Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Eng. Stella Martin Manyanya
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nyasa
Primary Question
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza:- Je, hatua gani imefikiwa kupeleka umeme Kitongoji cha Songea Pori na Nindi vinavyopakana na Msumbiji kama ilivyoahidiwa na Serikali?
Supplementary Question 1
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninashukuru kwa majibu haya mazuri ya matumaini. Katika miradi hii ya vitongoji inayoendelea kama ambavyo niliongelea mara ya mwisho kwenye swali langu la nyongeza, kasi yake bado ni ndogo sana sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba umetoa maelekezo na wakandarasi, nimeona sasa wameanza kuripoti lakini kasi yao ni ndogo sana. Nini jitihada za Serikali za kuhakikisha kwamba wakandarasi hao wanaongeza makundi ya kutosha kuweza kukabili ule muda walioupoteza ili watu waweze kupata umeme katika Wilaya ya Nyasa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kwa kuwa wakati unaenda Nindi utakipita Kitongoji cha Magugu kwanza, je, Serikali itasaidia kukifanya na hicho kitongoji nacho kipate umeme wakati huo tunapeleka Nindi? (Makofi)
Name
Judith Salvio Kapinga
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza Mheshimiwa Engineer Stella Manyanya kwa kazi nzuri anayoifanya katika Jimbo lake na pia ninamshukuru kwa maswali haya mawili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na kasi ndogo ya mkandarasi ni kweli mkandarasi ambaye anatekeleza mradi huu katika Jimbo la Nyasa anaitwa MF. Pia, ni kweli kasi yake ni ndogo kwa sababu hatekelezi tu katika Jimbo la Nyasa, lakini pamoja na majimbo mengine vilevile.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshakaa na mkandarasi kwa siku ya juzi na tumeshakubaliana kwamba aweke wakandarasi wadogo (sub-contractors) watatu ili waweze kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi katika maeneo ambayo amepewa mkandarasi ikiwemo Jimbo la Nyasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tumeshachukua hatua za ziada za kumtaka mkandarasi aongeze kasi kupitia kuweka ma-sub-contractor hawa ambao kwa kweli tutawasimamia kwa weledi mkubwa sana kuhakikisha kasi ya miradi katika Jimbo la Nyasa inaendelea kuimarika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na Kitongoji cha Magugu, katika mradi huu ambao unakuja kupeleka umeme katika vitongoji, Jimbo la Nyasa litapelekewa takribani vitongoji 91. Kwa hiyo, tutaangalia katika orodha ile kama Kitongoji cha Magugu pia hakipo, basi tutaangalia kwa hatua zinazofuata namna ya kuwafikishia na Wananchi wa Kitongoji cha Magugu umeme ili na wenyewe waweze kunufaika na kuongeza tija katika shughuli zao za kiuchumi na kijamii.
Name
Aida Joseph Khenani
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Nkasi Kaskazini
Primary Question
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza:- Je, hatua gani imefikiwa kupeleka umeme Kitongoji cha Songea Pori na Nindi vinavyopakana na Msumbiji kama ilivyoahidiwa na Serikali?
Supplementary Question 2
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipatia nafasi. Mkandarasi aliyepewa kazi ya kupeleka umeme kwenye vitongoji vinavyozunguka Ziwa Tanganyika, mradi huo umekuwa unasuasua sana. Nini kauli ya Serikali ili wananchi waweze kupata huduma hiyo?
Name
Judith Salvio Kapinga
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, katika utekelezaji wetu wa miradi ya vitongoji, kwanza tumehakikisha tunawapata wakandarasi wenye weledi. Hata hivyo, kwa mara zote kwa wakandarasi ambao wamesuasua Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu amekuwa akiwaagiza mamlaka ambazo zinasimamia ikiwemo Wakala wetu wa Nishati Vijijini kuhakikisha wakandarasi hawa wanaendeleza kazi katika vijiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa suala hili la mkandarasi huyu ambaye anapeleka umeme katika vitongoji vilivyomo pembezoni mwa Ziwa Tanganyika, ninaomba kwa niaba ya Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu nimwelekeze Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Nishati Vijijini achukue jambo hilo alifanyie kazi kwa haraka, amsimamie mkandarasi na kufanya jitihada za ziada pamoja na mkandarasi kuhakikisha mradi huu unatekelezeka kwa kasi na wananchi ambao wanazunguka Ziwa Tanganyika ambao wako katika wigo wa mradi huu wanufaike na mradi huo.
Name
Christopher Olonyokie Ole-Sendeka
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Simanjiro
Primary Question
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza:- Je, hatua gani imefikiwa kupeleka umeme Kitongoji cha Songea Pori na Nindi vinavyopakana na Msumbiji kama ilivyoahidiwa na Serikali?
Supplementary Question 3
MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali. Kwa kuwa jiografia ya Wilaya ya Simanjiro, umbali kutoka kitongoji kimoja kwenda kingine, upo uwezekano ikawa ni zaidi ya kilometa 10 katika vijiji vingi vya wilaya hiyo, je, Serikali inaweka mpango gani kuhakikisha kwamba maeneo ya vijiji na vitongoji ambavyo viko mbali kutoka kimoja kwenda kingine na vyenyewe vinapata huduma ya umeme huu wa vitongoji? (Makofi)
Name
Judith Salvio Kapinga
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru pia kwa swali zuri la Mheshimiwa Mbunge. Kwa miradi hii ya sasa ya vitongoji, tumeenda kwa vigezo vya ziada, ndiyo maana kile kigezo cha kwamba tunatoa sawasawa katika kila jimbo katika miradi hii hatujafanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza tumeangalia ukubwa wa jimbo husika na vilevile tumeangalia ukubwa wa vitongoji katika jimbo husika pamoja na mahitaji ya kiuchumi na kijamii katika jimbo husika vilevile. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, mtaona utofauti katika miradi hii inayokuja ya vitongoji kwa sababu tumeangalia vigezo vya ziada kutokana na mahitaji ya jimbo husika na ndiyo maana kuna majimbo makubwa yatapata vitongoji vingi zaidi na yale ambayo hata miradi yao imetekelezwa sana kuliko majimbo mengine, basi tutapunguza idadi ya vitongoji.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo letu ni kuhakikisha kila jimbo linakuwa na vitongoji vingi zaidi ambavyo vina umeme ili kuweza kuweka usawa. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali imechukua hatua za ziada katika miradi hii ya vitongoji inayokuja. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved