Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
| Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
|---|---|---|---|---|---|---|
| 2025-2030 | Session 3 | Sitting 29 | Regional Administration and Local Government Authorities | Ofisi ya Waziri Mkuu-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) | 338 | 2026-05-14 |
Name
Mary Daniel Surati
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Serengeti
Primary Question
MHE. MARY D. SURATI aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha Halmashauri ya Serengeti inapata Service Levy kutokana na shughuli za utalii Wilayani humo?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Mary Daniel Surati, Mbunge wa Jimbo la Serengeti, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290 kifungu cha (6), (7), (8) na (9) vimebainisha vyanzo vya mapato vya Mamlaka za Serikali za Mitaa. Ushuru wa huduma ni miongoni mwa vyanzo vya mapato vilivyoainishwa katika Sheria hiyo kinachotozwa kwa kiwango cha 0.25% ya mauzo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti imekuwa na changamoto ya kukusanya ushuru huo kwa kuwa Kampuni nyingi za utalii zipo katika Halmashauri ya Jiji la Arusha hivyo kupelekea kampuni hizo kulipa ushuru wa huduma katika halmashauri hiyo licha ya utalii wenyewe kufanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetoa maelekezo ya mgawanyo wa ushuru huo kwa uwiano wa 60% kwa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ambapo shughuli za utalii hufanyika na 40% kwa Halmashauri ya Jiji la Arusha ambapo yapo makao makuu ya kampuni hizo. Hatua hii imepunguza mgongano wa utendaji katika ukusanyaji wa mapato yatokanayo na ushuru huo, pia takwimu za makusanyo zinaonesha kuwa mapato hayo yanaongezeka kila mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ipo kwenye hatua za mwisho za kuandaa Kanuni za Usimamizi na Ukusanyaji wa Ushuru wa Huduma. Pamoja na mambo mengine, Kanuni hizo zitaainisha namna bora ya kugawana mapato yatokanayo na ushuru wa huduma kati ya halmashauri moja na nyingine pale inapotokea migongano ya kimapato, ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved