Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2025-2030 Session 3 Sitting 11 Youth, Disabled, Labor and Employment Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira na Mahusiano 113 2026-04-17

Name

Dkt. Jasson Samson Rweikiza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Vijijini

Primary Question

MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:-

Je, lini Serikali itakuja na mpango wa kuhakikisha vijana wa nchi hii wanapata ajira za kutosha?

Name

Rahma Riyadh Kisuo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA MAHUSIANO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali ili kuhakikisha vijana wanapata ajira za kutosha. Miongoni mwa mikakati hiyo ni kubuni na kutekeleza programu mbalimbali zinazowawezesha vijana kujifunza kwa vitendo, kupitia sekta zinazozalisha ajira kwa wingi, pamoja na kufanya maboresho ya Sera mbalimbali, ikiwemo Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya Mwaka 2007 Toleo la Mwaka 2024 na Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la Mwaka 2023.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali inaendelea kukamilisha Mapitio ya Sera ya Taifa ya Ajira ya Mwaka 2008 kwa lengo la kukuza fursa za ajira. Vilevile, Serikali imekuwa ikiwezesha upatikanaji wa ajira kwa vijana kupitia ujenzi wa miundombinu ya miradi ya kimkakati inayochochea ukuaji wa uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kadhalika, Serikali imebuni na kutekeleza Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi kwa lengo la kuwezesha nguvukazi kupata ujuzi stahiki ili kumudu ushindani katika soko la ajira, ambapo hadi sasa Watanzania 168,657 wamenufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, Serikali inaratibu upatikanaji wa fursa za ajira nje ya nchi kwa njia rasmi, salama na zenye manufaa, ambapo vijana 6,367 wamenufaika katika mwaka 2025/2026. Sambamba na hayo, Serikali inatoa mikopo yenye masharti nafuu kwa vijana kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, pamoja na kuboresha Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura ya 410, inayotoa upendeleo wa 30% katika ununuzi wa Serikali kwa makundi maalum yakiwemo vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.