Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
| Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
|---|---|---|---|---|---|---|
| 2025-2030 | Session 3 | Sitting 11 | Home Affairs | Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi | 123 | 2026-04-17 |
Name
Omar Issa Kombo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wingwi
Primary Question
MHE. OMARI ISSA KOMBO aliuliza: -
Je, Serikali imefikia hatua gani ya kuanza ujenzi wa Ofisi ya NIDA katika Makao Makuu ya Wilaya ya Micheweni?
Name
Mohammed Mahmoud Ayoub
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chaani
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Omar Issa Kombo, Mbunge wa Jimbo la Wingwi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imekamilisha kazi ya usanifu (design) wa michoro ya majengo na miundombinu ya TEHAMA, na inaendelea na taratibu za kumpata Mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa majengo ambapo zabuni kwa ajili ya kumpata Mkandarasi wa ujenzi huo imetangazwa na taratibu za manunuzi zinaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia Machi, 2026, Serikali kupitia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imekamilisha kazi ya tathmini ya hali ya mazingira (Environmental Impact Assessment) pamoja na uchunguzi wa hali ya udongo na ardhi (Geotechnical Investigation) katika viwanja hivyo kwa lengo la kuhakikisha usanifu na ujenzi wa ofisi hizo unafanyika kwa kuzingatia hali ya mazingira na udongo katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Mamlaka imelipa fidia kwa wananchi wa Wilaya ya Micheweni waliokuwa wakifanya shughuli zao katika kiwanja hicho kwa ajili ya kupisha ujenzi wa ofisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kukamilika kwa Mradi wa Vitambulisho vya Taifa awamu ya kwanza ambao ilihusisha ujenzi wa Kituo cha Kanzidata, Kituo cha Uokozi wakati wa Majanga na Ofisi za Usajili za Wilaya 13, Serikali kwa sasa inaendelea na utekelezaji wa awamu ya pili ya Mradi wa Vitambulisho vya Taifa (National ID System Expansion Project- Phase II) ambao unahusisha ujenzi wa Jengo la Makao Makuu Jijini Dodoma, ujenzi wa Kituo cha matengenezo ya vifaa vya TEHAMA na ujenzi wa Ofisi za Usajili katika Wilaya 31 ikiwemo wilaya ya Micheweni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, ujenzi huo pia utahusika na kuboresha na kuimarisha Mfumo wa Usajili na Utambuzi kwa kuongeza njia za uhakiki kwa kutumia alama ya mboni za macho na sura (Iris and Facial Recognition System) ili kuwa na alama za uhakika zaidi za kibaiolojia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved