Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ally Juma Makoa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kondoa Mjini

Primary Question

MHE. ALLY J. MAKOA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari katika Jimbo la Kondoa Mjini?

Supplementary Question 1

MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru Serikali kwa kutupatia hawa walimu wapya 33. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa uwiano wa walimu wetu kustaafu, kuhama na kwenda kujiendeleza kimasomo na sababu nyingine zinazopelekea kuweka upungufu wa walimu katika Majimbo yetu, unakuwa ni mkubwa kuliko wale wanaoajiriwa, je, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha inakabiliana na jambo hilo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Ni upi mkakati wa Serikali wa muda mfupi wa kuongeza walimu hasa ukizingatia kasi kubwa ya Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kujenga shule mpya pamoja na kuongeza miundombinu, pia ongezeko la wanafunzi katika shule zetu?

Mheshimiwa Naibu Spika, je, ni upi mkakati sasa wa muda mfupi wa Serikali kuhakikisha inakabiliana na upungufu mkubwa wa walimu? (Makofi)

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Ally Juma Makoa kwa swali lake hili zuri kabisa linalolenga kuboresha sekta ya elimu ya msingi na sekondari katika Jimbo lake la Kondoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nianze kwa kumjibu swali lake la kwanza kuhusiana na kasi ya walimu kuhama kutoka kwenye maeneo wanayopangiwa kutoa huduma hii muhimu ya elimu. Ninaomba nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ili kukabialiana na changamoto hii ambayo unakuta walimu wanapangwa katika vituo na wanaanza kuhama na kutengeneza mazingira ambayo kunakuwa sasa na upungufu wa walimu katika maeneo hususan kule vijijini katika maeneo ya pembezoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia mwongozo uliotolewa na Wizara ya Utumishi, imetoa maelekezo kwamba mtumishi anapopangwa katika kituo cha kazi, hatakuwa na sifa ya kuhama kwenye kituo hicho cha kazi mpaka awe ametimiza miaka mitatu na kuendelea. Kwa hiyo, huo ni mkakati mmoja ambao unatumika kwa ajili ya kuhakikisha inapunguza ile kasi ya watumishi ikiwemo walimu kuhama kutoka katika maeneo na hususan haya ya pembezoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya kufanyia kazi na hasa katika maeneo ya pembezoni, ili walimu waweze kupata utulivu na waweze kuridhika katika mazingira ya kazi wanayokuwa wamepangiwa na wasiweze kuhama na kusababisha upungufu ambao Mheshimiwa Mbunge anazungumzia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na mkakati wa muda mfupi wa Serikali wa kuendelea kuongeza walimu na hasa ukizingatia utekelezaji wa Mpango wa Elimu Bila Malipo ambao umetengeneza mazingira ya udahili, sasa udahili umeongezeka na Serikali ya Awamu ya Sita imetumia zaidi ya trilioni 5.1 kwa ajili ya kuimarisha hii sekta ya elimu, kwa kujenga madarasa na shule nyingi kwa ajili ya kuwapokea wanafunzi hawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunahitaji pia kuongeza nguvu katika upande wa upatikanaji wa walimu. Serikali kwanza inaajiri kama nilivyotangulia kusema, kwamba katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita (kipindi cha miaka minne) tayari walimu 45,742 wameajiriwa na kupangwa katika maeneo mbalimbali katika shule zetu hizi. Pia, mpaka wakati huu kimetoka kibali kingine cha walimu zaidi ya 9,000 ambao na wenyewe wataajiriwa kwa ajili ya kupangwa katika maeneo tofauti kwenda kuwafundisha wanafunzi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, kuna mikakati mingine kwa mfano ya kutumia teknolojia ya TEHAMA kutumia madarasa janja, kwa ufundishaji mubashara, kuajiri kwa mikataba, mamlaka zetu za Serikali za Mitaa kupitia mapato ya ndani inaajiri walimu hawa kwa mikataba ya muda na kutumia walimu wanaojitolea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali itaendelea na taratibu hizi, itaendelea kuongeza nguvu ili ile dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuendelea kuimarisha sekta muhimu ya Elimu ya Msingi na Elimu ya Sekondari iweze kutimia, tupate walimu wa kutosha kwa ajili ya kutoa elimu bora kwa wanafunzi wetu.

Name

Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ALLY J. MAKOA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari katika Jimbo la Kondoa Mjini?

Supplementary Question 2

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi kuuliza swali la nyongeza. Katika majibu ya msingi uliyojibu umesema kutakuwa kuna ajira mpya takribani 9,000. Hamwoni sasa umuhimu wa kuangalia wale wanaojitolea ili waweze kupata hiyo nafasi ya kuendelea kufundisha, hasa katika Wilaya ya Rungwe, Shule ya Ikuti kuna walimu zaidi ya tisa wanaojitolea? (Makofi)

Name

Yussuf Salim Hussein

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Chambani

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, kwa kweli amekuwa akifanya ufuatiliaji wa mara kwa mara kwenye masuala muhimu ya kimaendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la kutaka walimu wale wanaojitolea wapewe kipaumbele katika ajira hizi za walimu. Ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge suala hilo tayari lilichukuliwa na Wizara ya Utumishi na tayari linatengenezewa utaratibu wa kuanza kutengeneza kanzidata ya kutunza taarifa na kumbukumbu muhimu za walimu hawa wanaojitolea. Mwisho wa siku, dhamira ni kwamba hawa walimu wanaojitolea waweze kuwa na sifa ya ziada katika kupata ajira hizi ambazo zinatoka katika kila mwaka wa bajeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hata walimu wako hawa tisa katika Shule hii ya Rungwe aliowataja, ninadhani na wenyewe watakuwa wanufaika wa mipango na mikakati hii ya Serikali ya kuwatazama walimu wetu wanaojitolea.

Name

Hussein Nassor Amar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyang'hwale

Primary Question

MHE. ALLY J. MAKOA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari katika Jimbo la Kondoa Mjini?

Supplementary Question 3

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaipongeza Serikali kwa kuendelea kutoa vibali kwa ajili ya kuajiri walimu. Kwa kuwa katika ajira hii kutakuwa na walimu wa kike na wa kiume, Wilaya ya Nyang’hwale ina upungufu mkubwa sana wa walimu wa kike kwenye shule zetu za sekondari na msingi. Je, Serikali inajipangaje kutupatia walimu wa kike wengi kwenye Wilaya ya Nyang’hwale? (Makofi)

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Hussein Amar, amekuwa akiuliza maswali mengi ya kuendelea kuweka msukumo katika kuboresha Sekta hii muhimu ya Elimu Msingi na Sekondari.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali inaendelea na mkakati wake wa kuajiri walimu na kila mwaka wa bajeti fedha zinatengwa kwa ajili ya kuendelea kuajiri walimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha miaka minne hii ya Serikali ya Awamu ya Sita, tayari walimu 45,742 wameajiriwa na sasa kimetoka kibali kingine katika mwaka huu wa bajeti kwa ajili ya kuajiri walimu wengine zaidi ya 9,000. Serikali inaajiri walimu hawa wote kwa kuzingatia jinsia zote (walimu wanawake na walimu wanaume).

Mheshimiwa Naibu Spika, haya ni maombi mahususi kabisa kutoka kwako Mheshimiwa Mbunge kwamba unahitaji walimu wanawake katika shule zako za msingi na sekondari katika Wilaya ya Nyang’hwale na nimeyapokea na tutayaweka katika kipaumbele ili walimu wanapoajiriwa naye aweze kupata mgao wa walimu wanaume na pia walimu wanawake. (Makofi)

Name

Hassan Zidadu Kungu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Primary Question

MHE. ALLY J. MAKOA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari katika Jimbo la Kondoa Mjini?

Supplementary Question 4

MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kumekuwa na changamoto kubwa sana ya walimu kuhama kuliko kuhamia hasa wilaya za pembezoni kama ilivyokuwa Tunduru. Je, Serikali haioni haja sasa ya kutoa ajira ama kuajiri walimu ambao wako karibu na maeneo yale ili kuondoa changamoto hizi za walimu kuhama? (Makofi)

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Hassan Kungu kwa swali lake hili muhimu sana. Kama nilivyotangulia kusema, yanatokea mazingira ambayo watumishi wetu wa kada zote, lakini hapa nitazungumzia wa kada hii ya elimu wanaoomba uhamisho na mara nyingi inatokana na mazingira ya watumishi kupenda vituo vya mijini kuliko vituo vya pembezoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa Serikali wa kwanza kwa maelekezo yaliyotoka Wizara ya Utumishi ni kwamba mtumishi anapopangwa kwenye kituo hatakuwa na sifa ya kuhama kwenye kituo hicho cha kazi mpaka atimize miaka mitatu. Kwa hiyo, hiyo ni njia moja ya kudhibiti walimu kuhama.

Mheshimiwa Naibu Spika, njia nyingine ni kuboresha mazingira ya kazi ya walimu wetu, na ndiyo maana Serikali inajenga nyumba za walimu, lakini inapeleka huduma za umeme kupitia REA. Pia, unaona inapeleka huduma za maji, inaboresha miundombinu na huduma za msingi kabisa za kijamii ili walimu wetu wapate amani ya kufundisha katika vituo ambavyo viko pembezoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, njia nyingine ni kuhamisha watumishi ikiwemo hawa walimu kwa kutumia namna ya kubadilishana vituo kwamba mwalimu anapotaka kuhama kutoka kwenye kituo kimoja awe amepata mwenzake wa kubadilishana naye kituo, wabadilishane ili kutengeneza uwiano na kupunguza ule ukali wa walimu kuhama kutoka katika maeneo ya vijijini au tuseme pembezoni kwenda mjini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali inaendelea na jitihada ya kutengeneza haya mazingira ambayo maeneo ya pembezoni yasikose walimu kwa sababu walimu wanakuwa wanahama.

Name

Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Primary Question

MHE. ALLY J. MAKOA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari katika Jimbo la Kondoa Mjini?

Supplementary Question 5

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa upungufu wa walimu ni mkubwa, je, Serikali ina mpango gani wa kuleta walimu katika Jimbo la Mbulu Vijijini ambako walimu wengi ni wanaume tu, na tuna upungufu wa walimu wa kike? Ahsante.

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimpongeze Mheshimiwa Flatei Massay kwa swali lake hili zuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuajiri walimu kila mwaka wa bajeti. Inapoajiri walimu hawa huwa wanaajiriwa kwa jinsia zote, wanawake na wanaume. Kwa hiyo, haya ni maombi ya Mheshimiwa Mbunge, anatamani kupata walimu hawa wa jinsia, yaani wapate walimu wanawake.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imemsikia na katika ajira hizi za walimu zinazotangazwa, Serikali itazingatia na kuweka kipaumbele katika kumletea walimu ikiwemo walimu wanaume na walimu wanawake ili waweze kufundisha katika shule katika Jimbo lake la Mbulu Vijijini.

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Primary Question

MHE. ALLY J. MAKOA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari katika Jimbo la Kondoa Mjini?

Supplementary Question 6

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Tarime Vijijini kwenye shule nyingi za sekondari hakuna walimu wa kike, lakini imetokea shida nyingine kwamba wale walimu wa masomo ya arts wa sekondari wameelekezwa kwenda kufundisha shule za msingi. Sasa ni nini mpango wa Serikali kuondoa changamoto hizo mbili katika Jimbo la Tarime Vijijini?

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimpongeze Mheshimiwa Waitara ambaye amekuwa akiuliza maswali mengi katika upande huu na kufanya ufuatiliaji katika upande huu wa elimu msingi na hasa kwa maana ya kutaka kuona ustawi wa Sekta hii muhimu katika Jimbo lake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake ninaomba nimhakikishie kwamba Serikali inaendelea kuajiri walimu na Serikali inaajiri walimu kwa jinsia zote kwa sababu mchakato huu wa ajira ni wa ushindanishi, yaani walimu graduate, wanaomba ajira hizi kwa sifa zao, na wanapatiwa ajira hizi kutokana na kuwa wamefaulu ile michakato ya kuwapata kwa maana ya usaili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali itaendelea na utaratibu huo kupata walimu wanaume na walimu wanawake na itahakikisha kwamba inaendelea kuwapanga katika vituo mbalimbali. Pia, itazingatia haya maombi mahususi kabisa ya Mheshimiwa Mbunge katika Jimbo lake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na walimu hawa wa sekondari kwenda katika shule za msingi, Serikali ina wajibu wa msingi wa kutengeneza uwiano kufanya msawazo. Kuna maeneo ambayo yana uhitaji zaidi wa walimu na walimu hao wa sekondari wana sifa pia za kufundisha katika masomo ya shule za msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali itaendelea na mikakati mbalimbali lakini itapunguza changamoto hizo unazozitaja Mheshimiwa Mbunge. Baada ya kujibu maswali haya, tutakaa, tutazungumza ili tuone umahususi wa changamoto hii katika Jimbo lako ili tuweze kuifanyia kazi.

Name

Salma Rashid Kikwete

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mchinga

Primary Question

MHE. ALLY J. MAKOA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari katika Jimbo la Kondoa Mjini?

Supplementary Question 7

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, Mikoa yetu ya Kusini na hasa Mtwara na Lindi kuna tatizo la walimu na watumishi wengine, lakini kikubwa zaidi, watumishi wanapopangiwa katika maeneo yetu ya kazi kabla ya muda wa kuhama, wanataka kuondoka, yaani wanakuja kuchukua check number na wakishazipata hizo check number wanaondoka. Nini tamko au kauli ya Serikali kwa watumishi hao? (Makofi)

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimpongeze Mheshimiwa Salma Kikwete kwa swali lake hili zuri kabisa lenye maslahi mapana kwa siyo tu kwa mikoa ya kusini (Mtwara na Lindi), lakini kwa nchi nzima kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhahiri kabisa yanatokea mazingira ambayo watumishi na hususan hapa tunazungumzia walimu ambao wakipangwa katika vituo vya kazi na hasa katika mikoa ya pembezoni, wanakuwa wana hamu ya kuhama na kuhamia katika maeneo ya mjini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ili kukabiliana na changamoto hii ambayo inatengeneza mazingira ya kuwa na upungufu wa watumishi (upungufu wa walimu katika maeneo ya pembezoni) ilishatoa maelekezo kupitia Wizara ya Utumishi kwamba mtumishi hatakuwa na sifa ya kuhama katika kituo cha kazi alichopangiwa mpaka awe ametimiza angalau miaka mitatu katika utumishi kwenye kituo hicho cha kazi na Serikali inazingatia maelekezo hayo yaliyotolewa na Wizara ya Utumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nitumie nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuendelea kuwasisitiza Wakurugenzi wote wa Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa na Makatibu Tawala wa Mikoa waweze kuzingatia mwongozo huu. Hata hivyo, kwa sababu uhamisho unafanyika katika mifumo, Serikali inazingatia maelekezo haya yaliyotolewa na Wizara ya Utumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, namna nyingine ambayo Serikali inatumia kukabiliana na hii changamoto ya watumishi kuhama sana kutoka kwenye maeneo ya pembezoni na kutengeneza upungufu endelevu wa walimu ni kutumia namna ya walimu kubadilishana vituo kwamba mwalimu akitaka kuhama kutoka katika kituo kimoja awe amepata mwenzake wa kituo kingine waweze kubadilishana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali itaendelea na jitihada mbalimbali kwanza za kuendelea kuajiri walimu wawe wengi watosheleze kuwafundisha wanafunzi wetu. Pia, itazingatia misingi ambayo imewekwa ya kudhibiti uhamisho kutoka katika vituo vya pembezoni kwenda mijini ili maeneo ya pembezoni yapate walimu wa kutosha wa kuwafundisha wanafunzi wetu.

Name

Mussa Azzan Zungu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ilala

Primary Question

MHE. ALLY J. MAKOA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari katika Jimbo la Kondoa Mjini?

Supplementary Question 8

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, kila kata ina mwalimu. Kwa nini msiwatumie hawa vilevile kusaidia kupunguza ukwasi wa walimu kwenye shule zetu? Kwenye kila kata kuna Maafisa wa Elimu ambao wako stationed kwa Mtendaji wa Kata, wanafanya kazi zao pale, hawaendi kwenye madarasa. Kwa nini msiwatumie hawa nao kusaidia kupunguza kero ya upungufu wa walimu?

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nimepokea maelekezo yako, tutayafanyia kazi kama Serikali, ahsante.