarasi mwenye uzoefu mkubwa katika masuala ya kutengeneza pitch ili kuhakikisha uwanja ule unatengemaa. Jana usiku mimi binafsi nilikuwa nina kikao kirefu cha kwenye simu na viongozo wa CAF akiwemo Rais Dkt. Motsepe’s ili kuhakikisha kwamba wanatusaidia na wao wenyewe wanatuletea consultants wa kimataifa, kuhakikisha tunashauriwa vilivyo namna ya kutunza pitch ile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe hofu Mheshimiwa Shangazi na wapenzi wengine wa mpira wa miguu wakiwemo wapenzi wa Simba, mechi ile itachezwa palepale na hakuna mahali itaenda. Tukio hili la kihistoria litafanyika mbele ya macho yao wakiwa wanalishuhudia. Ahsante. (Makofi)
Name
Joseph Michael Mkundi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ukerewe
Primary Question
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza:- Je, Serikali inafanya maandalizi gani kuhakikisha nchi yetu inafanya vizuri katika Mashindano ya AFCON 2027?
Supplementary Question 3
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni kwa nini Uwanja wa CCM Kirumba usifanyiwe matengenezo ili ukidhi vigezo vya kutumika kwa michezo ya AFCON, 2027? Ninashukuru.
Name
Hamis Mohamed Mwinjuma
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muheza
Answer
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna udhibiti wa kwenye idadi ya viwanja ambavyo vinaweza kutumika kwa ajili ya michezo ya AFCON. Hata hivyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Uwanja wa CCM Kirumba ni miongoni mwa viwanja ambavyo viko katika mpango wetu. Tunaanzisha Sports Infrastructure Management Agency kwa ajili ya kutunza viwanja hivi. Majadiliano yanaendelea kati ya wamiliki wa Uwanja wa CCM Kirumba na Serikali ili kuhakikisha kwamba wanatukabidhi kwa makubaliano rasmi ambayo yatakuwa hayampi hasara mtu yeyote na kuhakikisha kwamba vile viwanja vinatengenezwa kwa ajili ya kuendelea kutengeneza miundombinu mingi zaidi ya michezo nchini. Ni miongoni mwa viwanja vitano vya awali, ambavyo tuna mpango wa kuvifanyia ukarabati mkubwa na kuviweka katika kiwango cha kimataifa kwa ajili ya kutumika wakati wowote vitakapohitajika.
Name
Priscus Jacob Tarimo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Mjini
Primary Question
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza:- Je, Serikali inafanya maandalizi gani kuhakikisha nchi yetu inafanya vizuri katika Mashindano ya AFCON 2027?
Supplementary Question 4
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango gani ili faida zinazotokana na mashindano haya ziweze kufika maeneo mengi kwa kuhakikisha inaweka viwanja vya mazoezi katika miji iliyopo karibu na maeneo ambayo michezo inachezwa kwa ajili ya kuweka kambi kwa timu zinazoshiriki?
Name
Hamis Mohamed Mwinjuma
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muheza
Answer
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, matwaka ya CAF ni kwamba kila mji ambao mashindano ya AFCON yatakuwa yanachezwa unatakiwa kuwa na viwanja vitano vya mazoezi. Sasa kwa mahali ambapo Mheshimiwa Priscus Tarimo anatoka, Moshi ni karibu sana na ni moja ya miji ambayo mashindano haya yanachezwa ambayo ni Arusha. Ninaomba niongee na Mheshimiwa Priscus baada ya Kikao hiki cha Bunge ili kuona kama matakwa ya CAF yanaweza kuturuhusu kuweka moja ya viwanja vya mazoezi Jijini Moshi badala ya kuweka vyote vitano Arusha.